TAKUKURU yaokoa Milioni 73.7/- za udangayifu wa mauzo ya korosho hewa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi imeokoa sh. Milioni 73,666,484.00 zilizopatikana kwa udanganyifu wa mauzo ya korosho hewa, anaripoti Mwandishi Diramakini (Lindi).

Hayo yamebainishwa Februari 22, 2021 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Mhandisi Abnery J.Mganga

“Ndugu waandishi wa habari, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa ili kuimarisha utawala bora na kuhakikisha haki ina tamalaki. Leo tunatoa taarifa ya kufanikiwa kuokoa fedha kiasi cha Shilingi 73,666,484.00 zilizopatikana kwa njia za udanganyifu.
“Mtakumbuka mnamo tarehe 27/10/2020 wakati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa akifunga Kampeni za Uchaguzi Mkuu Wilayani Nachingwea, alipiga marufuku waendesha maghala kuwakata fedha wanunuzi wa mazao ya Korosho kwa maelezo kuwa, korosho inapokuwa ghalani hunyauka na kupungua uzito (unyaufu), lakini pamoja na marufuku hiyo Uchunguzi wetu umebaini baadhi ya waendesha maghala kuendelea kuwakata wanunuzi unyaufu hali hii imepelekea baadhi ya Makampuni ya ununuzi kukosa Mizigo ghalani licha ya kuwa wamelipia.

“Katika kuyafanyia kazi maelekezo hayo ya Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TAKUKURU mkoa wa Lindi imebaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya Makampuni yaliyopewa dhamana ya kuendesha maghala. Udanganyifu huu unatokana na kuwepo kwa Korosho zinazopatikana kwa kuwakata wanunuzi kitu kinachoitwa “unyaufu” kwenye Maghala yao, na kisha waendesha maghala kwa kushirikiana na viongozi wa AMCOS wasio waaminifu hutumia mwanya huo kughushi stakabadhi mbalimbali za kutoa korosho hizo ghalani au kuziuza kwa wanunuzi wengine,”amefafanua Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Mhandisi Abnery J.Mganga.

Mhandisi Mganga amesema kuwa, mnamo tarehe 29/01/2021 Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya NACHINGWEA mkoani Lindi kupitia vyanzo vyake vya siri ilipokea taarifa za njama na udanganyifu zilizofanywa katika Ghala Kuu la PACHANI linaloendeshwa na Kampuni ya Mafubilo General Supplies Ltd katika wilaya ya NACHINGWEA.

Amesema, baada ya kupokea taarifa hiyo Ofisi ya TAKUKURU ya Wilaya ya Nachingwea kwa kushirikiana na ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa LINDI ilianzisha uchunguzi kuhusiana na udanganyifu huo na kubaini kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafubilo General Supplies Ltd kwa kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vya Ukombozi na Ndomondo vya NACHINGWEA walikula njama na kughushi Stakabadhi za Wakulima (Cash Produce Receipt), pamoja na Stakabadhi za kupokelea Korosho kwenye Ghala Kuu (Warehouse Receipt), ili kuwawezesha kufanya udanganyifu kuwa walikuwa wamepokea tani 35 za Korosho kutoka kwa Wakulima wawili.

“Uchunguzi uliendelea na kubaini kuwa udanganyifu huo ulisababisha watu hao ambao kimsingi siyo wakulima wa korosho, kulipwa fedha za Korosho kiasi cha Shilingi 73,666,484.00 katika akaunti zao binafsi kinyume na sheria. Aidha, uchunguzi huu ulibaini kuwa baada ya watu hao kulipwa fedha hizo haramu, walihamisha fedha hizo zote kwenda kwenye akaunti binafsi ya Bw. Juma Bakari Saidi ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya Mafubilo General Supplies Ltd ambapo zilitakatishwa na kisha kutumika kwenye matumizi binafsi.

Vitendo hivi ni makosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Utakatishaji Fedha Haramu (AML) ya mwaka 2012.

“Pamoja na mambo mengine, Uchunguzi uliwahoji mashahidi na watuhumiwa ambao wote walikiri kuwa korosho zilizotajwa hazikuwahi kupokelewa kwenye ghala hilo, na hata kampuni za usafirishaji zinazotajwa kupakia na kusafirisha korosho hizo zimekiri kuwa hawakuwahi kusafirisha korosho hizo kwa kipindi hicho,”amefafanua Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa.

Amesema, ktika hatua ya kwanza watuhumiwa wote wamekiri kufanya udanganyifu huo na kuamua kurejesha fedha zote kiasi cha Shilingi 73,666,484.00 ambazo zimelipwa katika akaunti maalumu ya TAKUKURU ya Mkoa wa Lindi. Aidha kwakuwa vitendo vilivyofanywa na viongozi hawa ni makosa kwa mujibu wa sheria kama nilivyoeleza hapo awali, uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika ili kukamilisha taratibu nyingine za kisheria zitakazowezesha watuhumiwa wote kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha haramu.

“Ninapenda kutumia nafasi hii pia, kutoa onyo kali kwa viongozi wa makampuni yote yenye dhamana ya kuendesha maghala ya mazao katika mkoa wa Lindi, pamoja na viongozi wote wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) vilivyoko katika mkoa wetu wasio waaminifu kuacha mara moja vitendo hivi vya udanganyifu na wizi, ambavyo kimsingi vimekuwa vikisababisha dhuluma na kuwanyima haki zao wakulima wanyonge.

“TAKUKURU mkoa wa Lindi inaendelea kuwashukuru wananchi, vyombo vya Habari, pamoja na taasisi mbalimbali (binafsi na za serikali) katika Mkoa wa Lindi kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa ofisi yetu. Aidha, tunawaomba waendelee kutuunga mkono kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kutumia njia mbalimbali hususani kupitia simu yetu ya bure ya 113 kwani mapambano dhidi ya rushwa sio ya TAKUKURU peke yake bali ni ya jamii nzima kwa ujumla,”amesema Mhandisi Mganga ambaye ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news