Rais Dkt.Mwinyi aongoza wananchi katika maziko ya Dkt.Mohamed Seif Khatib

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaongoza wananchi katika maziko ya marehemu Dkt. Mohamed Seif Khatib yaliyofanyika huko kijijini kwao Umbuji, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa,dini na Serikali pamoja na wananchi walihudhuria katika maziko hayo jana ambapo mapema Alhaj Dkt. Mwinyi aliungana nao katika sala ya kumuombea marehemu iliyosaliwa huko katika Masjidi Noor Muhammad (S.A.W), Mombasa kwa Mchina jijini Zanzibar.

Sheikh Mohammed Kassim akihitimisha kisomo cha Hitma na dua ya kumuombea Marehemu Mohammed Seif Khatib iliofanyika katika Masjid Noor Muhammad S.A.W. Mombasa kwa Mchina mwanzo, kabla ya kuusalia mwili wa Marehemu. (Picha na Ikulu).

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika maziko hayo ni Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, Rais wa Zanzibar Mstaafu wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu, Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wa Serikali, viongozi wa CCM na vyama vingine vya siasa.

Akisoma wasifu wa marehemu Dkt. Mohamed Seif Khatib huko Umbuji, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Khamis Abdalla Said alisema kuwa, marehemu alizaliwa tarehe 10 Januari 1951 huko kijijini kwao Umbuji, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Sheikh Mohammed Kassim (hayupo pichani) (kulia kwa Rais) Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaaf wa Zanzibar.Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein na (kushoto kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na Balozi Seif Ali Iddi Makamu wa Pili wa Rais Mstaaf na Mtoto wa Marehemu Seif Mohammed Seif. (Picha na Ikulu).

Amesema kuwa, marehemu Mohamed Seif Khatib ambaye kifo chake kilichotokea Februari 15,2021 huko katika Hospitali ya Al-rahma jijini Zanzibar baada ya kuugua kwa muda mfupi, marehemu ameoa na kubahatika kuwa na watoto sita.

Amesema kuwa, katika elimu, marehemu alijiendeleza sana kielimu na kutunukiwa shahada mbalimbali ikiwemo Shahada ya Ualimu ya Chuo cha Ualimu Nkrumah Zanzibar, Shahada ya Kwanza ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar-es Salaam, Shahada ya Uzamili katika Sanaa, London University SOAS na Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Katika uongozi wa Vijana, Naibu katibu Mkuu huyo amesema kuwa, Marehemu alianza uzoefu wa kazi kama Mwalimu wa Skuli mbalimbali akiwemo Mwalimu wa Skuli za Msingi, Mwalimu wa Skuli za Sekondari, Mkufunzi Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar pamoja na Mhadhiri wa muda, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Waumini wa Kiislam katika Sala ya kumuombea Marehemu Mohammed Seif Khatib ikiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi, iliofanyika katika Masjid Noor Muhammad SAW kwa mchina mwazo na (kulia kwa Rais) Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaaf wa Zanzibar Alhajj Dk. Mohamed Ali Shein na (kushoto kwa Rais) Katibu Ofisi ya Mufti Mkuu Sheikh Abdalla Talib na Alhajj Balozi Seif Ali Iddi Makamu wa Pili wa Rais Mstaaf, wakishiriki katika Sala ya kuusalia mwili wa marehemu.

Kwa upande wa uongozi katika wizara mbalimbali kuanzia mwaka 1988 hadi 2010, Marehemu aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ofisi ya Makamu wa Rais anaeshughulikia Mambo ya Muungano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na Waziri wa Mambo ya Ndani, Ofisi ya Waziri Mkuu (Habari na Siasa).

Naibu Katibu Mkuu huyo akisoma Wasfu huo alieleza kwamba kwa upande wa uzoefu katika Siasa, Marehemu aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Uzini kuanzia mwaka 1988 hadi 2015, Mjumbe wa NEC, CCM kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 2017, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa CCM (Idara ya Siasa na Uenezi kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 20170.
Vijana wa UVCCM wakiwa wamebeka jeneza likiwa na mwili wa marehemu Mohammed Seif Khatib, wakielekea katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya maziko yake yaliofanyika Kijijini kwao Umbuji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Sambamba na hayo, kwa maelezo ya Naibu katibu Mkuu huyo, marehemu ameandika vitabu mbalimbali kama vile, Fungate ya Uhuru, Wasaka Tonge, Utenzi wa Ukombozi, Chanjo, Vifaru Weusi na Kipanga ambapo pia, ana miswada ambayo haijachapishwa.

Pia, amesema kuwa Marehemu amesimamia wanafunzi wa Uzamili na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na kutunga nyimbo mbalimbali za taarabu na kuandika makala nyingi za Kiswahili.

Pamoja na hayo, Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba Marehemu vile vile alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar kuanzia mwaka 2014 hadi kufariki kwake lakini pia, alikuwa Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiweka udongo katika kaburi la Marehemu Mohammed Seif Khatib, wakati wa maziko yake yaliofanyika Kijijini kwao Umbuji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika wasifu huo pia, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa marehemu alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo waliochukua Uzamivu (PhD ya Kiswahili) hapa nchini.

Halikadhalika,Wasifu huo ulieleza kwamba Marehemu Dkt. Mohamed Seif Khatib ameacha athari kubwa kwenye lugha ya Kiswahili.Inalilahi waina ilaihi Rajiun, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amin.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news