TAKUKURU yawafikisha Mahakamani aliyekuwa Meneja Mkuu wa STAMIGOLD,wenzake watatu Kagera

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa KAGERA imewafikisha mahakamani aliyekuwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Taifa ya Madini (STAMIGOLD) na wenzake watatu mkoani Kagera,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamebainishwa Februari 19, 2021 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph.

"Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera tumeendelea kutekeleza majukumu yetu kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sheria namba 11 ya mwaka 2007.

Katika utekelezaji wa majukumu yetu tumeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya Rushwa wakiwemo waandishi wa habari, viongozi wa serkali na wananchi kwa ujumla. Aidha majukumu haya yametekelezwa katika wilaya zote zilizo chini ya Mkoa wa Kagera.

"Tunapenda kuujulisha umma kuwa mnamo tarehe 12/02/2021 tuliwafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo watuhumiwa wanne ambao ni watumishi wa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini - STAMIGOLD kwa makosa ya kujihusisha na vitendo dhidi ya Rushwa na matumizi mabaya ya ofisi chini ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na na Rushwa , namba 11 ya mwaka 2007 na wamefunguliwa Shauri la jinai lenye namba CC 12/2021.

"Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni hawa wafuatao; Dennis Joseph Sebugwao - ambaye alikuwa Meneja Mkuu (General Manager) wa Mgodi wa STAMIGOLD Co Ltd katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Bwire Kanyaranyara Eliaseph- ambaye alikuwa Afisa Manunuzi wa kampuni STAMIGOLD Co Ltd katika kipindi cha mwaka 2016/2017.

"Sadick Soud Kasuhya ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi cha Mgodi wa STAMIGOLD Co Ltd kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 na Clara Aaron Mwaikambo ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Fedha wa Kampuni ya STAMIGOLD Co Ltd,"amesema Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera.

Amesema, Uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Kagera umeweza kuthibitisha kuwa katika kipindi cha kuanzia 30/06/2016 hadi 31/12/2017 kwa nyakati tofauti wakiwa watumishi wa Kampuni ya STAMIGOLD CO. LTD ambayo ni Kampuni tanzu ya kampuni STAMICO (STATE MINING CORPORATION) yenye Makao Makuu yake katika Wilaya ya Biharamulo katika Mkoa wa Kagera walitumia vibaya nafasi zao na kusababisha Kampuni ya SUPERCORE kujipatia manufaa.

"Watuhumiwa wote kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa Kampuni ya STAMIGOLD kwa nafasi tofauti tofauti katika kipindi cha 30/06/2016 hadi 31/12/2017 walitumia vibaya nafasi zao na hivyo kupelekea kuingiwa kwa Mktababa baina ya STAMIGOLD CO LTD na kampuni ya SUPERCORE wenye thamani ya shilingi bilioni nne milioni mia sita ishirini na mbili elfu laki nne ( Shs 4,622,400,000/=) badala ya shilingi bilioni tatu milioni mia nne elfu tisini na sita elfu (Shs 3,496,000,000/=) na hivyo kupelekea kampuni ya SUPERCORE kujipatia manufaa ya jumla ya shilingi bilioni moja milioni mia moja ishirini na sita laki nne (Shs 1,126,400,000/=)

"Baada ya shauri hilo kufunguliwa, Mshitakiwa mmoja ambaye ni Clara Mwaikambo aliweza kupata dhamana na watuhumiwa wengine watatu waliobaki siku hiyo hawakuweza kutimiza masharti ya Dhamana. Hata hivyo washitakiwa wawili ambao ni Dennis Joseph Sebugwao na Bwire Kanyaranyara Eliaseph walifanikiwa kupata dhamana siku ya tarehe 16/02/2021 na Mshitakiwa Sadick Soud Kasuhya bado hajaweza kukidhi masharti ya dhamana hadi leo.

"Ikumbukwe kuwa maandiko matakatifu kutoka katika Vitabu vitakatifu hasa BIBILIA na QURAN yametamka bayana kuwa Rushwa ni dhambi, na yamekataza mtu yeyote kujihusisha na vitendo vya Rushwa kwa njia yoyote, hivyo kujihusisha na vitendo dhidi ya Rushwa ni kwenda kinyume na Makatazo ya Mwenyezi Mungu na ni kuharibu uhusiano baina yako ya Mwenyezi mungu.

"Ndugu zangu ni vyema ikaeleweka kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuchukua hatua kila anapoona kuna dalili ya vitendo vya rushwa kufanyika na ni vyema kila mmoja wetu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi zilizowekwa kwa maslahi mapana ya Taifa. Hivyo nitoe wito kwa Wananchi wote wa mkoa wa Kagera kuchukua hatua mahususi pale wanapoona kuna dalili au ukiukwaji wa sheria zetu za nchi au kuna viashiria vya uwepo wa vitendo vya rushwa,"amefafanua Mkuu huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news