TARURA inavyoendelea kutatua kero kwa wananchi mkoani Dodoma

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeendelea kutatua kero za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuendelea kufanya matengenezo na maboresho ya barabara pamoja na madaraja ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli za usafiri na usafirishaji kwa urahisi, wanaripoti Geofrey Kazaula na Erick Mwanakulya, Dodoma.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Posta – Ohea yenye urefu wa Km 1.12 iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma ikiwa imekamilika asilimia 100.

Miundombinu ya barabara pamoja na madaraja kwa kiasi kikubwa huathiriwa na mvua hasa pale mvua inaponyesha kupita kiasi kwa muda mrefu, mfano mvua zilizonyesha kwa mwaka wa fedha 2019/20 zilichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu madaraja na barabara katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, mvua hizo zilisababisha kuharibika kwa daraja lililopo Mto Bubu, Kata ya Thawi katika barabara ya Changaa – Thawi yenye urefu wa kilomita 14.9.
Muonekano wa Ujenzi wa Daraja la Miembeni lenye urefu wa Meta 25 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma.

Kuharibika kwa daraja hilo kulisababisha kero kubwa kwa wananchi ambao walishindwa kwenda hospitalini pamoja na shuleni baada ya mawasiliano kukatika kutokana na mvua hizo, TARURA ilitenga kiasi cha shilingi milioni 383 ili kurejesha mawasiliano.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Mhandisi Brighton Kimaro ambaye ni Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, ameeleza kuwa fedha hizo zilitolewa na kazi kuanza ambapo hadi sasa matengengenezo yamekamilika kwa asilimia 100 na Wananchi wanatumia daraja hilo kwa shughuli zao ambapo huduma kama elimu na afya zinafikika kwa urahisi.

“Eneo hili la daraja upande wa kuingilia lilikatika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano, tulifanya jitihada kwa kuomba fedha za kazi hiyo ya kurejesha mawasiliano na kuanza kujenga kuta za mawe (Gabions), ujenzi huu umegharimu shilingi milioni 383 na kingo zote mbili za daraja zimekamilika," amesema Mhandisi Brighton.

Juma Hapi ni Diwani wa Kata ya Thawi, ambaye ameelezea kuwa TARURA imetimiza vizuri wajibu wake wakuwezesha wananchi katika shughuli za usafiri na usafirishaji kwa urahisi kwani baada ya mawasiliano kukatika hawakutarajia kama yangerejeshwa kwa muda mfupi na hili linatokana na hali ya Mto Bubu kuwa na maji mengi, aliongeza kuwa Daraja hilo ni kiunganishi kikubwa kati ya kata ya Changaa pamoja na Kata ya Thawi.

Diwani ameeleza kuwa, daraja lilipokatika lilileta adha kwa wananchi kwa kukatisha mawasiliano baina ya kata mbili na kusimamisha huduma za kijamii hivyo kusababisha kukosekana kwa huduma kama shule pamoja na wagonjwa kushindwa kwenda hosptalini.
Muonekano wa Boksi Kalavati katika barabara ya Chandama – Soya – Mwakivabe yenye urefu wa Km 31.2 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma likiwa limekamilika sehemu hii inaunganisha kata tatu Soya, Kimaha, Msaada pamoja na Wilaya ya Chamwino.

“Hakuna mtu aliyetegemea kwamba eneo hili litapitika tena lakini tunawapongeza TARURA kwa kurejesha mawasiliano katika eneo hili kwa kushirikiana na Wananchi kuweza kurudisha mawasiliano katika Kata zetu hizi mbili maana huduma zote zimerejeaa kama hapo awali,”amesema Diwani.

Mbali na urejeshaji wa mawasiliano TARURA imetekeleza ujenzi wa barabara za lami zenye jumla ya urefu wa kilomita 6 ambazo zimebadilisha maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa na kuondoa kero za mda mrefu kwa wakazi wa mji huo.

Kwa upande wa Wilaya ya Chemba TARURA imeendelea kufanya matengenezo ya barabara ya Chandama – Soya – Mwakivabe yenye urefu wa kilomita 31.2, barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa wananchi kwa kuwarahisishia shughuli za usafiri na usafirishaji ili kuwawezesha kwenda Chamwino pamoja na kwenda katika maeneo ya jirani ambapo siku za nyuma ilikuwa haipitiki hasa katika kipindi cha mvua lakini baada ya TARURA kuanza matengenezo ya mara kwa mara hasa katika maeneo korofi sasa inapitika kwa vipindi vyote.

Naye Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Chemba, Mhandisi Mathias Makaju ameeleza kuwa mbali na matengenezo ya barabara hiyo, eneo korofi ambalo lilikuwa linakwamisha shughuli zote kwa kukatisha kwa mawasiliano ni katika eneo la Kata ya Soya ambapo ujenzi wa Kalavati ulifanyika ili kuunganisha Kata tatu ambazo ni Kata ya Kimaha, Kata ya Soya pamoja na Kata ya Msaada kwa gharama za shilingi Milioni 90 ili kuwaondolea kero za mda mrefu kwa Wakazi wa Chemba.

“Barabara ya Chandama – Soya – Mwakivabe ina urefu wa kilomita 31.2 imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Chemba pia daraja hili ni muhimu kwa wananchi wa Chemba, tumeamua kufanya hivi ili tuwawezeshe wananchi kuvuka kutoka eneo moja kwenda jingine na kuwawezesha kusafirisha mazao yao kama alizeti, mahindi pamoja na kuwezesha shughuli kubwa za mnada mkubwa ambao huwa unafanyika katika maeneo hayo.
Muonekano wa Daraja la Thawi lililopo Mto Bubu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma likiwa limekamilika baada ya kufanyiwa matengenezo, daraja la Thawi linaunganisha kata ya Hondomairo, Thawi pamoja na Changaa.

Mashaka Rajabu ambaye ni Mkazi wa Kata ya Soya ameeleza kuwa wananchi ni mashuhuda wa kazi za TARURA kwani wanatumia barabara hiyo katika vipindi vyote vya mwaka, amesema kuwa ilikuwa ni shida kwenda Mjini kwani barabara zilikuwa hazipitiki kabisa, lakini kwa sasa wanaipongeza TARURA kwa kutuunganishia Kata hizo tatu pamoja na Wilaya Chamwino na Kiteto na kuwezesha mnadana kufanyika kwa urahisi.

TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ipo katika ujenzi wa Daraja la Miembeni ambalo litaondoa kero ya kukatika kwa mawasiliano katika Mji wa Mpwapwa hasa katika kipindi cha mvua kwani Daraja hilo lenye urefu wa Meta 25 litagharimu Shilingi milioni 900 hadi kukamilika kwake na linajengwa chini ya Mkandarasi Technics Construction Group Ltd ambaye ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja hilo umefikia asilimia 50 ili kukamilika, mradi huo pia unatekelezwa baada ya daraja la awali lenye urefu wa Meta 10 kusombwa na maji kwa zaidi ya mara mbili na hivyo kusababisha kukatika kwa mawasiliano ndani ya Mji huo.

Mhandisi Emmanuel Lukumay ambaye ni Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ameeleza kuwa hadi sasa Mji wa Mpwapwa una Km 3 za lami, lakini pia ujenzi wa wa Daraja la Miembeni unaendelea kuunganisha mji huo.

“Ujenzi wa Daraja la Miembeni lenye urefu wa Meta 25 umefikia asilimia 50 na utagharimu shilingi million 900, pia mpaka sasa katika Wilaya yetu ya Mpwapwa tumetekeleza Km 10 za lami ya zege ambazo zipo milimani,” amesema Mhandisi Lukumay.

Samwel Mapuga ambaye ni mkazi wa Mpwapwa ameeleza kuwa kabla ya TARURA Halmashuri ya Wilaya ya Mpwapwa ilikuwa haina lami lakini kwa sasa wanaona jitihada za TARURA katika kuhakikisha Wilaya ya Mpwapwa inakuwa na lami na kuwawezesha kufanya shughuli zao za usafiri na usafirishaji katika kipindi chote cha mwaka, aliongeza kuwa baada ya TARURA kuanzishwa, sasa hatua zinachukulia kwa haraka hasa pale mawasiliano yanapokatika.

“Unaweza kujionea mwenyewe kuwa uwepo wa TARURA katika Halmashauri yetu ya Mpwapwa sasa ina barabara za lami na hatukuwahi kutegemea, lakini pia ujenzi wa daraja hili kubwa ni chachu ya maendeleo yetu,”amesema Mapuga.
Kwaupande wake, Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe ameeleza kuwa uboreshaji wa Barabara za Dodoma Mjini unaendelea huku akitolea mfano eneo la Kisasa maarufu kama Nyumba 300 - FFU tayari Mkandarasi amepatikana ili kuanza Ujenzi wa Barabara hiyo yenye urefu wa Km 1.0 kwa kiwango cha lami, aidha ameongeza kuwa matengenezo na maboresho ya miundombinu yanaendelea katika maeneo mbalimbali ya Jiji.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), mkoani Dodoma una mtandao wa Barabara wenye jumla ya urefu wa Km 6996.25 ambapo Km za lami na zege ni Km 179.70, Barabara za Changarawe 1034.198, na barabara za Udongo 5782.352.

TARURA imeendelea kujikita katika kuwezesha wananchi kupata huduma ya usafiri na usafirishaji kwa urahisi kwa kutengeneza na kuboresha barabara Vijijini na Mijini ikiwa ni pamoja na Makalavati, Madaraja na Mifereji ya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news