Mahakama ya Mwanzo jijini Ilala yavunja ndoa ya wanandoa waliotengana kwenda kutafuta watoto nje

Leo Machi 17, 2021 Mahakama ya Mwanzo Buguruni iliyopo Kata ya Bugurudi jijini Ilala imevunja ndoa kati ya Magreth Silaeli (37) na aliyekuwa mume wake, Raymond Kulaya (44), anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Ilala).

Uamuzi huo umefikiwa baada ya wawili hao kutengana kwa miaka 10 kwa madai kwamba kila mmoja wao akatafute watoto nje ya ndoa yao.

Silaeli ambaye ni mkazi wa Tabata Liwiti jijini Ilala, Dar es Salaam na Kulaya wote walibahatika kupata watoto saba baada ya kutoka nje ya ndoa yao kwa sababu kila mmoja wao alikuwa na matamanio ya kupata watoto katika ndoa yao.

Hakimu Matrona Luanda wa mahakama hiyo ndiye aliyesoma hukumu hiyo baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili na kufikia uamuzi wa kuivunja ndoa hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa ndoa hiyo imeshindwa kurekebishika.

Luanda amesema, ndoa hiyo ilishindwa kurekebishika kwa sababu ilipita kwenye baraza la usuluhishi ambalo limepewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo chini ya kifungu cha 101.

Hakimu huyo amesema, katika ushahidi wake,Silaeli alidai kuwa alifunga ndoa na Kulaya Machi 18, 2006 na hawakubarikiwa kupata watoto na wala hawakuchuma mali yoyote, ambapo mume wake (Kulaya) alikasirishwa na kitendo cha kutopata watoto hivyo, mwaka 2011 walitengana.

Silaeli alipata mwanaume na kuzaa naye watoto wanne huku mwanaume (Kulaya) alipata watoto watatu, Hakimu amesema katika maelezo ya mdai (Silaeli) aliamua kuomba talaka kwa sababu hawaishi pamoja na mdaiwa kwa zaidi ya miaka 10.

Pia Hakimu huyo amesema, mdaiwa (Kulaya) alipoitwa aliieleza Mahakama kwamba ni kweli walifunga ndoa na waliamua kutengana ili kila mmoja akatafute watoto nje ya ndoa.
"Baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ilijiuliza maswali matatu je, mdai na mdaiwa walioana kwa ndoa, je? Ndoa imevunjika na imeshindwa kurekebishika na nani mshindi katika shauri hili,"amesema.

Amesema, mdai na mdaiwa walieleza Mahakama kuwa walioana kwa ndoa ya Kikristo Machi 18,2006 na pia mdai alieleza kuwa yeye na mwenzake hawakuwahi kuchuma mali yoyote wala kupata mtoto na kwamba tangu mwaka 2011 hadi leo hawaishi pamoja.

"Baraza la usuluhishi lilijadiliana kuhusu kesi hii na kushindwa kusuluhisha, kwa hiyo mdai ndiye mshindi katika shauri hili na kwa mamlaka niliyonayo ndoa hii imevunjwa hivyo, mdai apate talaka yake ndani ya siku 45 na haki ya rufaa kwa asiyeridhika ipo wazi,"amesema.

Mahakama imevunja ndoa hiyo chini ya kifungu cha 107 (2) (f) cha sheria ya ndoa na imepewa mamlaka ya kufanya hivyo chini ya kifungu cha 110 cha sheria hiyo.

Hata hivyo, mdai (Silaeli) ameeleza kuwa, yeye na mzazi mwenzake wa sasa, wanatarajia kufunga ndoa Novemba, mwaka huu jambo ambalo liliungwa mkono na mdaiwa ambaye alieleza kuwa atashirikiana naye kufanikisha ndoa hiyo mpya.

Silaeli akiwa nje ya Mahakama amesema kuwa,waliishi kwa miaka mitano na hawakupata watoto na kwa sababu matamanio yao ni kupata watoto waliamua watengane.

Amesema, tangu kipindi hicho mpaka sasa ndio wameamua kuja mahakamani kudai talaka ili kila mmoja abariki ndoa yake maana kila mmoja anafamilia yake.

"Nimefurahia hukumu hii kwa sababu naenda kubariki ndoa yangu Novemba, mwaka huu na mtu ambaye naishi naye sasa ili tuishi maisha ya kumpendeza Mungu na endapo mahakama ingeamua vinginevyo tungevumilia mpaka mwakani,"amesema Silaeli.

Pia amesema kwamba yeye na aliyekuwa mume wake hawana tatizo lolote kwani wanaishi vizuri na wanaendelea kuwasiliana kama marafiki wa kawaida.

Naye Kulaya amesema, ndugu zake hawakuwahi kuingilia kati ni kwa nini hawapati watoto badala yake walikaa wenyewe na kuamua kila mmoja akatafute mtoto ili kuepusha kugombana endapo mmoja wapo angepeleka mtoto wa nje ndani ya ndoa yao.

Kulaya amesema, wakati wanaishi pamoja walikuwa wameokoka na sio kwamba alikuwa na fedha au kumnyanyasa mke wake hivyo, yanayosemwa kwenye mitandao ya kijamii wanajifurahisha wenyewe.

"Tunaishi kwa amani kwani mwenzangu amejaliwa watoto wanne na mimi ninao watoto watatu na kabla ya ndoa ninao wengine wawili. Nakubaliana na maamuzi ya mahakama na wote tumeshinda katika kesi hii kwani hatukuwa na mali hivyo, tusingweza kugawana vyumba vya kupanga,"amesema Kulaya.

Post a Comment

0 Comments