Simba SC yasaka alama nne kuifuata Yanga SC kileleni

Simba SC kwa sasa wanatafuta alama nne tu kuweza kuwa sawa na watani wao Yanga SC katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dar es Salaam).
Ni baada ya Wekundu hao kuendelea kuwapa raha mashabiki na wapenzi wao kutokana na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Ni kupitia mtanange uliochezwa katika Dimba la Benjamin Mkapa Machi Mosi, 2021 lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

Chini ya Kocha Mfaransa, Didier Gomes Da Rosa anayesaidiwa na Mtanzania, Suleiman Matola Simba SC inafikisha alama 45 baada ya kucheza mechi 19, ingawa inabaki nafasi ya pili, ikizidiwa alama nne na Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi mbili zaidi.

Luis Jose Miquissone ameendelea kuwa nyota mwenye mchango mkubwa katika klabu hiyo baada ya kufunga bao moja na kutengeneza bao moja kipindi cha kwanza cha mtanange huo.

Kiungo huyo wa Kimataifa alianza kumtengenezea kazi nzuri mshambuliaji Mkongo, Chris Mutshimba Kope Mugalu kufunga bao la kwanza dakika ya nane.

Ni kabla ya yeye mwenyewe mchezaji huyo wa zamani wa UD Songo ya kwao, Msumbiji na Mamelodi Sundowns, Chippa United na Royal Eagles za Afrika Kusini kufunga la pili dakika ya 37 akimalizia pasi ya beki mzawa, Erasto Edward Nyoni.

Aidha, dakika ya 70 kipa namba moja Tanzania, Aishi Salum Manula wa Simba SC alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia kufuatia kugongana na mshambuliaji wa JKT, Daniel Lyanga na nafasi yake kuchukuliwa Beno David Kakolanya aliyekwenda kumalizia mtanange huo.
"Baada ya mchezo kuisha daktari ameniambia kuwa kila kitu kipo sawa, amepelekwa hospitali kufanyiwa vipimo na tunasubiri majibu. Manula ni mchezaji muhimu sana na nina uhakika ataweza kucheza Sudan,"Kocha Didier Gomes akizungumza kuhusu golikipa Aishi Manula ambaye alitolewa nje na kukimbizwa hospitali baada ya kuumia wakati mchezo ukiendelea.

John Raphael Bocco ambaye ni nahodha alihitimisha dakika ya 90 kwa kuipa klabu yake bao la tatu baada ya pasi ya mtokea benchi mwenzake, kiungo Rally Bwalya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news