Rais Dkt.Mwinyi: Kifo cha Rais Magufuli kimeacha simanzi na huzuni kubwa kwetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kimeacha simanzi na huzuni kubwa katika mioyo ya wananchi wa Tanzania na wapenda amani kote Bara la Afrika, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Zanzibar).

Dkt. Mwinyi amesema hayo Uwanja wa Amani jijini hapa, katika hafla maalum ya kuuga mwili wa Hayati Dkt.Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2012.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa hafla ya kumuaga marehemu katika Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar leo 23/3/2021. (Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia wananchi wa Zanzibar katika hafla ya kuuaga mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na wananchi katika hafla ya kuuaga mwili wa Hayati Dkt.Jon Pombe Magufuli katika uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
Wananchi wa Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia wakati wa hafla ya kuuaga mwili wa Hayati Dkt.John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia wananchi wa Zanzibar katika hafla ya kuuaga mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Amesema, kuhusiana na kifo hicho, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar zimefanya juhudi kubwa kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa Kiongozi huyo.

Amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kujitokeza kwa wingi katika hafla ya kutoa heshima na kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli, huku akitoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na wana familia, huku akibainisha kuwa kifo hicho kimeleta simanzi na huzuni kubwa kwao kutokana na mapenzi makubwa walionayo kwa kiongozi wao.

Ameeleza kuwa, Watanzania wamepoteza kiongozi mahiri na mwenye kipaji katika Bara la Afrika, mwenye kijipambanua na mtetezi wa haki za wanyonge, sambamba na mwenye azma ya kudumisha Muungano wa Tanzania.

Amesema, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa Kiongozi mwenye maono makubwa ya kuhakikisha Taifa la Tanzania linapata maendeleo makubwa kupitia rasilimali zake.

Aidha, amesema Hayati Dkt. Magufuli atakumbukwa kwa kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi pamoja na kufanya juhudi ya kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa salama na utulivu.

Amesema, Watanzanaia watendelea kumkumbuka kiongozi huyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za wanyonge, aliyepigania rasilimali za Taifa na kupinga rushwa pamoja na kusimamia uwajibikaji katika utumishi wa umma, huku akibainisha kuwa ameiacha Tanzania ikiwa salama na amani na kuwa kigezo katika Afrika katika kila nyanja.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, Kiongozi huyo ni hidaya kutoka kwa Mungu, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuendelea kuyaenzi na kuyadumisha yale aliyoyaacha pamoja na kumtegemea Mungu kwa kila jambo.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha majonzi.

Amesema ni wajibu wa Watanzania wote kumomba Mungu ampe malazi mema kiongozi huyo pamoja na kubainisha azma ya Serikali anayoingoza ya kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kutumikia wadhalifa alionao, akibainisha uwezo mkubwa alionao kiongozi huyo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itampa kiongozi huyo kila aina ya ushirikiano ili kufanikisha malengo yaliowekwa, ikiwemo yale aliyoyaacha Hayati Dk. Magufuli.

Mapema, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliongoza mapokezi ya mwili wa Hayati Dk. Magufuli, uliowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume majira ya saa 3.15 za asubuhi ukitokea Mkoani Dodoma kwa ndege ya shirika la Ndege la Air Tanzania, kabla msafara wake kufikishwa Uwanjwa wa Amani kwa ajili ya kuagwa..

Nae, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa ambae Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi Kitaifa alisema Watanzania wanaendelea kupita katika kipindi cha huzuni kubwa, tangu kifo cha Rais Dk. John Pombe Magufuli kilipotokea Machi 17, 2021.

Alisema tukio la kuondokewa na Kiongozi mkuu wa Taifa alioko madarakani sio jambo la kawaida, akibainisha limetokea kutokana na kudra za Mungu, hivyo akawataka Watanzania waipokeee hali hiyo mbali na marajio makubwa waliyonayo.

Alisema mkusanyiko huo mkubwa wa wananchi ulioanzia Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume hadi Uwanja wa Amani unathibitisha huzuni waliyonayo wananchi hao kwa Kiongozi huyo.

Aidha, alisema mkusanyiko huo ni tukio linalotoa fursa kwa wananchi kupata nafasi ya kupita mbele ya Jeneza na kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu.

Waziri Mkuu Mjaaliwa alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, Wananachi pamoja na wanafamilia wa Marehemu Mmagufuli kwa msiba huo mzito na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu.
Mama Fatma Karume, Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani karume, akitoa heshima zake za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja leo Jumanne Machi 23, 2021.
 
Katika hatua nyingine, Viongozi mbali mbali wa dini na madhehebu tofauti hapa Zanzibar, akiwemo Mhashamu Askofu Agostino Shao kutoka Kanisa la Roman Katoliki, Askofu Michael Hafidh kutoka Kanisa la Anglikan pamoja na Kiongozi wa Dini ya Kihindu waliomba dua ya kumtakia malazi mema Marehemu ,sambamba na Naibu Kadhi wa Zanzibar Sheikh Othman Hassan Ngwali, alieomba dua kama hiyo kwa upande wa dini ya Kiislamu .

Katika hafla hiyo Viongozi mbalimbali wa Kitaifa walishiriki, akiwemo Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kasssim Majaliwa, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Makamo wa Pili wa Rais mstaafu Balozi Seif Ali Iddi, Mawaziri wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Mabalozi wa Tanzania walioko nchi za nje, Mabalozi wan je nchini Tanzania, Wanafamilia pamoja na viongozi wengine.
Taswira mbalimbnali za Maelfu ya wananchi wa Zanzibar wakiwa wamejipanga barabarani wakati mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Joseph Magufuli ulipokuwa unapelekwa Hospitali ya Jeshi katika kitongoji cha Bububu baada ya kuagwa na maelfu kwa maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Amaan wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi leo Jumanne Machi 23, 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news