Rais Magufuli aitaka Wizara ya Katiba na Sheria kutoa ajira alizotoa kibali

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ameishangaa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutotangaza nafasi za kazi licha ya kuwapa kibali cha kuajiri watumishi 200, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Zepharine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzaia kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino Februari 2, 2021. (Picha na Ikulu).

Ameelezea kutofurahishwa na ucheleweshaji wa mambo unaofanywa na wizara hiyo na amemuagiza Waziri Dkt.Mwigulu Nchemba kufuatilia na kuhakikisha mchakato wa kuwaajiri watumishi hao wa Mahakama ambao kibali cha kuajiriwa kwao kilishatoka wanaajiriwa.

Dkt.Magufuli ameyasema hayo katika hafla ya kumuapisha Zephrine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Ikulu, Dkt.Moses Kusiluka, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na viongozi wa taasisi ambazo ni wadau wa karibu wa Mahakama.

“Nimekuwa nikitoa vibali kwa ajili ya watu kuajiriwa katika wizara mbalimbali, mwaka jana nilitoa 1,000 kwa madaktari na waliajiriwa, nilitoa vibali kwa walimu 800 ambao hawakuchukua mwezi waliajiriwa. Lazima tujiulize kwenye Wizara ya Katiba na sheria kuna tatizo mbona wizara nyingine wanafanya? Wao mwaka mzima, waziri yupo, Katibu Mkuu yupo na mwanasheria mkuu yupo,”amehoji Rais Dkt.Magufuli.

Galeba ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu aliapishwa baada ya kupandishwa cheo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Magufuli ikiwa ni kutambua mchango wake wa kuthamini lugha ya Kiswahili ambapo alitumia lugha hiyo kutoa hukumu ya kesi ya mapitio namba 23/2020 kati mgodi wa dhahabu wa North Mara na mwananchi Gerald Nzumbi.

Rais Magufuli amempongeza kwa mara nyingine Jaji Galeba kwa kupandishwa cheo na alimtaka kwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za Mahakama na kwa kumtanguliza Mungu mbele.

Ametoa wito kwa Mahakama na Wizara ya Katiba na Sheria kufanya mabadiliko ya sheria na mifumo ya Mahakama iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni na ambayo imesababisha hukumu za Mahakama kutolewa kwa lugha ya Kiingereza ambayo haifahamiki kwa Watanzania wengi, ili hukumu hizo zitolewe kwa lugha ya Kiswahili.

Rais Dkt.Magufuli amesema kuwa, hoja za kuwa Kiswahili hakina misamiati ya kutosha hazina mashiko kwa kuwa mwaka 1999 timu ya Wanasheria iliandika kamusi ya sheria na pia lugha hiyo inatumiwa na watu wengi,mataifa na taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya Kimataifa.

Pia katika maelezo yake, Rais Magufuli aliitaka wizara hiyo kurekebisha kasoro, “ni rahisi kusema mnahitaji watu wa aina gani awe IT au hakimu kisha mnatangaza nafasi. Shughulikieni hili.”

Ameitaka wizara hiyo kuharakisha mchakato wa kufanya mabadiliko ya Sheria ya mwaka 1984 (13) inayozuia Jaji au Hakimu kutotumia lugha ya Kiswahili kuandika hukumu.“Wale wanaohusika kufanya mabadiliko wafanye haraka ikiwezekana hata kwenye Bunge linaloendelea,”alisema Rais Dkt. Magufuli.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amemueleza Rais Dkt. John Magufuli kuwa Mahakama imeanza mchakato wa hukumu kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza.

Prof. Juma amesema, ingawa utaratibu huo hauwezi kwenda haraka kwa sababu baadhi ya nyaraka zipo kwa lugha ya Kiingereza, lakini kwa mamlaka aliokuwa nayo ameshaanza kugawa kanuni kwa majaji kuhusu mchakato huo.

“Baada ya miezi miwili au mitatu tutakuja na kanuni zaidi ya 50 zilizokuwa lugha ya Kiingereza na kuwekwa kwa Kiswahili. Lengo ni kesi ikija mahakamani ubishi usiwe kwenye tafsiri ya lugha, tubishane haki na siyo lugha,” amesema Jaji Juma.

Prof. Juma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli kwa kumteua Jaji Galeba akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza mzigo kwenye Mahakama ya Rufani nchini.

“Mahakama ya Rufani haina sifa nzuri, kuna mrundikano wa mashauri unaotokana na uchache wa majopo wa kuamua kesi zinazosajiliwa kila siku. Tunashukuru huyu mmoja uliyetupa bado kuna wengine,”amesema Prof.Juma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news