🔴𝐋𝐈𝐕𝐄: Dkt.Philip Isdor Mpango akiapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

"Sote ni mashahidi, nataka kukumbusha matukio mawili, wakati tunaomboleza, wananchi wanyonge kabisa kule Dar es Salaam waliruka fensi kwenda kumsikiza kipenzi chao Hayati Magufuli wakati mwili wake unataka kupakiwa kwenye ndege kuja Dodoma. Tukio la pili nilishuhudia hapa Dodoma bodaboda walivyoamua kumsikindikiza kipenzi chao.

"Matukio haya mawili yanatoa ujumbe kazi ambazo zimeachwa na kipenzi chetu zisipokwenda vizuri hatuna namna, kwa hiyo tunatakiwa kuhakikisha ndoto za watanzania zinatimia, wanataka SGR yao ikamilike, wanataka bwawa la Mwalimu Nyerere likamlike, wanataka barabara na hasa za vijijini zikamilike.

"Wanataka huduma za afya ziwe bora zaidi, wanataka maji safi na salama, wanataka usalama wao waendeee kufanya shughuli zao.Hawataki rushwa, ninachotaka kusema kama Bunge litanithibitsha haya ndio mambo nitakayokwenda kumsaidia Rais wetu ili nchi yetu isonge mbele, kiu ya wananchi itimie.Bunge ni chombo muhimu sana na katika miaka mitano na kidogo nimejifunza sana,"amesema hayo Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango bungeni jijini Dodoma Machi 30,2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema hakuona mtu mwingine mwenye sifa kama za Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na ndio sababu za kumteua kushika wadhifa huo.
 
Ameyasema hayo leo Machi 31, 2021 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma muda mfupi baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma kumwapisha Dkt.Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia ametumia fursa hiyo kuishukuru Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge kwa kupitisha jina la Dkt.Mpango bila kikwazo.

“Nilizunguka sana kutafuta nani awe, nilipata salamu nyingi nikaangalia ndani na nje ya Bunge, lakini nikarudi ndani ya Bunge. Mtu niliyemuona kwa sasa hivi anayeweza kwenda nami ni ndugu yetu Phillip Isdor Mpango,”amesema.

Rais Samia alitaja sifa nyingine ya Dkt.Mpango kuwa pamoja na kumcha Mungu ni mchumi mzuri,mchapa kazi na mtu aliyetulia katika majukumu yake.

“Kubwa, Philip ametulia hana hili wala lile. Majina mengine nilikuta (mtu) ana hili ana lile, lakini Philip nilikuta katulia kwa hiyo nikasema huyu atanifaa kwenda naye, kwa hiyo hongera sana,”amesema Rais huku akisema atamsaidia kwenye uchumi na pia katika udhibiti wa fedha za Serikali.

Aidha, kuhusu suala la Muungano, Rais Samia alimtaka Dkt. Mpango kumaliza kero ya uhusiano wa fedha kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano akisema haikupata ufumbuzi na aliyekuwa ameikalia alikuwa ni kiongozi huyo.
Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akitia saini Hati ya Kiapo mara baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kushuhudia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisoma majina ya Mawaziri na Manaibu Waziri aliowateua katika Baraza la Mawaziri mara baada ya kushuhudia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge Job Ndugai, mara baada ya hafla ya Uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya Uapisho wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango wakiwa katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 31 Machi 2021. (Picha zote na Ikulu).
 
“Waswahili wanasema mwanga mpe mtoto wako akulelee. Sasa matumaini yangu ni kwamba Dkt.Mpango utatafuta wanga wenzio ili myamalize yale mambo,”amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais, Dkt.Philip Mpango akizungumza baada ya kiapo hicho amesema kuwa, atafanya kazi kwa bidii na kamwe hatamsaliti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Wiki hii Wakristo wanasherekea tunaita Ijumaa Kuu na hasa siku ya kesho mtu anaitwa Yuda Iskariote kwenye Biblia alipomsaliti Yesu kwa vipande vya fedha. Mheshimiwa Rais sitakuwa kama huyo Yuda. Nitatekeleza kwa bidii na weledi kazi zote utakazonielekeza pamoja na mengine yalivyoelekezwa kwenye ile ibara ya 47. Katika kutekeleza majukumu unayonituma nitashirikiana na viongozi wenzangu inavyopaswa na ninasema hivyo, nisisitize ni kwa pande zote za muungano na mihimili yote ya dola,”amesema Makamu wa Rais huyo.

Awali Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema, Dkt. Philip Mpango anakwenda kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muungano huku akimtaka akamalize kero za Muungano huo.

“Sina shaka chini ya uongozi wako na kero zilizobaki na zile mpya zitakazojitokeza, kama tunavyotambua Muungano ndani yake kuna mambo yanayokuja mapya. Binafsi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tuitakupa ushirikiano wa kutosha,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Rais Samia atangaza Baraza la Mawaziri


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 31 Machi, 2021 amefanya uteuzi wa Wabunge 3 na kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambapo amewabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri na ameteua Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya.

Mhe. Rais Samia amefanya uteuzi wa Wabunge 3 ambao ni


Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Kabla ya uteuzi huu alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi)


Mhe. Balozi Liberata Mulamula


Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk

Mhe. Rais Samia amemteua Mhe. Balozi Hussein Athuman Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Balozi Katanga alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.

Baada ya mabadiliko, ifuatayo ni orodha ya Baraza la Mawaziri.

Ofisi ya Rais.


Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


Waziri – Mhe. Ummy Ali Mwalimu

(Kabla ya uteuzi huu alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira).


Naibu Mawaziri – Mhe. Dkt. Festo John Dugange


Naibu Waziri - Mhe. David Silinde

Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Waziri – Mhe. Mohammed Omar Mchengerwa


Naibu Mawaziri – Mhe. Deogratius Ndejembi

Ofisi ya Makamu wa Rais.


Muungano na Mazingira


Waziri – Mhe. Selemani Jafo

(Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa TAMISEMI)


Naibu Waziri – Mhe. Hamad Hassan Chande


Ofisi ya Waziri Mkuu.


Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu


Waziri – Jenister Joakim Mhagama


Naibu Mawaziri – Mhe. Patrobas Katambi


Naibu Waziri - Mhe. Ummy Nderiananga


Uwekezaji


Waziri – Mhe. Geofrey Mwambe (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara)


Naibu Waziri – Mhe. William Tate Ole Nasha

Wizara


Wizara ya Fedha na Mipango


Waziri – Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria)


Naibu Waziri – Mhe. Hamad Yussuf Masauni


Wizara ya Katiba na Sheria.


Waziri – Mhe. Prof. Palamagamba Aidan Kabudi (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki)


Naibu Waziri – Mhe. Geofrey Mizengo Pinda


Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)


Waziri – Mhe. Elias Kwandikwa


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Waziri – Mhe. Balozi Liberrata Mulamula


Naibu Waziri – Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk


Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Waziri – Mhe. George Simbachawene


Naibu Waziri - Mhe. Khamis Hamza


Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi


Waziri – Mhe. Leonard Chamriho


Naibu Waziri – Mhe. Geofrey Kasekenya


Naibu Waziri - Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara


Wizara ya Viwanda na Biashara.


Waziri – Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Uwekezaji)


Naibu Waziri – Mhe. Exaud Kigahe


Wizara ya Madini.


Waziri – Mhe. Dotto Mashaka Biteko


Naibu Waziri – Mhe. Shukrani Manya


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


Waziri – Mhe. William Lukuvi


Naibu Waziri – Mhe. Dkt. Angelina Mabula


Wizara ya Maji


Waziri – Mhe. Jumaa Hamidu Aweso


Naibu Waziri – Mhe. MaryPrisca Mahundi


Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo


Waziri – Mhe. Innocent Bashungwa


Naibu Waziri – Mhe. Pauline Gekul (Kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi)


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Waziri – Mhe. Prof. Joyce Ndalichako


Naibu Waziri – Mhe. Omar Kipanga


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.


Waziri – Mhe. Dorothy Gwajima


Naibu Waziri – Mhe. Godwin Mollel


Naibu Waziri – Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Waziri wa Fedha)


Wizara ya Nishati


Waziri – Mhe. Dkt. Medard Matogolo Kalemani


Naibu Waziri – Mhe. Stephen Byabato


Wizara ya Maliasili na Utalii.


Waziri – Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro


Naibu Waziri – Mhe. Mary Francis Masanja


Wizara ya Kilimo.


Waziri – Mhe. Prof. Adolf Mkenda


Naibu Waziri – Mhe. Hussein Mohammed Bashe


Wizara wa Mifugo na Uvuvi.


Waziri – Mhe. Mashimba Mashaka Ndaki


Naibu Waziri – Mhe. Abdallah Khamis Ulega (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo)


Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.


Waziri – Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile


Naibu Waziri - Mhe. Kundo Mathew

Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya na waliobadilishiwa wizara wataapishwa kesho saa 9:00 Alasiri Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa miezi 3 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Naibu Waziri wake kuanzisha wizara hiyo vinginevyo watahesabiwa kuwa wameshindwa kufanya majukumu yao.

Mhe. Rais Samia amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri hao kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwamba watakaoshindwa kutimiza wajibu wao hatosita kufanya mabadiliko.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu Profesa Khamis Juma, Spika wa Bunge, Job Ndugai na Naibu Spika, Dkt.Tulia Ackson, mawaziri, viongozi wastaafu na viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini. 
 
 
Ripoti hii imeandaliwa na Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).

Post a Comment

0 Comments