Serengeti, hifadhi ya kipekee yenye maajabu zaidi ya ujuavyo, nyumbu wazidi kuwa kivutio bora zaidi

Viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Serikali mkoani Mara wameendelea kuhamasisha Watanzania kutembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii yakiwemo matukio ya nyumbu yenye upekee wa aina yake.

Wakizungumza katika tukio la kuhamasisha utalii wa ndani na uhifadhi endelevu hifadhini humo jana, wamesema nyumbu wa Serengeti wana matukio mengi lakini yanayotia fora na kuvutia zaidi watalii wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania ni matatu yanayofanyika kwa nyakati tofauti.
Baadhi ya nyumbu waliokusanyika eneo la Barafu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama walivyokutwa na camera ya Mara Online News, jana Februari 21, 2021.

Matukio hayo ni uzaaji, upandanaji na uvukaji mito Grumeti na Mara ndani ya hifadhi hiyo iliyoshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kwa miaka miwili mfululizo (2019 na 2020).

Akizungumza katika eneo la Barafu ambalo ni miongoni mwa maeneo matatu ambako tukio la uzaaji wa nyumbu linaendelea, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema walianza kutangaza tukio hilo mwaka jana kuhamasisha utalii wa ndani na ushirikiano wa jamii katika kulinda ubora wa hifadhi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika eneo la Barafu.

“Mwaka jana tulijiwekea utaratibu wa kutembelea hapa [maeneo ya Barafu, Ndutu na Naabi] ambako nyumbu zaidi ya milioni moja na nusu hukusanyika hapa kila mwaka kwa ajili ya kuzaa.

“Tukio hili ni la pekee… tunafanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na mikoa jirani [Arusha na Simiyu] kuhakikisha kuwa urithi huu unaendelea kubaki katika hali yake ya asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

“Tumesema lazima Watanzania wahamasishwe kuthamini vilivyo vyao kwa kutembelea vivutio hivi, lakini pia wajue wana wajibu wa kushiriki kuvitunza ili tupate watalii wengi wa ndani na wa kigeni,” amesema Malima.
Sehemu ya maelfu ya nyumbu waliokusanyika katika eneo la Barafu kwa ajili ya uzaaji msimu huu.

Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kuwa mkakati wa uongozi wa Serikali na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka huu ni kuhamasisha utalii wa ndani sambamba na kuimarisha uhusiano na jamii inayozunguka hifadhi hiyo iweze kushiriki kikamilifu katika kuilinda na kuitunza.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Masana Mwishawa amesema ushirikiano wa dhati wanaoupata kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Malima, unawapa matumaini ya kufikia lengo la kutangaza tukio la uzaaji wa nyumbu liweze kuwavuta watalii wengi zaidi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Masana Mwishawa akieleza walivyojipanga kutumia tukio la uzaaji wa nyumbu kuhamasisha utalii wa ndani.

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Neema Molel amesema wameendelea kufanya vikao na wadau wa utalii wakiwamo wasafirishaji kwa ajili ya kuhamasisha Watanzania kutambua kuwa utalii ni kwa watu wote, siyo kwa wageni pekee.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Neema Molel akielezea mkakati wa kuhamasisha utalii wa ndani.

Akizungumzia uzaaji wa nyumbu, Mwikolojia wa Hifadhi hiyo, Gadiel Moshi amesema tukio hilo hufanyika kwa takriban siku 28 zinazohusisha miezi ya Februari na Machi kila mwaka.

Moshi amefafanua kuwa ndama wa nyumbu wanaozaliwa kwa siku ni kati ya 5,000 na 8,000, na wanaozaliwa hadi siku 28 zinakamilika ni wastani wa 600,000, huku idadi ya nyumbu waliopo hifadhini ni takriban milioni 1.5.
Mwikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Gadiel Moshi akizungumzia msimu wa uzaaji wa nyumbu.

“Katika kipindi hicho nyumbu hujikusanya na kuzaa pamoja ili kuongeza ulinzi wa ndama wanaozaliwa wasiwindwe na wanyamapori wengine,” amesema na kuongeza:

“Kama mnavyoona eneo hili ni la uwazi mkubwa unaowezesha nyumbu kutazama mbali na kuona adui, na lina virutubisho vya maziwa vinavyosaidia ndama kukua.”
Mmoja wa ndama wa nyumbu waliozaliwa msimu huu katika eneo la Barafu.

Kwa mujibu wa mwikolojia huyo, nyumbu hutembea umbali wa kilomita 800 kwenye mzunguko na kujikusanya katika meneo ya uwanda wa nyasi fupi ya Ndutu, Naabi na Barafu kwa ajili ya tukio la uzaaji Februari kila mwaka.

Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii wa Hifadhi hiyo, Tutindaga George amesema matukio ya nyumbu wa Serengeti ni mengi, hayaishii kwenye uzaaji.

Ameongeza kuwa inapofika Mei kila mwaka nyumbu zaidi ya 500,000 huenda kujikusanya eneo la Seronera lililopo katikati ya hifadhi hiyo kwa ajili ya kupandana.
Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii wa Hifadhi hiyo, Tutindaga George amesema matukio ya nyumbu ni miongoni mwa vivutio vikuu vya utalii katika hifadhi hiyo.

“Aidha, inapofika Juni kila mwaka makundi ya nyumbu hufanya tukio la kuvuka mto Grumeti na kisha mto Mara, matukio haya huvutia sana watalii wanaotembelea hifadhi hii. Watalii wa kigeni wengi wanatoka Marekani na mataifa ya Ulaya,” amesema mhifadhi huyo.

Kuhusu utalii wa ndani, Tutindaga amesema wanaendelea kuhamasisha na kuandaa taasisi na vikundi mbalimbali kutembelea hifadhi hiyo ambapo kupitia mpango wa ujirani mwema inawezesha wanafunzi kwenda kujifunza na kujionea shughuli za utalii na uhifadhi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Ulinzi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Davis Mushi amesema wameendelea kupunguza ujangili na kuimarisha usalama hifadhini.

“Tumeimarisha ulinzi… kwa miaka mitatu sasa hakuna mnyama mkubwa aliyeuawa hifadhini. Tunatumia ndege, magari, pikipiki na mbwa kufanya ulinzi. Ukiona wanyama wametulia hifadhini ni ishara kuwa ujangili umepungua,” ameeleza Mushi.
Mhifadhi Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Ulinzi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Davis Mushi akielezea wanavyoimarisha ulinzi na usalama hifadhini humo.

Ubora na usalama wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyosheheni vivutio lukuki vya aina yake likiwemo tukio la uzaaji wa nyumbu, vimeendelea kumpa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Malima, ujasiri wa kualika watalii kuitembelea kwa wingi na hivyo kupaisha mapato ambayo sehemu yake huelekezwa kuchangia uboreshaji wa miradi ya kijami katika vijiji vinavyoizunguka.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akitoa wito kwa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ajili ya kujifunza na kujionea vivutio lukuki likiwemo tukio la uzaaji wa nyumbu.

“Plan to visit Serengeti National Park, welcome to Serengeti,” amesisitiza Malima kwa lugha ya Kiingereza - akimaanisha “Panga kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, karibu Serengeti”._(Habari na picha zote na Mara Online News)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news