India, Japan na Oman zamwandikia BARUA ya Kiserikali Rais Samia Suluhu Hassan

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya India, Mhe. Narendra Modi amemwandikia barua ya kiserikali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kumpa pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Katika barua hiyo, Mhe. Modi amesema amesikitishwa na kifo cha Dkt.Magufuli kutokana na kumbukumbu zake alipoitembelea Tanzania mwaka 2016 na kupata mapokezi yenye ukarimu mkubwa ambapo walizungumza masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayohusu Taifa la India na Tanzania na hata hivi karibuni walipozungumza kwa njia ya simu.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Emmanuel Buhohela ambaye ni Mkurugenzi,Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Nimempoteza rafiki wa karibu na mwenye thamani kubwa na nitamkumbuka kwa namna alivyojitolea kulijenga Taifa lake kwa manufaa ya Watanzania,”amesema Mhe. Modi.

Mhe. Modi amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kuwa na moyo wa subra hususani wakati huu anapopokea madaraka ya Urais katika kipindi kigumu cha maombolezo ya Taifa na kumhakikishia kuwa India itaendelea kuwa rafiki mwema kwa Tanzania na Serikali iko tayari kushirikiana naye. 

Mwisho Mhe. Modi amemalizia kwa kusema kwa niaba ya serikali na watu wa India anatoa salamu za rambirambi kwa Mhe. Rais, Familia, Serikalina Watu wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Katika tukio jingineNaibu Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Ulinzi wa Serikali ya Oman, Mtukufu Sayyid Shihab bin Tarik bin Taimur Al-Said, akiambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi pamoja na Viongozi wengine wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman amesaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Oman. 

Katika Salamu zake Mtukufu Sayyid Shihab bin Tarik bin Taimur Al-Said amemuelezea Hayati Dkt. Magufuli kama Kiongozi mchapakazi, mzalendo na mwana maendeleo ambaye Tanzania, Afrika na Dunia itaendelea kumkumbuka. 

Pia amemtakia utendaji kazi mwema na uliotukuka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi wengine walioandikia barua ya kiserikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni Waziri Mkuu wa Japan Mhe SUGA Yoshihide. Katika barua yake Mhe Yoshihide ameeleza kusikitishwa kwake kufuatia kifo cha Dkt. Magufuli na kwa niaba ya Serikali na watu wa Japananatoa pole kwa familia,Serikali na Watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Katika barua hiyo amesema Hayati Magufuli enzi za uhai wake amekuwa kiongozi aliyetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yake kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda,kutengeneza ajira,na kuweka kipaumbele katika suala la kukuza uchumi usiotegemezi.

“Katika kipindi hiki cha maumivu na huzuni ambacho Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakipitia hivi sasa, Japan iko pamoja na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mhe. Yoshihide.

Mhe. Yoshihide amemalizia barua yake kwa kusema Japan itaendelea kushirikiana na kukuza ushirikiano baina yake na Tanzania.

Post a Comment

0 Comments