Rais Magufuli atangaza kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Kijazi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli anasikitika kutangaza kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John William Kijazi kilichotokea leo Februari 17,2021 saa 3:10 usiku akiwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma alikokuwa anapatiwa matibabu,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais Magufuli amesema taratibu za mazishi ya marehemu Balozi Kijazi zitatangazwa baadae.

Mungu amuweke mahali pema peponi. Amina

 Kuhusu Balozi Kijazi

Balozi Mhandisi John William Herbert Kijazi amekuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 - 2016 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.

Kabla ya kuwa Balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.

Aidha, kati ya mwaka 1996 hadi 2002,Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamiziwa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya wizara hiyo hiyo.

Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992. 

Hata hivyo, Balozi Mhandisi John Kijazi amemuoa Fransiscar Kijazi na pamoja wamejaliwa kuwa na watoto watatu ambao ni David, Emmanuel na Richard. 

Uongozi wa Kampuni ya Diramakini Business Limited ambao ni wamiliki wa mtandao huu wa www.diramakini.co.tz  unachukua nafasi hii kutoa salamu za pole kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kwa kuondokewa na mmoja wa watumishi wake muhimu ambao walikuwa nguzo kuu katika kufanikisha juhudi zake za kuwaletea maendeleo Watanzania.

Vivyo hivyo, tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kuondokewa na kiongozi huyo mahiri ambaye amekuwa mstari wa mbele kumsaidia bega kwa bega Rais wa Jamhuri kutimiza majukumu yake ya kuliletea Taifa maendeleo kila siku. Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu. Amen

BADA YA KUUAGA MWILI WA KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI JOHN KIJAZI JIJINI DODOMA

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AONGOZA MAPOKEZI YA MWILI WA BALOZI KIJAZI JIJINI DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Februari 18, 2021 ameongoza mapokezi ya mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. Pichani, Mheshimiwa Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali wailoshiriki katika kuupokea mwili huo wakimpa pole, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi ambaye alikuwa ni mmoja wa Wanafamilia na viongozi wa serikali waliosafiri pamoja na mwili wa marehemu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ukiwekwa katika gari wakati ulipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam kutoka jijini Dodoma, Februari 18, 2021. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliongoza mapokezi ya mwili marehemu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi likiondoka kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya mwili kuwasili uwanjani hapo Februari 18, 2021. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliongoza mapokezi ya mwili wa marehemu. (Piocha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 
 

RAIS DKT. MWINYI AMTUMIA RAIS MAGUFULI SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kufuatia kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John William Kijazi kilichotokea tarehe 17 Februari, 2021.

Balozi Kijazi amefariki dunia majira ya saa 3:10 usiku akiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Jijini Dodoma alikokuwa akipata matibabu.

Salamu hizo za rambirambi amezitoa kwa niaba ya wananchi wote wa Zanzibar na kueleza kwamba amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Balozi John William Kijazi.

Salamu hizo zilieleza kwamba yeye binafsi, familia yake pamoja na wananchi wa Zanzibar na wa Tanzania kwa ujumla wamesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo hicho.

“Namfahamu Balozi John William Kijazi kuwa ni kiongozi mchapa kazi mahiri ambaye alikuwa na mashirikiiano mazuri na wenziwe wote," alieleza Rais Dk. Mwinyi katika salamu hizo za rambirambi.

Aidha, kupitia salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu kuwapa moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba, familia, ndugu pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments

Powered by Blogger.