Ukame wachochea njaa, utapiamlo uliokithiri

Imebainika kuwa miaka mitatu mfululizo ya ukame Kusini mwa Madagascar imekuwa mwiba kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuwa mazao yamekauka na ongezeko la vimbunga vya mchanga kwenye ardhi yenye rutuba, limesababisha wakulima washindwe kupanda mazao na sasa wanakabiliwa si tu na njaa bali pia utapiamlo uliokithiri.

Ukame wa muda mrefu na uhaba wa maji katika maeneo mengi umesababisha watu kutembea mwendo mrefu kwenda kuteka maji ya baharini.

Picha na Africanews.

UNnews imeripoti kuwa, miongoni mwa waathirika ni Ikemba, anayeishi na watoto wake watano na wajukuu saba katika kijiji kilicho ndani zaidi.

“Bado tuna majani machache ya mdungusi kakati. Ninaposhindwa kwenda kuombaomba kwa jirani, nachimba majani ya mdungusi kakati bila uhakika wa kuyapata.Tunapokosa chochote, tunakunywa maji ya baharini. Ni mbaya kwa afya zetu, lakini hatuna jinsi kwa sababu tutasihnda njaa,”amesema.

Aidha, hali ni mbaya katika kaya nyingine ambako wanaloweka ukwaju na kunywa rojo lake na udongo mweupe,ingawa mlo huu hauna virutubisho vyovyote kwa miili yao.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limechukua hatua ya kusambaza mgao wa chakula kwa kaya 787 ambapo Vola Marie alitembea kilomita nane na mwanae kupokea msaada huo.

Vola amesema, wao ni maskini na hawana chakula kwa sababu ya ukame na hawana chochote wanachoweza kufanya.

Mkurugenzi wa WFP Kanda ya Kusini mwa Afrika, Lola Castro amesema, “Idadi ya watu wasio na chakula na ya watoto wenye unyafuzi inaongezeka. Tunahitaji fedha na tunahitaji rasilimali ili WFP iweze kuongeza operesheni zake hadi maeneo ya Kusini zaidi ya Madagascar.”

Ingawa hali hiyo, mgao wa WFP umeleta nuru na sasa hata jikoni moto umewaka na wanufaika wameweza kupika mlo wenye lishe kwa familia zao.

Wakati huo huo WFP kwa sasa imegeukia njia mbalimbali bunifu katika mnyororo wake wa usambazaji Afrika Mashariki na Kati kwa lengo la kuokoa na kubadili haraka maisha ya mamilioni ya watu wanaohitaji msaada.

Kwa mujibu wa WFP myororo wa usambazaji ndio uti wa mgongo wa shirika hilo ambalo kila siku kwa wastani huakikisha malori 7,500 yanakuwa barabari kwenda kusambaza chakula, ndege 92 hudondosha vifurushi vya chakula na meli 22 zinakuwa baharini zikisafirisha shehena kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu milioni 90 kote duniani.

Ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa endelevu ni lazima kutumia njia ambazo zina ufanisi na za gharama nafuu. Tarek Keshavjee ambaye ni afisa wa kikanda wa masuala ya kiufundi ya WFP Nairobi nchini Kenya alisema,“WFP kila wakati inasaka mbinu bunifu ili kuboresha mnyororo wetu wa usambazaji na katika ubunifu ni kuingia ubia na mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi.

"Mashirika ambayo yanakuja na uzoefu mkubwa na wa jinsi gani kama WFP tunaweza kufanya vyema zaidi kazi zetu kwa kutumia ubunifu ni katika ari ya kutaka kufikisha msaada kwa namna yeyote ile na kutoruhuru chohote kuingilia ari hiyo,”amesema.

Afrika Mashariki kwa mfano, WFP inashirikiana na Kampuni ya Nembo za Biashara (East Africa Trademarks) na hivyo imepewa hadhi ya mwendeshaji wa uchumi aliyeidhinishwa ambayo imesaidia shirika hilo kuokoa muda unaotumiwa na malori ya WFP mpakani yanaposafirisha shehena na kupunguza gharama za usafirishaji lakini pia kufikisha msaada wa chakula haraka kwa wenye njaa.

Richard Kamajugo ni afisa mkuu wa oparesheni za East Africa Trademark,“Hii hususan ni kutokana na kutekeleza sheria na kulipa kodi mizigo inavyosafirishwa na inamaanisha kwamba makampuni yanayofuata sheria yanalipa gharama ndogo za biashara kama zawadi, hivyo malori yanayobeba mizigo ya WFP yanapita bila usumbufu mpakani na huo ni ushidi kwa kila mtu,”amesema.

WFP pia inaangalia njia nyingine ya ubunifu mpya kabisa wa kuanza kutumia meli za angani (Airship) ambazo zitapunguza gharama kwa asilimia 50 na kuweza kufikia hata maeneo yaliyo mashinani zaidi kwa urahisi, zikibeba kuanzia tani 20 hadi 500 za chakula njia ambayo itahakikisha hakuna atakayesubiri miezi au wiki kupata msaada.

Aidha,ubunifu mwingine shirika hilo linasema ni kutumia mashine kama za ATM ili kutoa chakula. Hii itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuokoa muda wa wahitaji msaada kupanga foleni kungoja mgao wa kila mwezi kwani kwenye mashine hizi kwa kutumia kadi maalum wanaweza kuchukua kila siku au wakati wowote.

Pia mbinu ya mwisho bunifu ni kutumia teknolojia ya shamba kwenye makasha au makontena kupanda sawa na ekari kama tano za mboga na mazao mengine kwenye makasha hayo, teknolojia ambayo inatumia maji na nishati ya jua au sola.

Katika hatua nyingine, teknolojia hiyo ikifanikiwa WFP inasema inaondoa gharama zote za usafirishaji na usambazaji kwa asilimia kubwa.

No comments

Powered by Blogger.