Watu 6 kufikishwa Mahakamani kwa makosa ya udanganyifu, utakatishaji fedha Bilioni 8/-

Ndugu WanaHabari,

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jen. John Mbungo, napenda kuujulisha Umma kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU – Makao Makuu, imekuwa ikifanya uchunguzi dhidi ya Kampuni iitwayo Peertech Company Limited na kubaini kuwa Wakurugenzi na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wamejihusisha na kutenda makosa ya udanganyifu na wizi wa zaidi ya Shilingi Bilioni 8.

Kutokana na uchunguzi huo, leo Februari 25, 2021, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, tunawafikisha Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi – Kisutu jijini Dar Es Salaam, watuhumiwa sita (6) kati ya watuhumiwa (9) wanaotuhumiwa kuhusika wa wizi huo ili wakajibu mashitaka dhidi yao.

Ndugu Wana Habari,

Awali, mnamo mwezi Septemba mwaka jana (2020), TAKUKURU ilipokea malalamiko yanayowatuhumu baadhi ya viongozi wa Peerterch Company Limited – Kampuni ambayo inajishughulisha na masuala ya Mawasiliano, Teknolojia na Habari nchini, kwamba iliwasilisha kwenye mabenki mbalimbali majina ya wafanyakazi hewa na kuomba mikopo kwa kutumia majina hayo - mikopo ambayo haikurejeshwa kwenye mabenki husika.

Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, pamoja na mambo mengine, ulibaini mambo yafuatayo: 

-Kwamba katika kipindi cha kati ya mwaka 2018 hadi 2020, kwa kutumia orodha ya majina ya watumishi hewa, Kampuni ya Peertech iliingia makubaliano na Benki za NBC, ABC na ABSA zote za jijini Dar Es Salaam, na kuweza kujipatia fedha kiasi cha shilingi bilioni nane (8) kwa njia za kughushi.

-Kwamba, orodha ya watumishi iliyowasilishwa katika benki hizo na kampuni ya Peertech kwa ajili ya kupatiwa mikopo, hawajawahi kuajiriwa wala kufanya kazi katika Kampuni ya Peertech Company Limited na hivyo ili watuhumiwa waweze kufanikisha nia yao ovu, walitengeneza na kughushi mikataba, salary slips pamoja na vitambulisho vya kazi na kuziwasilisha nyaraka hizo katika benki nilizozitaja.

-Vile vile, uchunguzi wa TAKUKURU umebaini kuwa, ili kufanikisha upatikanaji wa mikopo hiyo ya kughushi, Kampuni hii ya Peertech iliwasilisha ‘bank statements’ za kughushi kutoka benki za NMB, CRDB, GT Bank pamoja na BOA Bank – zote za jijini Dar Es Salaam.

-Jambo jingine ambalo lilibainishwa katika uchunguzi huo ni kwamba, Kampuni ya Peertech iliwasilisha kadi za wapiga kura na vitambulisho vya Uraia ambavyo ni vya kughushi.

-Kwamba, kati ya mwaka 2019 na 2020, kampuni hii kupitia waajiriwa wao waliotambulika kama Mohamed Kombo, Leena Francis pamoja na Benard Mndolwa - ambao walikuwa ndiyo watia saini (signatories) katika nyaraka za mikopo, iliwasilisha nyaraka za wafanyakazi 78 katika benki za NBC, wafanyakazi 40 katika Bank ya ABC na wafanyakazi 22 katika benki ya ABSA kuonyesha kwamba watumishi hao ni waajiriwa wa kampuni ya Peertech Company Ltd huku wakijua si kweli.

-Ilibainika pia kwamba, kutokana na kuwasilisha maombi hayo ya mikopo, jumla ya mikopo ya Sh. Bil 4.7/- ilipatikana kutoka NBC, Bil 1.9/- ilipatikana kutoka Bank ya ABC na mikopo ya Shilingi Bil 1.3/- ilipatikana kutoka benki ya ABSA na mikopo hii ilitolewa kwa ‘wafanyakazi hewa’ 140 wa kampuni hiyo.

Ndugu WanaHabari,

Kupitia hadhira hii, tunapenda kuujulisha umma kwamba watuhumiwa tisa wafuatao, watafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu – Jijini Dar Es Salaam leo.

1. MARK JULIUS MPOSO – Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Peertech Company Limited.

2. BARAKA GRATIAN MADAFU – Mkurugenzi wa Uendeshaji – wa Peeterch Company Limited

3. BENARD SEMBOJA MNDOLWA – Mkaguzi wa Ndani wa Peeterch Company Limited

4. LEENA FRANCIS JOSEPH – Meneja Operesheni wa Peeterch Company Limited

5. LUSEKELO MBWELE- Meneja wa Fedha wa Peertech Company Limited

6. SALVINA KARUGABA - BANK OFFICER, NBC BANK, Tawi la MNAZI MMOJA

Ndugu WanaHabari,

Tuhuma zinazowakabili watuhumiwa hawa ni pamoja na tuhuma sita (6) zifuatazo:

1. Kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

2. Kughushi

3. Kuendesha genge la uhalifu

4. Kusaidia kutenda kosa

5. Kukwepa kulipa kodi pamoja na

6. Kutakatisha fedha haramu

Ndugu WanaHabari,

Kupitia kwenu tunatoa taarifa kwamba Watuhumiwa watatu (3) wafuatao walihusika katika uhalifu huu ambao bado TAKUKURU inawatafuta:

1. MOHAMED KOMBO @ MOHAMED ABDALLAH MAKANDA @SUZUKI

Huyu ni Afisa Raslimali watu wa Kampuni ya PEERTECH






2. HUSSEIN ABDALLAH MOHAMED@ AMANI

Huyu alikuwa akitumika kuchukua fedha benki

3. PAUL EDWARD SHAYO @ KIKY

Huyu ni kutoka Kampuni ya UNICREDIT MICRO – FINANCE.

Tunatoa wito kwa yeyote atakayekuwa na taarifa za kuwezesha upatikanaji wa watuhumiwa hawa, tafadhali atoe taarifa katika ofisi zetu zilizoko katika kila Wilaya na kila mkoa – Tanzania Bara.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.


IMETOLEWA NA:


SIGNED

Doreen J. Kapwani

AFISA UHUSIANO WA TAKUKURU

KWA NIABA YA MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news