Mbunge Mtenga:Tumeumia sana kuondokewa na shujaa wetu Hayati Dkt.Magufuli

Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amesema kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Magufuli si tu kwamba Taifa limempoteza shujaa bali limepoteza mzalendo namba moja ambaye alikuwa mstari wa mbele kuyalinda maslahi ya Taifa na kuwatetea wanyonge, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).
Amesema, kifo cha Hayati Dkt.Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini walikipokea kwa huzuni kubwa na majonzi.

"Kilikuja ghafla mno, Wana Mtwara Mjini walikuwa na mategemeo makubwa sana kutoka kwa Serikali yake, tutendelea kumuenzi na kumuombea,Taifa limempoteza Hayati Rais Dkt.John Magufuli ambaye alikuwa kiongozi hodari, shupavu na alikuwa mstari wa mbele kuyatetea maslahi ya Taifa.

"Tumeumia wengi sana, wana Mtwara Mjini wameumia sana, sasa jambo la msingi ni kuendelea kumuombea Hayati Dkt.Magufuli kwa Mwenyenzi Mungu ampe pumziko la amani. Pia tuendelee kuiombea familia yake, Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote, Mwenyenzi Mungu atupe faraja katika kipindi hiki kigumu kwetu,"amesema Mtenga.

Hayo aliyasema jijini hapa wakati akizungumza namna ambavyo wananchi wake walitamani ratiba ya kumuaga Hayati Dkt.Magufuli ingebadilishwa ili na wao waweze kupata nafasi ya kumuaga.

"Hayati Magufuli alikuwa ni changuo la wananchi na wote walimpa upendo kwa namna ambavyo alikuwa kiongozi wa kipekee, ndiyo maana walitamani hata kupata saa moja pale Mtwara Mjini waweze kumuaga mpendwa wao, lakini kutokana na wingi wa watu na ratiba, haikuwezekana, hivyo nimewaomba waendelee kumuombea kwa Mwenyenzi Mungu na hakika ndoto zake zote zitaenda kutimizwa kwa manufaa ya Watanzania wote,"amesema Mtenga.

Mtenga amesema, Hayati Dkt.Magufuli baada ya kuondoka duniani, ameacha msaidizi wake hodari katika nafasi ya urais ambaye ni Samia Suluhu Hassan, mama ambaye ni mchapa kazi na asiyependa mizaha katika mambo ambayo yanahusiana na Taifa pamoja na wananchi wake.

"Hivyo, tumpe Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan ushirikiano wa kutosha na tuendelee kumuombea maana, mafanikio na mipango ambayo alikuwa nayo Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli anakwenda kuisimamia na itatekelezeka kwa wakati maana wakati wote yote yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanatekelezeka kwa manufaa ya umma wote,"amefafanua Mtenga.

Post a Comment

0 Comments