Zanzibar mbioni kuanza kutumia mfumo wa risiti za kielektroniki kukusanya mapato

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo mbioni kuanza kutumia mfumo wa utoaji risiti kwa njia ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato ya Serikali, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akijibu swali la Mhe. Machano Othman Said ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini aliyetaka kujua kuhusu changamoto ya ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara huko katika Baraza la Wawakilishi Chukwani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Mhe. Jamal Kassim Ali amesema katika kipindi cha majaribio mfumo huo ulibainika kuwa na dosari ambazo zimeanza kufanyiwa marekebisho.

Amesema kuwa, mfumo huo wa majaribio umewashirikisha wafanyabiashara 150 kutoka makundi tofauti ya biashara Unguja na Pemba.

Waziri Jamal amesema, mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika mwezi Aprili, mwaka huu kwa watu wote waliosajiliwa kulipa kodi na kwamba hivi karibuni Serikali itazindua rasmi matumizi ya vifaaa vya mfumo wa kutolea risti za kieletroniki.

Aidha, Waziri Jamali amewataka wananchi kudai risiti kila wanapolipa fedha kwa ununuzi wa mafuta ili kuimarisha maendeleo ya nchi na kufikia malengo yake.

Vilevile serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mufti imekusudia kufanya uhakiki wa misikiti na madrasa zote za Zanzibar ili kuhakikisha misikiti na madrasa inasajiliwa kwa mujibu sheria na taratibu.

Akijibu swali la Mhe. Salma Mussa Bilali kutoka nafasi za wanawake aliyetaka kujua serikali imejipanga vipi kuhakisha misikiti na madrasa zote Zanzibar zinasajiliwa,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema kwa sasa ofisi hiyo imeshaanza kufanya uhakiki wa madrasa za Mkoa wa Mjini Magharibi na Kaskazini Unguja ambapo zoezi hilo litaendelea Mkoa wa Kusini Unguja na Mikoa yote ya Pemba.

Amesema, ofisi hiyo imeandaa utaratibu wa kufanya ukaguzi wa misikiti na madrasa ili kubaini matatizo yanayozikabili na kuyapatia ufumbuzi kwa kushirikiana na wananchi wenyewe.

Akiuliza swali la nyongeza Mhe. Panya Abdalla kutoka nafasi za wanawake alilouliza kwa nini walimu wa madrasa baadhi yao hawana taaluma ya kutosha na katika kusomesha na kutaka kujua ofisi hiyo imejipanga vipi.

Waziri Haroun amesema, Ofisi ya Mufti imejipanga vzuri katika kuwapa elimu ili kupata walimu bora katika ufundishaji.

No comments

Powered by Blogger.