Ndejembi:TAKUKURU ongezeni nguvu kesi za ubakaji na mimba za utotoni

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imetakiwa kuongeza nguvu kwenye kesi za ubakaji na mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikiminywa kwenye ngazi za chini na kusababishwa wahanga kukosa haki zao,anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo (kushoto) akimkabidhi muongozo wa TAKUKURU Naibu Waziri wa Nchi. Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Utawala na Utawala Bora,Deogratius Ndejembi leo Machi 2, 2021 baada ya kufungua mkutano huo jijini Dodoma. (Picha na Mwandishi DIRAMAKINI).

Naibu Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi ameyasema hayo leo Machi 2, 2021 wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU uliowakutanisha wakurugenzi,wakuu wa vitengo na watendaji wakuu jijini Dodoma.

Ndejembi amesema pamoja na TAKUKURU kushughulikia kesi nyingi na kuwasaidia wanannchi waliodhulumiwa,bado suala la kesi zinazohusu mimba za utotoni linawatesa wanafunzi wengi hali inayowanyima kuendelea na haki ya masomo yao.

“Nategemea na hili mtalimaliza na hatimaye watoto wetu waishi kwa amani bila kudhihakiwa kwenye jamii,ninaamini sana hasa ukizingatia mimi mwenyewe ni mnufaika wa TAKUKURU,bila ninyi kusimamia haki hata leo hii nisingesimama hapa,”amesema Ndejembi.

Pamoja na hayo Ndejembi ambaye amesema kuwa ni mnufaika wa taasisi hiyo yenye dhamana ya kupambana na rushwa amesema ikiwa mapambano ya rushwa ya ngono yatafanikiwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ongezeko la kesi za mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikimalizwa kimya kimya.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo ameeleza kuwa wao kama watendaji wenye dhamana ya kuisaidia jamii kuondokana na vitendo vya rushwa watahakikisha wanatumia muda wao wote kupambana na waovu wanaokandamiza watu kwa rushwa ya ngono.

Amesema,jamii inahitaji kuishi katika usawa hivyo taasisi hiyo kwa kuzingatia utumishi na utunzaji wa siri watashirikiana bega kwa bega na jamii kuhakikisha uovu wote unaotokana na rushwa unadhibitiwa.

Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa wa TAKUKURU, Bi.Sabina Seja. (Picha na Mwandishi DIRAMAKINI).

Naye Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa wa TAKUKURU, Sabina Seja amesema,TAKUKURU kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo itaendelea kusimamia kwa dhati kesi za rushwa ya ngono na kuwapa haki wahanga ambao mara nyingi ni wanafunzi wa vyuo vikuu na mashuleni.

“Tutapambana na kusimamia haki bila upendeo,hadi hali itakapokaa sawa,furaha yetu ni kuona jamii ikishi kwa amani bila vitendo vya rushwa kwa kuwa tunaamini rushwa ni adui wa haki hivyo ili haki itendeke lazima tushughulike na wala rushwa,”amesema.

Post a Comment

0 Comments