Wakurugenzi wa Halmashauri waagizwa kukutana na Watendaji wa mitaa na vijiji uandikishaji nyumba zote nchini

Serikali imewataka Wakurugenzi wote Nchini kukutana na watendaji wa mitaa, vijiji na kuwapa maelekezo ya namna watakavyoenda kusimamia zoezi la uandikishaji nyumba zote katika Malaka za Serikali za Mitaa,anaripoti Angela Msimbila (TAMISEMI).
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo wakati alipokutana Menejimenti ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI leo jijini Dodoma.

Waziri Jafo amesema zoezi la uandikishaji litaambatana na kampeni maalum ya uandikishaji wa kurodhesha nyumba zote nchini na kampeni ya ulipaji kodi ya majengo lengo likiwa ni kuhakikisha Serikali inakusanya mapato.

“Zoezi hili linatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu tarehe15 hadi 28 mwezi Februari mwaka huu,"amesisitiza Waziri Jafo.

Waziri Jafo amewaagiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za mitaa nchini kuwa tarehe 11 Februari, 2021 kukutana na watendaji wa mitaa na vijiji ili kuweka mikakati ya namna nzuri ya kukusanya kodi ya majengo katika Mamlaka zao.

Aidha, Waziri Jafo ameitaka Bodi ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuweka mifumo yake vizuri ya ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya magari ili makusanyo hayo yaweze kukusanywa ipasavyo.

Katika hatua nyingine Mhe. Jafo ametoa wito kwa watanzania kutoa ushirikiano kwa viongozi wao katika mamlaka ya serikali za mitaa ili kufanyikisha mazoezi yote kwa ufasaha ili lengo la ukusanyaji mapato kuwa na tija kwa taifa.

No comments

Powered by Blogger.