BARAZA LA WAFANYAKAZI LA WIZARA YA MADINI LAFANYIKA DODOMA

Wizara ya Madini imeshiriki katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ambapo wamejadili changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa Wizara ya Madini, wanaripoti Tito Mselem na Steven Nyamiti Dodoma (WM) Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa walioshiriki Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini Machi 27, 2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa walioshiriki Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini Machi 27, 2021 jijini Dodoma.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini Justine Ludamila akijajadili jambo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Augutine Ollal katika kokao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini Machi 27, 2021 jijini Dodoma.
Katika kikao cha baraza hilo, kilichofanyika jijini Dodoma kilihusisha watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ambapo Mwenyekiti wa Baraza ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Augustine Ollal aliongoza majadiliano ya baraza hilo.

Akifungua kikao cha baraza hilo, Ollal ametoa pole kwa Watanzania wote kwa kuondekewa na mpendwa wao aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambapo amesema tumuenzi Hayati Dkt Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na kwa moyo wa uzalendo ili kufanikisha maono aliyotaka yafikiwe.

Wakati huo huo, Ollal amempongeza Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kumpa ushirikiano katika kutimiza majukumu yake.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi (TUGHE) wa Wizara ya Madini Joseph Ngulumwa, ameupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa kutekeleza maazimio yaliyo jadiliwa kwenye baraza lililopita ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwapeleka mafunzo mbalimbali ambapo Wizara imepeleka watumishi wake 13 katika mafunzo ya muda mfupi na watumishi 19 mafunzo ya muda mrefu.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango Fredy Matola, amesema Wizara ya Madini inaendelea na Utekelezaji wa kuimarisha udhibiti na usimamizi wa uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini na kuweka mazingira bora yatakayohamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini.

"Kwasasa Wizara ya Madini tunawawezesha Wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija, kudhibiti utoroshaji na biashara haramu ya madini nchini, kuweka mikakati ya kuimarisha soko la Tanzanite na madini mengine na Kuhamasisha shughuli za Uongezaji thamani Madini" amesema Matola.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini Antony Tarimo amesema kuwa, matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 kuanzia tarehe 1 Julai, 2020 hadi 28 Februari, 2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliidhinisha Bajeti ya jumla ya TZS 62, 781,586,000.00 ambapo fedha hizo zilitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wizara, matumizi mengineyo pamoja na fedha za mishahara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Issa Nchasi, amesema kuwa, Idara yake inaendelea kuwahudumia watumishi wa Wizara hiyo ambapo Wizara imenunua vifaa vya kupimia afya ya watumishi wake ikiwa ni pamoja na kifaa cha kupimia shinikizo la damu, kiwango cha sukari mwilini, uzito pamoja na ukimwi kwa lengo la kuhakikisha afya za watumishi zinaimarika.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, Kiongozi wa TUGHE Makao Makuu, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Afisa Kazi Mkoa wa Dodoma na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news