Dodoma, Jumatano 24 Februari, 2021.
Magonjwa haya yanaweza kusababishwa na vimelea vya bakteria, virusi na fangasi huambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali ikiwemo hewa, kula au kunywa kitu ambacho siyo kisafi na salama.
Mifano ya magonjwa haya ni pamoja homa za mapafu (Nimonia), mafua, malaria, kuhara, kuhara damu, kipindipindu typhoid, dengue, na mengine mengi.
Baadhi ya magonjwa ya kuambukiza yanaenda na vipindi vya majira ya mwaka au kutokea kama mlipuko.
Ndugu Wananchi, tukiacha mwenendo huu wa magonjwa kila mwaka, kipindi hiki pia tumeshuhudia Dunia ikipambana na wimbi la pili la mlipuko wa ugonjwa wa COVID- 19.
Kwa msingi huu tunahitaji kuongeza kasi zaidi ya kuchukua tahadhari dhidi ya mwenendo huu wa magonjwa yote haya kwenye kipindi hiki kama Wizara ya Afya tunavyoelekeza.
Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya inayo miongozo ya kutosha ambayo imekuwa ikisambazwa na kuelimishwa na wataalamu wetu kupitia mifumo ya afya kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya kijiji.
Miongozo hii imetamka bayana uhusika wa wadau wote wa sekta na wizara zote, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi za Umma na Binafsi kuwa nani anahusika wapi katika kila mkakati wa udhibiti wa magonjwa haya.
Hivyo, kila mmoja kwa nafasi yake sasa achukue hatua na atimize wajibu wake.
Ndugu Wananchi, Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu wameshafanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa matamko ya kukumbusha na kuelimisha taifa juu ya mwelekeo wa tahadhari za kuchukua ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.
Vilevile, Viongozi wa Wizara ya Afya tumetoa matamko mbalimbali ya kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wananchi, Jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote yakiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ni la kila mmoja wetu.
Aidha, niwakumbushe viongozi wa Serikali na sekta binafsi, Viongozi wa Kijamii, Viongozi wa Dini wa Madhehebu mbalimbali ngazi zote tuache kusubiri matamko zaidi bali tuamke tuwajibike kila mmoja kwa nafasi yake.
Aidha, narudia tena kuzitaja bidhaa za tiba asili ambazo tulizitaja awali kuwa zimeshasajiliwa na baraza la tiba asili kwa ajili ya magonjwa yanayohusu mfumo wa hewa kuwa ni pamoja na bidhaa dawa (COVIDOL, NIMRCAF, PLANET++, BINGWA, COVOTANXA), Mafuta tete (UZIMA HERBAL DROPS, BUPIJI, EUCALYPTUS OIL, LEMONGRASS ESSENTIAL OIL).
Niwaombe Viongozi wote kuanzia Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri, Wataalamu wote Afya na Sekta zote sasa tubebe silaha zetu za miongozo ya afya, uzalendo, uthubutu na ujasiri twendeni tuongeze kasi zaidi ya utekelezaji kila mmoja kwa kadri ya eneo lake.
Kwa kutekeleza mikakati niliyoeleza hapo juu tutakuwa tunajikinga na kutibu hata magonjwa yasiyoambukiza hivyo, miili yetu itaziidi kuwa imara zaidi dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.
Ndugu Wananchi, Napenda kuwakumbusha kuwa, kama taifa tunazo ajenda nyingi za kufanyia kazi ili kuchochea kasi ya maendeleo.
Hivyo tushikamane kutekeleza yale tuliyokwisha pokea kutoka kwa viongozi wetu . Mheshimiwa Rais wetu kila siku anatukumbusha kuwa tuko kwenye vita ya uchumi hivyo tusimame imara kulinda Afya zetu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Ndugu Wananchi, Adui maradhi tunamjua na silaha za kumpiga tunazo na mara nyingi tulishampiga na tukamshinda hivyo tubebe silaha twende mstari wa mbele tukampige tena.
Silaha zetu ni kuzingatia miongozo yetu ya Afya na umoja wetu wa kuwajibika kwenye utekelezaji wa miongozo hiyo kila mmoja kwa nafasi yake.
Ni katika umoja wa kitaifa kwenye kukabiliana na changamoto mbalimbali ndiyo tutashinda. Tubebe maono, uthubutu na ujasiri wa Mheshimiwa Rais wetu tuondoe hofu tuchape kazi huku tukichukua tahadhari.
Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iko kwenye mwelekeo wa kuimarisha zaidi misingi ya afya bora kwa kujenga ushirikiano wa karibu zaidi na imara zaidi na sekta zote zinazobeba ajenda ya afya kwenye utekelezaji wao.
Lengo ni kumkabili adui maradhi kwa kusuka upya na kuimarisha zaidi mifumo na mikakati ya kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyoambukiza bila kusahau nafasi ya tiba asili.
Mwelekeo huu ni wa uwekezaji wa afya kwa vizazi vingi vijavyo katika taifa hili ambapo mtoto wa shule ya msingi anaanza kujengewa uwezo wa kupambanua changamoto za afya na mikakati ya kujikinga na maradhi.
Ndugu Wananchi, Nachukua fursa hii kuwapongeza Wizara na sekta zote pamoja na Wadau wote wakiwemo wananchi kwa kushirikiana vyema kwenye kuchochea na kuleta mabadiliko endelevu ya tabia kuelekea kwenye kulinda na kuimarisha afya.
Tuzidi kushirikiana daima. Nawapongeza Wataalamu wetu wa afya kwa kujitoa kwao daima katika kutetea afya za watanzania.
Kwenu Wajumbe wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA), nyie ndiyo nguzo ya maendeleo ya jamii kwa kuwa mnazo funguo za kubadilisha fikra za jamii.
Twendeni mstari wa mbele kwenye kuifikia jamii na kuchochea mabadiliko ya fikra ili wapokee miongozo ya afya na kuitekeleza bila kusukumwa. Mnayo nafasi yenu kwenye kufikia malengo ya afya ngazi zote.
Ndugu Wananchi, Viongozi na Wadau wote kwa ujumla, Wataalamu wa Wizara ya Afya kwa ushirikiano na sekta zote kuanzia leo hii muda huu wataanza kufanya ufuatiliaji wa kina wa utekelezaji wa matamko, miongozo na maelekezo yote ambayo yamekuwa yakitolewa.
Pale ambapo utekelezaji uko vizuri tutapongeza hadharani na pale ambapo utekelezaji uko dhaifu bila sababu za msingi tutachukua hatua stahiki za uwajibikaji kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
TUKO KWENYE VITA YA MARADHI YANAYOATHIRI UCHUMI NA VITA SIKU ZOTE SI LELEMAMA. HIVYO KILA MMOJA ASIMAME KWA NAFASI YAKE.