Uzini watakiwa kushirikiana na viongozi kuharakisha maendeleo

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Uzini, Khamis Hamza Khamis (Chilo) amewataka wananchi wa Kijiji cha Bambi kushirikiana na viongozi waliowachagua ili kuleta maendeleo ya kielimu hasa wakati huu ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hayo ameyasema alipokuwa akikabidhi vifaa vya ujenzi wa jengo la Skuli ya Bambi lenye madarasa matatu yanayojengwa kwa nguvu za wananchi ili kupunguza uhaba wa madarasa unaoikabili skuli hiyo.

Amesema, maendeleo ya elimu yatapatikana kwa kuboresha usomeshaji na kuweka mazingira ya wanafunzi kwa kuondoa vikwazo vinavyowakabili na kupata elimu bora.

Ameeleza kuwa, atashirikiana na viongozi wa jimbo la hilo kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wao.

Nae Mwakilishi wa jimbo hilo Haji Shaaban Waziri amemtaka Mkurugenzi wa jiji Wilaya ya Kati kumalizia ujenzi wa kituo cha Afya cha Mpapa baada ya wananchi kulalamika kuwa fedha zilizotolewa na Mwakilishi aliyemaliza muda wake hazikutumika ipasavyo.

“Nataka ndani ya siku tatu uhakikishe kuwa suala la kituo hicho unalitafutia ufumbuzi ili kuondosha malalamiko ya wananchi wanaotumia kituo hicho cha afya,”ameeleza Mwakilishi huyo.

Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi wa jiji la Wilaya ya Kati Salum Mohammed Salum alikiri kupokea fedha kwa ajili kumalizia ujenzi huo wa kituo cha afya, lakini hakuifanya kazi hiyo ameahidi kutekeleza na kuimaliza kadhia hiyo ndani ya siku mbili.

Mapema viongozi hao walipata nafasi ya kuwasalimia viongozi wa mashina (balozi) ambapo Bwana Ramadhan Zagila anaesumbuliwa na maradhi ya kuvimba miguu aliomba msaada wa kupatiwa matibabu ya uhakika ili arudi katika hali ya kawaida na kuendelea na majukumu yake.

Akitoa neno la shukurani Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Bambi Kibabu Ali Haji amesema atahakikisha anasimamia vyema ujenzi wa banda hilo hadi litakapokamilika.

No comments

Powered by Blogger.