Rais Magufuli:Lipeni madeni yao ndani ya siku 30

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli amezipa mwezi mmoja taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na Jeshi la Magereza ili liweze kufanya shughuli zake za maendeleo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo Februari 4, 2021 wakati akizungumza katika uzinduzi wa ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dodoma. Rais amesema kuwa, watakaoidi kufanya hivyo apatiwe majina yao ili awakate moja kwa moja Hazina.

Aidha, Dkt.Magufuli amelitaka jeshi hilo wakati mwingine kutumia mamlaka waliyo nayo ili kuhakikisha wanaodaiwa wanalipa madeni yao.

Katika hatua nyingine ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kulipatia jeshi hilo kiasi cha shilingi bilioni 3.6 ili liweze kumalizia ujenzi wa ofisi hiyo ya Makao Makuu huku akieleza kufurahishwa na utendaji kazi wa jeshi hilo unaofanywa na Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee.
“Nimeyaona majengo ambayo nimeyatembelea mimi mwenyewe nina uhakika yangekuwa yametengenezwa na wengine tusingezungumzia sh.milioni 900 kwa sababu haijafika hata bilioni moja, lakini majengo haya yote yamekamilika na mengine yamesimama,asante sana.

 “Nina uhakika maaskari mtakubaliana na mimi nilifanya vizuri kufanya mabadiliko na kumuweka Mzee,kwa mwendo huu hamwezi mkakwama kwa sababu mimi napenda kuona matokeo, lakini siku za nyuma ilikuwa shida,hata sare mnazozizungumza Kamishana aliyetoka yeye ndio alikuwa msambazaji wa sare hizo kupitia mke wake.

“Nataka niwaleze ukweli,ukishaona hatua hiyo imefikia hapo ujue jeshi halipo nikabadilisha nikaweka mwingine naye hivyo hivyo mpole,nikaona bora nimpe ubalozi, kwa hiyo Mzee umefanya mabadiliko kwenye Jeshi nimefurahi sana,”amesema.

Amezungumzia kuhusu changamoto ya watumishi katika jeshi hilo huku akihoji wanataka watumishi wa aina gani wakati wanao nguvu kazi ya wafungwa wenye fani mbalimbali.

“Hapa mmeeleza kwamba mna changamoto ya watumishi,nashindwa kuelewa sijui mataka watumishi wa aina gani wakati mna wafungwa wenye utaalam wa kila fani,

“Kinachotakiwa ninyi ni kupanga utaratibu wa kuwatumia wafungwa kufanya shughuli mbalimbali kwani najua hapa wapo wanaojua kila kazi,"amesisitiza Dkt.Magufuli.
Pia amesema, wafungwa hao wakiwekewa utaratibu mzuri wanaweza kufanya shughuli za kilimo na kuwezesha kulisha jeshi hilo huku akisema ni aibu kuona mfungwa ambaye ametumia nguvu kufanya uhalifu halafu anafungwa na kulishwa chakula na wananchi.

Amesema, wafungwa hao hao watumike hata kushona hizo sare wanazosema ni changamoto kwao, lakini pia wakazalisha na ziada ya chakula ambacho kinaweza kulisha familia za watumishi wa jeshi hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameeleza uhaba wa magereza katika wilaya 51 nchini huku akieleza mafanikio lukuki yaliyofanywa na jeshi hilo.

Kamishna Jenerali Mzee amesema, ujenzi wa ofisi hiyo pamoja na majengo mengi umegharimu kiasi cha shilingi milioni 900  huku akimuomba Rais Magufuli kubadilisha matumizi ya kiasi cha shilingi bilioni 13 kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news