TAKUKURU YAMFIKISHA MAHAKAMANI MWALIMU MKUU KWA MAKOSA YA RUSHWA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka imemfikisha mahakamani Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwanangwa Bw. BARAKA MWAMBIPILE MWANSASU (34) kwa makosa ya Rushwa kinyume na Kifungu cha 31 matumizi mabaya ya mamlaka, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Pia kifungu cha 28 (1) (3) ubadhirifu na ufujaji vifungu hivyo vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 makosa yaliyosomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 na marekebisho yake ya mwaka 2019.

Hayo yamebainishwa na FRANK MKILANYA ambaye ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza.

Ameeleza pia, Bwana BARAKA MWAMBIPILE MWANSASU (34) ameshtakiwa kwa kosa la kughushi nyaraka kinyume na Kifungu cha 333, 335, 337, pamoja na

Kosa la kuwasilisha nyaraka za uongo kinyume na kifungu cha 342 na 337 vifungu hivyo vyote vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na marekebisho yake ya mwaka 2019.

Awali ilidaiwa kwamba, mnamo mwaka 2018 shule ya msingi Mwanangwa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, iliingiziwa fedha kwenye akaunti ya shule na Wizara ya Elimu kiasi cha sh. 2,000,000 kwa ajili ya motisha kwa walimu kwa vile shule hiyo mwaka 2017 ilifanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba.

Hata hivyo, uchunguzi wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi ulibaini kwamba, baada ya wizara kuingiza fedha hizo, katika kipindi hicho cha mwaka 2018, Bwana BARAKA MWAMBIPILE MWANSASU (34) akiwa Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwanangwa aligushi muhtasari wa kamati ya shule na kuuwasilisha kwa Afisa Elimu Kata pamoja na Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Misungwi kwa lengo la kuonesha kuwa kamati ya shule ilikaa na kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo kiasi cha Sh. 2,000,000 ili ziweze kutumika.

Aidha baada ya kutimiza lengo lake hilo huku akijua kuwa anachokifanya ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi, aliweza kutoa fedha hizo sh. 2,000,000 na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.

Uchunguzi wa tuhuma hii dhidi ya mwalimu mkuu huyo umekamilika na mtuhumiwa jana Februari 10, 2021 amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi na kufunguliwa kesi namba ECC. 1/2021 ili kujibu mashtaka yanayomkabili.

Akisomewa mashtaka yake na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Bi. SAIDA SALUM mbele ya Hakimu Mkazi Mheshimiwa ERICK MARLEY, mtuhumiwa amekana mashtaka yote manne (4) yanayomkabili.

Aidha, kwa sasa Mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana na amepewa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja kusaini bondi yenye thamani ya Sh. 1,000,000.

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 25/02/2021 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

WITO

TAKUKURU Mkoa wa Mwanza inaendelea kuwahimiza watumishi na wananchi wote wa mkoa wa Mwanza kuwa waadilifu kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuepuka vitendo vya rushwa. Aidha wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili wahusika wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

PENDA NCHI YAKO, KATAA RUSHWA

Kwa taarifa za vitendo vya rushwa fika ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu nawe, tumia TAKUKURU APP, piga simu ya dharura namba 113 au tuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au Piga *113# fuata maelekezo huduma hii ni ya bure.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news