Watu 60 washikiliwa kwa uhalifu mkoani Kilimanjaro

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na kikosi kutoka makao makuu ya jeshi hilo yaliyopo Dodoma, limewakamata watu 60, katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, wakituhumiwa kujihusisha na makosa ya uhalifu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Watu hao wanatuhumiwa kufanya makosa mbalimbali ya uhalifu ukiwemo wizi wa pikipiki, usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na kujihusisha na utengenezaji na biashara ya pombe haramu ya gongo.
Akitoa taarifa ya operesheni hiyo, leo Jumapili Februari 14, 2021,mkuu wa operesheni maalumu za jeshi hilo kutoka makao makuu, Mihayo Msikhela amesema watu hao wamekamatwa kufuatia operesheni maalumu ya siku saba waliyoifanya mkoani humo.

Amesema watu hao wamekamatwa na pikipiki nne, lita 549.2 za pombe haramu ya gongo, mitambo 18 ya kutengenezea pombe hiyo, mapipa matupu 112 ya kutengenezea gongo, madumu tupu 38, pamoja na ndoo tupu mbili.

Vitu vingine walivyokamatwa navyo ni dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 68.8, misokoto ya bangi 2,340, mbao 497, pamoja na nyavu haramu za uvuvi nne.

Pia amesema kati ya watu hao waliokamatwa, wapo wezi wa pikipiki wawili, waliokutwa na mitambo ya kutengeneza pombe haramu ya gongo 13, waliokutwa na gongo 26, watatu waliokutwa na misokoto ya bangi, tisa waliokutwana mirungi, wanne waliokutwa na nyavu haramu na mtu mmoja akikamatwa na mazao ya misitu.

Kwa upande wake Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona, amesema operesheni hiyo ni endelevu na kwamba yapo majina ya watu waliyoyaorodhesha, ambao wanaendelea kuwasaka ili kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria

Post a Comment

0 Comments