🔴𝐋𝐈𝐕𝐄: Maziko ya Hayati Dkt.Magufuli wilayani Chato leo Machi 26, 2021 KWAHERI SHUJAA WA AFRIKA


Kwaheri Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli.

IBADA MAALUM YA MAZISHI YA HAYATI JPM KATIKA UWANJA WA MAGUFULI CHATO MKOANI GEITA

Msafara wa viongozi wanaosindikiza mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ulipokuwa ukiingia katika uwanja wa Magufuli uliopo Chato mkoani Geita tayari kwa ajili ya ibada maalum ya mazishi, huku viongozi mbalimbali wakihudhuria wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan.

Msafara wa viongozi wanaosindikiza mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ulipokuwa ukiingia katika uwanja wa Magufuli uliopo Chato mkoani Geita tayari kwa ajili ya ibada ya mazishi, huku viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakihudhuria.
Kutoka Chato mkoani Geita kwenye ibada maalum ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Tayari viongozi mbalimbali na wananchi wameshawasili katika uwanja wa Magufuli ambapo shughuli za ibada zitafanyika.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wabunge, wasanii pamoja na wananchi tayari wamefika katika uwanja wa Magufuli uliopo Chato mkoani Geita tayari kwa ajili ya ibada maalum ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Viongozi mbalimbali,wasanii na wananchi walianza kuingia katika viwanja vya Magufuli kuanzia majira ya saa 11 alfajiri tayari kabisa kushiriki ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Stanslaus Mabula mbunge wa jimbo la Nyamagana ni miongoni mwa wabunge waliofika Chato katika viwanja vya Magufuli kwaajili ya kumshiriki misa maalum ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mwili wa Hayati Magufuli umefika katika viwanja vya Magufuli majira ya saa 03;45 asubuhi na kupokelwa kwa Majozi makubwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Wabunge, wasanii pamoja na wananchi waliofika katika uwanja huo wa Magufuli.

Hayati Magufuli anatarajiwa kuzikwa leo wilayani Chato baada ya Ibada maalumu na Salamu mbalimbali kutolewa.
 
MKUU WA MAJESHI

Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF), Venance Mabeyo amesema kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vyombo vitaendelea kukulinda kama Rais, kukutii kama amiri jeshi mkuu na kutekeleza majukumu yetu kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo ameyasema leo Machi 26,2021 wilayani Chato Mkoani Geita kwa niaba ya Wakuuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa Ibada ya Mazishi ya Hayati Dkt.John Magufuli,Mabeyo amesema kuwa hali ya nchi ni shwari na wataendelea kuimarisha ulinzi.

CDF Mabeyo amesema kuwa vyombo hivyo vitaendelea kuonyesha uadilifu, utiifu na uaminifu kwake kama ilivyokuwa kwa awamu za uongozi zilizopita.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vinapenda kukuhakikishia kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vitaendelea kukulinda wewe, kukutii na kutekeleza majukumu yake aidha vinakuhakikishia utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kwako,” amesema CDF Mabeyo.
 
Mabeyo amesema kuwa tangu aingie madarakani mwaka 2015 Hayati Dkt. John Magufuli, alionesha kuviamini na kuvipenda vyombo vya ulinzi na usalama kwa dhati kubwa, alihakikisha kuwa anaviwezesha kwa mahitaji ya kiutendaji na kiutawala ili viweze kutekeleza majukumu yake.
 
“Upendo wake kwa vyombo vya ulinzi na usalama aliuonesha kwa namna ambavyo alivishirikisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya nchi yetu, alisema hatuwezi kuwa na vyombo imara bila kuwa na uchumi madhubuti”amesema Mabeyo
 
Hata hivyo amesema kuwa Vyombo vya ulizni vilishirikishwa katika shughuli zote za kiuchumi mifano michache ni ushiriki wetu wa kuulinda mgodi wa Tanzanite, kabla ya kuulinda lakini tulijenga ukuta kuzunguka mgodi huo pia katika kujenga uchumi ambapo aliwekeza kwenye miradi ya kimkakati na kuweka miundombinu bora.

Aidha Mabeyo amemuomba Rais Samia kuwatunuku nishani askari wanafunzi waliotakiwa kutunikiwa nishani hizo Machi 10, 2021 na Hayati Rais Magufuli

”Hayati Magufuli alitakiwa awatunuku nishani Februari 20 lakini kutokana na kazi zake tukasogeza mbele hadi Machi 6,alipomaliza ziara yake Dar es Salaam akaniambia hajisikii vizuri hivyo akaomba tusogeze hadi Machi 10 ili ajitazamie afya yake,” amesema Mabeyo
Aidha CDF Mabeyo amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ataitwa pia Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania na sio Amirat kama ambavyo ilipendekezwa,“Nashukuru Baraza la Kiswahili limerekebisha uendelee kuitwa Amiri Jeshi Mkuu na sio Amirat kama ilivyokuwa inapendekezwa”


Katika hatua nyingine amesema, Hayati Dkt.John Magufuli alionesha kuviamini na kuvipenda vyombo vya ulinzi na usalama kwani alihakikisha anaviwezesha kwa mahitaji ya utendaji na kiutawala ili viweze kutekeleza majukumu yake.

Ameyasema hayo leo Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo katika tukio la kuaga mwili wa hayati John Pombe Magufuli wilayani Chato.

Akizungumza katika tukio hilo Mabeyo amesema Hayati Magufuli upendo wake aliuonesha kwa namna ambavyo alivishirikisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya nchini.

“Vyombo vyetu vimeshirikishwa katika shughuli zote za kiuchumi mifano michache ni ushiriki wetu wa kuulinda mgodi wa Tanzanite, kabla ya kuulinda lakini tulijenga ukuta kuzunguka mgodi huo,"amesema Jenerali Mabeyo.
 
JAKAYA KIKWETE
 

Hayati Dkt.John Pombe Magufuli atakumbukwa kwa mengi hasa katika utendaji kazi wake kwani alikuwa hodari kuanzia alipokuwa Waziri mpaka alivyokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameyasema hayo leo Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete katika tukio la kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa hayati John Pombe Magufuli wilayani Chato mkoani Geita.

Akizungumza katika tukio hilo Mhe.Dkt.Kikwete amesema Magufuli alikuwa ni mmoja wa Mawaziri aliowaamini na kuwatumaini ndio maana alimuweka kwenye Wizara tatu zilizokuwa ngumu.

“Nilipokuwa Rais, Magufuli alikuwa ni mmoja wa mawaziri niliowaamini na kuwatumaini, alikuwa jembe langu. Ndio maana nilimuweka kwenye wizara tatu zilizokuwa ngumu ili anyooshe mambo”.Mhe.Dkt. Kikwete.

Aidha Mhe.Dkt.Kikwete amesema katika mchakato wa kupitisha majina ya wagombea Urais 2015 hakuweza kusita kulichagua jina la Magufuli kwani alifahamu fika utendaji kazi.

Amesema alishangazwa na maneno yaliyokuwa yanasemwa kuwa hampendi Magufuli kwani Magufuli ni mmoja wa viongozi ambao ambao alikuwa hana mashaka nae katika utendaji kazi wake.

“Akutukanae hakuchagulii tusi, kuna mengi yamesemwa, mara ooh.. JK hampendi Magufuli, jamani mimi ndiye nilimkabidhi ilani ya Uchaguzi labda JK mwingine”. Amesema Mhe.Dkt.Jakaya Kikwete.RAIS MHE. SAMIA ALIPOONGEA NA TAIFA WAKATI WA MAZISHI YA MTANGULIZI WAKE DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI WAKATI WA MAZISHI WILAYANI CHATO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongea na Taifa wakati wa mazishi ya mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kijijini Chato mkoa wa Geita Ijumaa Machi 26, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 26 Machi, 2021 ameongoza mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye amezikwa katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Wengine ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Ndg. Philip Mangula, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa mashirika na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali na wawakilishi kutoka sekta binafsi. Misa Takatifu ya Mazishi ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Gervas Nyaisonga aliyeambatana na Maaskofu na Mapadre na maziko yamefanyika kwa heshima zote za Kijeshi na Kidini.

Katika hotuba yake, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewashukuru wote waliohusika kushughulikia msiba huu uliolikumba Taifa tangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipofariki dunia tarehe 17 Machi, 2021 ikiwemo Kamati ya Mazishi ya Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, familia na Ofisi Binafsi ya Rais kwa kufanikisha uagaji wa mwili wa Marehemu katika sehemu zote ulizopita, mazishi ya Kitaifa yaliyofanyika Jijini Dodoma na hatimaye maziko yaliyofanyika Chato.

Mhe. Rais Samia amewashukuru viongozi wa ndani na nje ya nchi waliojitokeza kumsindikiza Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika safari yake ya mwisho na ameeleza kuwa ujio wao umedhihirisha mapenzi ya dhati waliyokuwa nayo kwake.

Ametoa pole kwa Mjane wa Hayati Dkt. Magufuli, Mama Janeth Magufuli, familia na wananchi wa Chato, na amewaihakikishia familia hiyo kuwa hatoitupa na wana Chato kuwa atahakikisha anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ahadi alizozitoa Hayati Dkt. Magufuli sio tu kwa wana Chato bali kwa Watanzania wote ikiwemo kufanyia kazi mchakato wa kuifanya Chato kuwa Mkoa endapo utakidhi vigezo. Mhe. Rais Samia amewataka Watanzania wote kuendelea kumuombea Hayati Dkt. Magufuli ili apumzike kwa amani na amesema japo kuwa mwili wake umezikwa lakini maono na mikakati yake ingali inaishi, hivyo ametaka kuwepo mshikamano na upendo kwa Taifa la Tanzania katika utekelezaji wake.

Viongozi mbalimbali waliopata fursa ya kutoa salamu wamemuelezea Hayati Dkt. Magufuli kuwa alikuwa kiongozi mchapakazi, mwenye maono, mwenye ubunifu na maarifa ya kutekeleza mipango mbalimbali hasa miradi ya maendeleo, mwenye upendo wa dhati, mkweli, aliyependa matokeo ya kazi, aliyemcha Mungu na aliyeipenda Tanzania kwa dhati.

Wameeleza imani yao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushamiri zaidi na zaidi, hivyo ni muhimu kwa kila Mtanzania kutoa ushirikiano wa dhati. Baada ya mazishi hayo, Mhe. Rais Samia ambaye ameongozana na mumewe Baba Hafidh Ameir amerejea jijini Dodoma.

Viongozi mbalimbali wakiweka mashada ya maua kwenye kaburi la Hayati Dkt.Magufuli
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Sita wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Taifa wakati wa ibada maalumu ya mazishi ya aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Chato Mkoani Geita, Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Sita wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka mchanga kwenye Kaburi la aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliefariki kwa maradhi ya Moyo tarehe 17 Machi na kuzikwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita Tarehe 26 Machi 2021 Mhe. Mama Janeth Magufuli , Mjane wa aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiweka mchanga kwenye Kaburi la mumewe wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake Chato mkoani Geita Tarehe 26 Machi 2021 Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mhe Dkt. Huseein Ali Mwinyi akiweka mchanga kwenye kaburi la aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mazishi yake kijijini chato Rais mstaafu wa awamu ya pili Mhe Ali Hassan Mwinyi akiweka mchanga kwenye kaburi la aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mazishi yake kijijini chato Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mkewe Mama Salima Kikwete wakiweka mchanga kwenye kaburi la aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mazishi yake kijijini chato Rais mstaafu wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mhe Dkt. Mohamed Shein akiweka mchanga kwenye kaburi la aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mazishi yake kijijini chato Watoto wa aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakielekea kuweka shada la maua kwenye kaburi la Baba yao. Mhe. Mama Janeth Magufuli , Mjane wa aliekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Bendera ya Taifa kuashiria heshima na kumbukumbu ya utawala wa awamu ya Tano wa Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Dkt. Magufuli Mwanamwema wa Afrika, Mwamba wa sekta ya Sanaa nchini

Kifo cha Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye alikuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si pigo tu kwa nchi, bali ni pigo katika tasnia ya Sanaa nchini.

Akitoa hotuba yake wakati wa mazishi ya Kitaifa ya Hayati, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwashukuru Watanzania kwa kuonesha umoja, mshikamano na upendo kwa kujitoa kwa moyo wakati wote tangu msiba utokee.

“Asanteni sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kumuaga kipenzi chetu, watu wametandaza nguo barabarani hii ni namna ya kuenzi utu wake, kazi zake alizofanya, uzalendo wake kwa taifa, maisha yake yote aliitanguliza Tanzania. Vizazi na vizazi watasimulia hadithi nzuri” alisema Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa aliwashukuru wasanii kwa kuendelea kuimba nyimbo za maombolezo ambayo yatadumu kwa  siku 21 tangu kutokea kifo cha mpendwa wetu Hayati Dkt. Magufuli.

“Wasanii endeleeni kutoa faraja kwa kipindi chote kwa kutoa hisia zenu na kuwashirikisha Watanzania kufarijiana wakati wa kipindi chote cha kumuaga kipenzi chetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Awamu ya Kwanza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitambua umuhimu wa Sanaa na utamaduni katika taifa kwa kusema,  “Utamaduni ni kiini cha taifa lolote, nchi isiyo na utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu wasio na roho ambayo inayofanya taifa.”

Sekta ya Sanaa ni  nguvu laini (soft power) ya kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli zote za kijamii ambapo sekta hiyo inasimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Ni dhahiri Dkt. Magufuli amekuwa Rais wa kwanza kuunda wizara yenye sekta ya sanaa inayojitegemea na kuwafanya wasanii watembee kifua mbele kwa kushiriki kazi mbalimbali za Serikali ikiwemo matamasha na dhifa za kitaifa.

Aidha, Hayati Dkt. Magufuli alijipambanua kwa kupenda kazi za Sanaa ambapo wakati wa uhai wake alipokuwa akitekeleza majukumu yake aliwatumia wasanii na kila mara alisikika akisema “Ni lazima wasanii wetu wanufaike na matunda ya kazi zao za Sanaa.”

Tangu kutangazwa msiba wa Hayati Dkt. Magufuli Machi 17, 2021, tumeshudia wasanii mbalimbali wakiandaa na kuimba nyimbo za maombolezo zinazosadifu utendaji kazi wake ambazo wanaendelea kuziwasilisha kwa jamii kwa umahiri mkubwa kwa kuwapa familia na Watanzania faraja.

Enzi za uhai wake akiwa kiongozi Mkuu wa nchi, katika moja ya hotuba zake Dkt. Magufuli akihitimisha Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma, Juni 16, 2020 alisema Sanaa ni sekta ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.   

“Sekta nyingine, ambayo haijasemwa sana lakini kwa sasa ina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu ni sanaa na utamaduni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2018, shughuli za Sanaa na Burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo ilikua kwa asilimia 13.7 na mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia 11.2, hongereni sana wasanii wetu mbalimbali, hususan wa Bongo Fleva na Filamu. Kazi zenu sio tu zinaburudisha na kuchangia ukuaji uchumi, lakini pia zinaitangaza nchi yetu kimataifa”, Hayati Dkt. Magufuli.

Katika maombolezo ya msiba huu, wasanii kupitia tungo zao wameonesha jinsi walivyoguswa wakisema Dkt. Magufuli amewaachia Watanzania majonzi, simanzi kwenye mioyo yao.

Moja ya wimbo waliotunga wasanii umebainisha kuwa kazi aliyoitiwa duniani Dkt. Magufuli ameimaliza, ametumika kikamilifu utumishi wake hautasahaulika nchini, nenda salama tutakukumbuka daima buriani Mwanamageuzi mahiri.

Wakati wa mazishi ya kitaifa yaliyofanyika Machi 22, 2021 Wasanii “Tanzania all-stars”  waliimba wimbo maalum usemao “Tusihuzunike bado tumaini lipo”, tutakukumbuka daima maana tulikupenda sana, pumzika kwa amani.”

Ujumbe wa wasanii hao unaonesha umahiri wa jinsi Dkt. Magufuli alivyoongoza nchi na kuheshimu kazi yake ya kishujaa, kijasiri na uhodari katika kufanya mapinduzi ya kweli katika sekta mbalimbali ikiwemo sanaa na kusema Watanzania wataikumbuka kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu.’

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni  Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hasaan Abbasi amesema “Katika uhai wake kama kuna kitu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikipigania na kukipangia kukipigania zaidi kikue zaidi ni sekta ya sanaa.

Katika kampeni zake wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, neno wasanii lilikuwa kinywani mwake sana, kiasi cha kuambatana nao kwenye kampeni zake. Taswira hiyo ilianza kuonekana tangu mwaka 2015 ambapo amekuwa Rais wa kwanza kuunda wizara yenye sekta ya sanaa kama sekta inayojitegemea.

“Leo hatuko naye mtu huyu Dkt. John Pombe Magufuli, bingwa katika kuipigania sekta ya sanaa, anapaswa kuimbiwa, nyimbo za maombolezo, nyimbo za kumwombea pumziko la amani na la milele. Hivyo Machi 25 kuanzia saa 10 kamili jioni hadi saa moja katika uwanja wa Magufuli hapa Chato tumewapa nafasi wasanii wote watakaoweza kufika Chato na waliokwishafika Chato kumuimbia Magufuli kwa nyimbo mbalimbali za maombolezo walizozitunga mmoja mmoja na kama makundi,” alisema Dkt. Hasaan Abbasi

Kwa kutambua na kuthamini kazi ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, baadhi ya wasanii wameshiriki kuimba kwa pamoja wimbo maalum wa maombolezo chini ya usimamizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Wasanii hao ni pamoja na Nandy, Marioo, Dogo Janja, Young Lunya, GoodLuck Gozbeth, Christina Shusho, Majid, JayMelody, Khadija Kopa, Mzee Yusuph, Mrisho Mpoto, Jesca Mshama, Linah, Hamadai, Whozu, Stamina, Merissa, Meja Kunta, Mzee Kalala na Ndelah.

Mwisho.

\
Post a Comment

0 Comments