Rais Dkt.Mwinyi: Zanzibar sasa ni mwendo wa kazi na maendeleo

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetia saini Hati za Maelewano (MOU) zinazohusu Mpango Mkuu wa Upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa Bandari Shirikishi ya Uvuvi katika eneo la Mpiga Duri Unguja na Bandari ya Mkoani Pemba pamoja na Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa Nishati ya Gesi, anaripoti Mwandishi Diramakini
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa Saini ya Maelewano (MOU) Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa Nishati ya Gesi, (kulia kwa Rais) Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tangen Bw. Allan Kesseler na kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara Maji Nishati na Madini Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji (kushoto kwa Rais) hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Hafla ya utiaji saini hati za maelewano hayo imefanyika Februari 3, 2021 Ikulu jijini Zanzibar ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alishuhudia utiaji saini huo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya INTERTORCO yenye makao makuu yake mjini Madrid, Hispania.

Utiaji saini Hati ya Maelewano kuhusu kazi ya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa Nishati ya Gesi kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulisainiwa na Katibu Wizara ya Maji na Nishati, Dkt. Mngereza Mzee Miraji ambapo kwa upande wa Kampuni ya TANGEN & INTERTORCO GROUP ilisainiwa na Allan Kessler, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ambaye pia ni mkuu wa Kampuni ya Monitor Power System.

Aidha, kwa upande wa Hati ya Maelewano juu ya ujenzi wa Bandari ya uvuvi aliyesaini kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Katibu Mkuu, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe ambapo kutoka Kampuni ya TANGEN & INTERTORCO GROUP aliyesaini ni Mhandisi Michael Angaga ambaye ni mwakilishi wa kampuni hiyo.
Mwakilishi wa Kampuni ya Tangen & Intertorco Bw. Michael Angaga akitowa maekezo ya Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Mpiga Duri Unguja na Mkoani Pemba, wakati wa hafla hiyo iliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Mara baada ya utiaji saini hati hizo za maelewano, Rais Dkt. Mwinyi amepata fursa ya kuwahutubia wananchi waliofika katika hafla hiyo pamoja na wale waliokuwa wakifuatilia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambapo alisema kwamba Zanzibar imeanza safari mpya ya uchumi wa buluu.

Amesema kuwa, amefurahishwa na utiaji saini mradi huo mkubwa ambao unajumuisha bandari za uvuvi Unguja na Pemba ambao utahusisha ujenzi wa maegesho ya meli za uvuvi zenye gati tano kwa upande wa Mpigaduri Unguja na gati mbili katika bandari ya mkoani Pemba.

Aidha, amesema kuwa, kutakuwa na ununuzi wa meli za uvuvi kwa ajili ya uvuvi bahari kuu, ujenzi wa chelezo cha kujenga na kutengeneza meli, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza boti ndogo kwa wavuvi, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nyavu na zana za uvuvi.

Ujenzi mwingine ni kiwanda cha kusindika minofu ya sakaki, kiwanda cha kutengeneza mbolea itakayotokana na mabaki ya samaki, ujenzi wa soko la mnada wa samaki la Kimataifa, ujenzi wa majokofu mbalimbali ya kuhifadhia samaki, pamoja na Chuo Kikuu cha kufundishia uvuvi na ubaharia.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, mradi huo ukitekelezwa uchumi wa Zanzibar utakuwa kwa haraka sana ambapo Serikali itatekeleza mradi huo kwa ushrikiano na kampuni 12, kutoka nchi tano za Norway, Hispania, Ujerumani, Korea Kusini na Marekani.

Ametumia fursa hiyo kuwashukuru wabia hao ambao wameona haja ya kuiunga mkono Serikali kwa kuleta miradi mbalimbali hapa Zanzibar.

Amewasisitiza wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar kwani miradi bado iko mingi na Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa utaratibu wa aina tatu.

Amesema kuwa, mradi wa aina ya kwanza ni ile miradi ya miundombinu ya kibiashara kama ule uliotiwa saini wiki iliyopita ya mradi wa Bandari ya Mangapwani/Bumbwini pamoja na Bandari ya Mpigaduri ambayo itahusisha uvuvi.

Ameongeza kuwa, aina ya miradi inayotaka kuanzishwa itahitaji umeme mwingi na hivi sasa kwa upande wa Unguja ina umeme wa megawati 100 tu na Pemba megawati 20 tu ambapo ni vyema safari ya kuzalisha umeme mwingi ikaanza kwani umeme huo bado ni mdogo na hauendani na maendeleo yaliokusudiwa.

Rais amesema kuwa, Serikali imeona umuhimu wa kuingia makubaliano ya kuzalisha umeme, huku akieleza kwamba miradi hiyo ya biashara itakuwa ni ya ubia kati ya wawekezaji na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa, miradi mingine ni ile ya huduma kama vile barabara, elimu, afya na maji, hiyo itatekelezwa na Serikali ambapo itatafuta fedha kwa njia mbalimbali ikiwemo bajeti yake pamoja na mikopo ya masharti nafuu na ufadhili wa nchi rafiki.

Aina ya tatu amesema ni ile miradi itakayotekelezwa na sekta binafsi peke yake ambapo bado Zanzibar ina hitaji wawekezaji katika viwanda, hoteli pamoja na mambo mengi katika utalii na mambo mengineyo.

Rais Dkt.Mwinyi amefurahishwa na mradi huo kutoka kampuni hiyo ya INTERTORCO GROUP ambao wanakusudia kuwekeza Zanzibar dola za Kimarekani Bilioni 6.3 ambazo ni fedha nyingi huku Rais Dk. Mwinyi akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza Zanzibar.

Ameyataja maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji likiwemo eneo la Hoteli ya Bwawani, Mji Mkongwe wa Zanzibar, viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba kwani mradi kama huo wa Mpigaduri utahitaji usafiri wa kutosha hivyo ni vyema mipango ikapangwa juu ya uwekezaji katika viwanja vya ndege.

Ameongeza kuwa, tayari ameshapokea maombi kadhaa kutoka kwa wawekezaji ambao wanataka kuja kuwekeza katika viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba na kusisitiza kwamba kasi hiyo ikiendelea Zanzibar itapata miradi mikubwa sana ya kimaendeleo.

Amesema kuwa, wananchi ni vyema wakatambua kwamba miradi hiyo inawahusu kwani wageni wanaokuja kujenga miradi hiyo watahitaji makazi, hivyo ni vyema wakajenga nyumba kwa ajili ya kukodisha, hoteli, vyakula na mambo mengine mengi.

Amesema kuwa, miradi hiyo itasaidia kubadilisha hali ya maisha ya Wazanzibari kwa kiwango kikubwa na kuishukuru kampuni hiyo kwa kuonesha njia ya Sera ya Serikali ya uchumi wa buluu.

Sambamba na hayo, amesema kuwa mradi huo utasaidia hata wavuvi wadogo kwani tayari watakuwa na soko la uhakika ambapo pia, miradi hiyo italeta neema kwa wananchi wote hasa vijana ambao watachangamkia fursa nyingi za ajira zitakazotokana na miradi hiyo.

Pamoja na hayo, ameeleza kwamba yale yaliyokuwa yakisemwa sasa mwanga unaanza kuonekana na kueleza kwamba hatua kama hizo za utiaji saini hati za maelewano zitaendelea hatua ambayo itabadilisha uchumi wa Zanzibar.

Allan Kessler, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni TANGEN & INTERTORCO GROUP ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Monitor Power System amesema kuwa, Zanzibar ambayo ipo ndani ya Jamhuri ya Muuungano inaendelea kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Ameeleza kuwa, kuwepo kwa utulivu wa kisiasa, historia tajiri ya biashara ya Zanzibar inafanya kuwa ni eneo bora la usafirishaji wa biashara hasa ikizingatiwa kwamba umeme ni ufunguo wa ukuaji wa viwanda na kueleza azma ya kampuni hiyo kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Mwinyi za kuimarisha uchumi wa buluu.

Kessler ameeleza hatua na njia itakayotumika kupatikana kwa umeme huo wa gesi ambao utasaidia katika kuendeshea mradi huo pamoja na miradi mengine ambapo tayari miradi kama hiyo wameshaifanya katika nchi za Sudan, Somalia, Msumbiji, Eswatini na nchi nyinginezo.

Amesema kuwa, mradi huo utakuwa na kituo chake kikubwa huko Fumba ambapo bomba la gesi kutoka Tanzania Bara litaingiza kupitia baharini.

Nae Mwakilishi wa kampuni hiyo ya TANGEN & INTERTORCO GROUP, Mhandisi Michael Angaga amesema kuwa, ujenzi huo utaanza mara moja na wawekezaji wako tayari na kuweleza kushirikiana na serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara.

Amesema kuwa, ujenzi huo utatekelezwa pia, katika bandari ya Mkoani ambao umejumuisha miradi mingine kumi ambayo itaifanya Zanzibar kuwa sehemu maalum ya bandari ya uvuvi katika ukanda wa Afrika.

Amesema kuwa, hatua hiyo itapelekea wawekezaji na wafanyabiashara wengi kuvutiwa na kuja kufanya biashara Zanzibar badala ya kwenda nchini Dubai.

Utiaji saini miradi hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt.Mwinyi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar hasa uchumi wa Buluu sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina fursa maalum ya kuendeleza uchumi wake kupitia rasilimali za bahari.

Wiki iliyopita Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alishuhudia utiaji saini Hati ya Maelewano (MOU) kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari huko Mangapwani/Bumbwini
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzin Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa Saini ya Maelewano (MOU) na Kampuni ya Tangen &Intertorco Group ya Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Unguja na Mkoani Pemba, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dkt. Aboud Suleiman Jumbe (kushoto kwa Rais) na(kulia kwa Rais) Mwakilishi wa Kampuni ya Tangen &Intertorco Group Bw. Michael Angaga, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 3-2-2021.(Picha na Ikulu).

No comments

Powered by Blogger.