TAKUKURU: Tupeni taarifa za rushwa zikiwemo za ngono kazini

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imewataka waandishi wa habari na wadau kushiriki kikamilifu katika utoaji wa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotokea katika taasisi zao, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mwanza).

Hayo yameelezwa na Mwanasheria wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Wakili Maximillian Kyabona katika usiku wa waandishi wa habari na wadau ulioadhimishwa hivi karibuni katika ukumbi wa Gold Crest uliopo jijini Mwanza.

Kupitia hafla hiyo TAKUKURU Mkoa wa Mwanza pamoja na kushiriki, pia ilipata fursa ya kutoa elimu ya Sheria ya Utakatishaji Fedha Namba 423 ya Mwaka 2016 pamoja na kosa la rushwa ya ngono kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.

Akielimisha kuhusu sheria hiyo Wakili Kyabona amesema, Serikali imetunga Sheria hii ya Utakatishaji Fedha kwa lengo la kufuatilia fedha zote za Serikali na za wafadhili zinazoporwa na watu wachache kwa kutumia njia za ujanja kuficha ukweli wa namna zilivyopatikana.

Pia sheria hiyo inamgusa kila mmoja aidha awe anafahamu au asiwe anafahamu.

Hivyo amevitaka vyombo vya habari kama daraja la mawasiliano kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa muhimu, sahihi tena kwa wakati.

Amesema, kwa mujibu wa sheria hii ya Utakatishaji Fedha mtu yeyote anayejipatia fedha kwa njia za wizi, rushwa na makosa mengine ya kijinai hataachwa bila kufuatiliwa na fedha hizo zitafuatiliwa popote atakapokuwa amezificha.

Akizungumzia kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007, Wakili Kyabona amesema ni kosa kwa mtu mwenye mamlaka kutaka upendeleo wa kingono ili aweze au asiweze kufanya maamuzi ya jambo fulani ambalo ana mamlaka nalo.

Amesema, rushwa ya ngono ni changamoto katika tasnia ya habari hususani waandishi wa habari wanawake, hivyo waandishi wamehimizwa kuwatolea taarifa wale wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Wakili Kyabona amewataka waandishi wa habari na wadau wote wa mkoa wa Mwanza kuibua ubadhirifu wa fedha unaofanyika katika taasisi zao kwa kutoa taarifa ili TAKUKURU iweze kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Kupitia jukwaa hilo mwanasheria huyo wa TAKUKURU amewaeleza wadau kuhusu uwepo wa utaratibu wa TAKUKURU MOBILE, yaani TAKUKURU inayotembea kuwa ni moja kati ya mkakati wa TAKUKURU kwa mwaka 2021 wa kuhakikisha kuwa TAKUKURU inawafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao kwa lengo la kusikiliza pamoja na kutatua kero zao.

“Kwa mkoa wa Mwanza tumetenga siku ya Jumatano ya wiki ya pili ya mwezi kuwa siku maalumu kwa zoezi hili.

“TAKUKURU Mkoa wa Mwanza kwa mwaka 2021 itaendelea kutekeleza majukumu yake ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa mujibu wa sheria kwa kuchunguza makosa ya rushwa na kufuatilia fedha za Serikali, wafadhili pamoja na wananchi zinazofanyiwa ubadhirifu na kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,”amesema.

“Kwa pamoja tutashinda vita dhidi ya rushwa. Kwa taarifa za vitendo vya rushwa fika ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu nawe, tumia TAKUKURU APP, piga simu ya dharura namba 113 au tuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au Piga *113# fuata maelekezo. Huduma hii ni ya bure,”ameongeza.

No comments

Powered by Blogger.