TARURA INAVYOBORESHA MIUNDOMBINU MKOA WA RUVUMA

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), unaendelea kufanya matengenezo na maboresho ya miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko katika Mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuifanya miundombinu hiyo iwe katika hali nzuri kwa kipindi chote cha mwaka kwa lengo la kuwezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa na mazao yao kwa haraka na kwa gharama nafuu,wanaripoti Bebi Kapenya na Thereza Chimagu (TARURA).

Katika Mkoa wa Ruvuma ambao Makala hii inauangazia, TARURA imekuwa ikihakikisha miundombinu ya barabara hasa mashambani inapitika ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima yanafika sokoni haraka kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi.
Muonekano wa Barabara ya Tunduru-Seed Farm kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Km 1.25 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Mratibu wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Edward Lemelo anaeleza kuwa tangu TARURA ianzishwe hali ya barabara katika Mkoa wa Ruvuma asilimia 30 ya mtandao wa barabara una hali nzuri na hali ya wastani ambapo zinapitika mwaka mzima.

“Tumefanya matengenezo mengi kwa maana ya matengenezo ya Kawaida (Routine Maintenance) zaidi ya Km 1291.7, matengenezo ya Sehemu Korofi (Spot Improvement) sehemu zilizokuwa zinasumbua wananchi zaidi ya Km 540, tumefanya matengenezo ya Muda Maalum yaani matengenezo makubwa
(Periodic Maintenance) zaidi ya Km 665 pamoja na kujenga madaraja madogo na makalavati 633 katika barabara mbalimbali za TARURA kwenye Mkoa wetu,"anasema Mhandisi Lemelo.
Muonekano wa Barabara ya Katibu Tarafa-Ikulu Ndogo kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Mita 490 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Mhandisi Lemelo anaeleza kuwa TARURA Mkoa wa Ruvuma imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa kuanzia Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Wakala umejenga Daraja kubwa la Fundimbanga lenye urefu wa mita 45 kwa kutumia Shilingi Bilioni 1.5 na sasa wananchi wa eneo hilo wanapita bila shida tofauti na hapo awali.

“Ukitoka kwenye barabara kubwa kuna kijiji kinaitwa Tabora mpaka kufika kijiji cha Fundimbanga wananchi walikuwa hawawezi kutoka kwenye vijiji hivyo kufika mjini hasa kipindi cha masika, lakini tumewezesha wananchi kufikia barabara kubwa kwa kutumia daraja hilo ili waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kupeleka sokoni”, anasema Mratibu.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ambayo ni Halmashauri mpya, eneo hilo halikuwahi kuwa na lami lakini kwa kutumia fedha za Ahadi za Viongozi wamejenga Barabara ya Madaba-LITA Km 1 kwa kiwango cha Lami na kuweka taa za barabarani. Pia kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara wamejenga Barabara ya Kona Bar-NMB-Makalavati Juu kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Mita 750. Pia, wanaendelea na ujenzi wa Barabara ya Wino-Ifinga-Luhuji kwa kiwango cha Changarawe Km 15 ambapo ikikamilika itasaidia wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwani eneo hilo wanalima sana mazao ya maharage, mahindi, ndizi, mpunga na tangawizi.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, utekelezaji wa miradi mbalimbali umefanyika ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Peramiho-Lundusi Km 6.43 na Peramiho-Morogoro Km 7.34 zote kwa kiwango cha Lami, barabara hizo zimesaidia wananchi kutoka katika vijiji vya Morogoro na Peramiho kuweza kufikia hospitali ya Peramiho kwa urahisi zaidi, na kwa sasa wapo katika maandalizi ya ujenzi wa Daraja la Mto Muhukulu mradi ambao bado upo katika hatua ya Usanifu (Design) na ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wamejenga barabara kwa kiwango cha Lami Km 12.3 na kuweka taa za barabarani kwa kutumia Mradi wa Uimarishaji Halmashauri za Miji “Urban Local Government Strengthening Program” (ULGSP) mradi ambao umeweza kupendezesha Mji wa Songea, lakini pia kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara wamejenga Barabara ya Lami (Tunduru Seedfarm) Km 0.75, Barabara ya Pachanne-Mjimwema kwa kiwango cha Lami nyepesi Km 0.4 na Barabara ya Seedfarm kwa kiwango cha Changarawe Km 3 na pia wanaendelea kujenga Km 1 za Lami kila mwaka ili kuuboresha Mji.

Mhandisi Lemelo anasema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, wameweza kujenga Barabara ya Mbinga-Litoho kwa kiwango cha Lami Km 25 ambayo hapo awali ilikuwa na hali mbaya kwani wananchi walikuwa wanatembea wiki nzima kusafirisha mazao yao.
Muonekano wa Barabara ya Peramiho–Morogoro–Nakahuga kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Km 7.34 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

“Kuna sehemu inaitwa Litoho ambapo ni mpakani mwa Nyasa na Mbinga kule kuna wananchi wengi ambao ni wakulima wa mazao ya kahawa na ndizi walikuwa wanatumia wiki moja kuleta mazao yao mjini lakini baada ya kuweka Lami kwa sasa wanatumia dakika 30 tu kufika mjini na kuuza mazao yao kwa urahisi, kwa hiyo ujenzi wa barabara hii umesaidia sana wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kwa gharama nafuu”, anasema Mratibu.

Pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, wameweza kujenga Daraja kubwa la Tingi-Lulimbo-Mtuha na kufungua barabara Km 15 katika Barabara ya Tingi-Lulimbo-Mtuha ambayo imeweza kusaidia wananchi kuvuka kutoka Nyasa kwenda Wilaya ya Mbinga kwa kutumia njia fupi na kusafirisha mazao yao kwa haraka kupeleka sokoni, pia kwa kutumia fedha za Ahadi za Viongozi wametengeneza Lami Km 1 na kuweka taa za barabarani kwa lengo la kuuboresha Mji.

Aidha, wamejenga Barabara ya Tumbi-Mango-Kindili kwa kutumia zege (concrete strips) Km 15 sehemu ambayo ilikuwa korofi lakini baada ya ujenzi wa barabara hiyo imewasaidia wananchi kuzifikia huduma za afya kwa urahisi.

TARURA katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga kazi kubwa iliyofanyika ni matengenezo ya barabara ya Lipembe yenye urefu wa Km 32.61 kwa kiwango cha Changarawe ambapo hapo awali ilikuwa haipitiki lakini baada ya matengenezo hayo imeweza kusaidia wananchi katika suala la usafiri. Pia,
wamejenga Barabara ya Mpepai-Kihungu Km 16.50 na Pachasita-Tulila Km 10.66 kwa kiwango cha lami.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wameboresha Barabara iitwayo Libango–Kiburungutu-Mtumbatimaji kwa kiwango cha Changarawe Km 10 barabara ambayo inatoka katika kijiji cha Libango kuja mjini sehemu ambayo kuna wakulima wa mazao ya mahindi na ufuta na kusaidia wananchi hao kuvusha mazao yao kutoka mashambani hadi mjini kwenye masoko.
Muonekano wa sehemu ya Barabara kwa kiwango cha Lami zenye urefu wa km 12.3 zilizojengwa chini  ya Mradi wa Uimarishaji Halmashauri za Miji “Urban Local Government Strengthening Program” (ULGSP) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Mkazi wa Kijiji cha Fundimbanga Wilaya ya Tunduru Bw. Alto Luambano, anaipongeza TARURA kwa kutengeneza Daraja kubwa la Fundimbanga lenye Mita 45 ambalo limesaidia kusafirisha mazao na hivyo kufika sokoni kwa urahisi.

“Kabla ya ujenzi wa daraja hili, wananchi wa vijiji vya Tabora na Fundimbanga tulipata shida katika kusafirisha mazao yetu lakini TARURA wametuondolea hilo tatizo kwa kututengenezea daraja ili tuweze kufika barabara kubwa na kusafirisha mazao yetu kwa urahisi na kupeleka sokoni”, anasema Bw. Luambano.

Naye, Jeremiah Makelele ambaye ni mkulima wa zao la maharage Kata ya Wino Halmashauri ya Madaba, anasema katika Kata yao wanalima sana mazao ya maharage, mahindi, ndizi, mpunga, tangawizi pamoja na uvunaji wa mazao ya misitu, vilevile eneo hilo lina shughuli za kijamii kama vile shule na vituo vya afya, hivyo mahitaji ya miundombinu bora na ya uhakika ni muhimu sana na
anaipongeza TARURA kwa kuanza ujenzi wa Barabara ya Wino-Ifinga-Luhuji yenye urefu wa Km 15 kwa kiwango cha Changarawe ambayo itawasaidia kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Naye, Bi. Happy Sawali Mkazi wa Peramiho Wilaya ya Songea, anaipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kutengeneza ya Barabara ya Peramiho-Lundusi Km 6.43 na Peramiho-Morogoro Km 7.34 zote kwa kiwango cha Lami na kwamba barabara hizo zimerahisisha usafiri na kusaidia wananchi kutoka katika vijiji vya Morogoro na Peramiho kufikia hospitali ya Peramiho kwa urahisi.

Kwa upande wake Bw. Othman Ndunguru, Mkazi wa Kijiji cha Matutu Wilaya ya Mbinga, anasema anawashukuru TARURA kwa kujenga Barabara ya Mbinga- Litoho kwa kiwango cha Lami Km 25 kwani barabara hiyo ni muhimu kwavile inaunganisha Wilaya ya Nyasa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

“Barabara hii inatupunguzia umbali mrefu sisi wananchi ambao tulikuwa tunalazimika kuzunguka umbali mrefu kwenda Mbinga ambapo tulikuwa tunatumia wiki moja, lakini baada ya ujenzi wa barabara hii tunatumia dakika 30 tu kufika Mbinga, hivyo tunaishukuru sana TARURA kwa kututengenezea barabara hii na sasa tunasafirisha mazao yetu kwa urahisi”, anasema Bw.
Ndunguru.

Mkoa wa Ruvuma una mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa Km 7,143.7 ambao unahudumiwa na TARURA na kati ya hizo jumla ya Km 82.2 ni Barabara za Lami ambazo ni asilimia 1.2% ya mtandao mzima, jumla ya Km 937 ni Barabara za Changarawe ambazo ni asilimia 11.7% ya mtandao mzima na jumla ya Km 6,124.5 ni Barabara za Udongo ambazo ni asilimia 87.1% ya
mtandao mzima.

Post a Comment

0 Comments