Waziri Jafo: Halmashauri zianze kukusanya ushuru wa majengo, mabango, vitambulisho vya wajasiriamali

Serikali imesema kuanzia sasa ushuru wa majengo, mabango na vitambulisho vya Wajasiriamali umerejeshwa rasmi kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa, isipokuwa ule unaosimamiwa na TANROADS na TARURA, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Tamko hilo limetolewa leo Februari 1, 2021 mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati walipozungumza na waandishi wa habari.

Wamesema lengo la kurejesha ushuru huo ukusanywe na Halmashauri ni kuongeza wigo mpana wa kukusanya mapato yake ili kupitia vyanzo hivyo ili kuiwezesha Serikali kutekeleza shughuli mbali mbali za maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano huo na Waandishi wa Habari, Waziri Jafo alisema kuanzia sasa ushuru wa majengo, mabango na vitambulisho utakusanywa na halmashauri kama awali isipokuwa ule unaosimamiwa na TANROADS na TARURA.

Amesema kutokana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwa na Mtandao mpana ambao umekwenda hadi katika ngazi za vijiji, mitaa na vitongoji, na kwa kuwa zipo karibu na kutambua mabango ni dhahiri zitaweza kukusanya ushuru wa mapato kwa urahisi zaidi

“Hivyo nitumie fursa hii, kuwataka Wakurugenzi wote kupitia, Maafisa biashara, maafisa Kata, na Vijiji waweze kukusanya kodi kwa kuwafikia wafanya biashara wote katika maeneo yao,” amesema Waziri Jafo.
Ameongeza kuwa, kutokana tamko hilo hatarajii kuanzia sasa kuona kuna mfanyabiashara anayefanya biashara bila kulipa kodi ya mapato ya TRA, leseni ya biashara ya Halmashauri au bila kitambulisho cha wajasiliamali na kuonya kuwa sheria kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaofanya biashara zao kinyume na agizo la serikali.

Kuhusu vitambulisho vipya vya wajasiliamali Waziri Jafo amesema, vitambulisho hivyo tayari vimekwishachapishwa na kupelekwa katika ofisi za TRA nchini kote na sasa vitakuwa chini ya Wakuu wa Mikoa hivyo, Wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa wakachukue tayari kwa kuwafikishia wajasiriamali.

Amesema, vitambulisho vilivyoboreshwa vitapatikana kwa bei ile ile ya shilingi elfu ishirini (20,000) kwa kitambulisho kimoja ambapo mfanyabiashara ataweza kufanya biashara zake mwaka mzima bila kubugudhiwa.

Aidha, Waziri Jafo amewaonya baadhi ya wafanyabiashara wa maduka makubwa wasiokuwa waaminifu wanaowapatia bidhaa wajasiriamali wadogo, kuacha mara moja tabia ya kuwapatia bidhaa wajasiriamali wadogo ili wakatembeze mitaani kwa lengo la kukwepa kodi.

“Mfanyabiashara yoyote anayefanya hivyo ni mhujumu uchumi kupitia mapato, kama walivyo wahujumu chumi wengine, hivyo Serikali haitamfumbia macho na badala yake mkondo wa sheria utachukua nafasi yake, ni rai yangu kila mtu anayeuza bidhaa, atoe risiti na kila anayenunua bidhaa adai risiti,” Mhe. Jafo amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, ambaye alizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha amesema, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kulipa uzito suala la kulipa kodi kama ajenda ya kudumu ambayo inatajwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi-(CCM) 2020/2025.

Akiongea kwa njia ya simu kutoka wilayani Magu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Lutengano George Mwalwiba amepongeza hatua ya serikali kuwarejeshea kukusanya vyanzo hivyo vya mapato kwani mtandao wa Mamlaka hizo ni mpana ikilinganishwa na taasisi zingine.

Ushuru wa huo uliondoshwa katika mamlaka hizo mwaka 2018 na kukabidhiwa Wizara ya Fedha chini ya mamlaka ya mapato Tanzania TRA, hata hivyo katika kile kinacho onekana kuzidisha wigo wakukusanya Mapato, Serikali imeamua, kazi hiyo kurejeshwa tena kwenye mamlaka hizo ili kuongeza tija na ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news