Tanzania yawasilisha ombi maalum Umoja wa Afrika

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini zimewasilisha ombi maalumu kwa Umoja wa Afrika kuzitambua rasmi njia zilizotumika na wapigania uhuru kutoka Dar es Salaam kupitia nchi mbalimbali Kusini mwa Bara la Afrika hadi Namibia kuwa urithi wa Kimataifa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ombi hilo limewasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini,Cyril Ramaphosa katika Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia mtandao na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Pia Tanzania imeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni sanaa,utamaduni na urithi.

Akiufunga mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi alisisitiza kuwa umoja, mshikamano na amani katika bara la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakayoliwezesha bara hilo kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali ilizonazo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news