Joseph Mgongolwa: Vijana tumuenzi Hayati Dkt. Magufuli kwa kudumisha uzalendo, amani na umoja

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini, Joseph Mgongolwa amesema,njia pekee vya vijana wa Kitanzania kumuenzi aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ni kudumisha uzalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Mheshimiwa Mgongolwa ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea namna ambavyo, vijana wana wajibu mkubwa wa kumuenzi Hayati Dkt.Magufuli kwa kudumisha uzalendo.

"Kifo cha mzee wetu Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kiliwashtua wengi sana nikiwemo mimi pia, kama tunavyojua Rais wetu huyo alikuwa mzalendo namba moja, ni kiongozi ambaye aliwapenda vijana na watu wote hapa nchini bila kujali dini, itikadi au imani zao, hivyo sisi kama vijana tunapaswa kumuenzi kwa kudumisha uzalendo, upendo, amani na mshikamano.

"Tuwe na bidii katika kazi huku tukizingatia umoja na mshikamano utatuwezesha kuziendea ndoto za mpendwa wetu za kulifanya Taifa la Tanzania kuwa Taifa linalostawi kiuchumi. Ni rai yangu kwa kila mmoja, asione aibu kudumisha umoja, amani na mshikamano. Tanzania ndilo Taifa letu na hatuna taifa lingine, hivyo ni wajibu wetu kuonyesha uzalendo na kujivunia kuwa Watanzania,"amesema Mgongolwa.

Mjumbe huyo ameungana na Watanzania wote kutoa salamu za pole kwa familia ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kwa kuondokewa na mpendwa wao huyo

Amesema kuwa, Hayati Dkt.Magufuli atamkumbuka daima kwa moyo wake wa uzalendo na upendo mkubwa kwa wananchi hususani wanyonge na taifa kwa ujumla ikiwemo dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi kuanzia vijijini hadi mijini.

Pia Mgongolwa amesema, Hayati Dkt.Magufuli wakati wa uhai wake aliifanyia mambo mengi na makubwa Tanzania ndio maana kila mpenda maendeleo ameumizwa na kifo hicho hasa kutokana na dhamira yake ya dhati ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kati wa viwanda ili kuharakisha maendeleo.

Wakati huo huo, Mgongolwa ameema kuwa, wao kama vijana wapo mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za maendeleo chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ili aweze kuyafikia malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Unajua Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 hadi 2025 imejaa mambo mengi, ni kitabu chenye kurasa zaidi ya 300 ambacho kinaangazia mahitaji yote ya Watanzania kuanzia kule vijijini hadi mijini, tunaamini kwa uhodari na uchapakazi wa mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wake unakwenda kufanikiwa kwa asilimia 100 na tutarajie mafanikio makubwa mno. Kubwa zaidi tuendelee kumuombea afya njema,"amesema Mgongolwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news