TAKUKURU yamfikisha mahakamani Muuguzi kwa tuhuma za kuomba 200,000/- kwa mgonjwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Igunga mkoani Tabora imemfikisha mahakamani Mtumishi wa Idara ya afya katika hospitali ya wilaya hiyo, Wallace Kazili (52) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya sh.200,000 kutoka kwa mgonjwa, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Tabora).

Akisomewa mashitaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU wilayani humo, Mazengo Joseph amesema mshitakiwa ambaye ni mkazi wa mtaa wa Masanga kata ya Igunga mjini alitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha sheria na 11/2007 ya taasisi hiyo.

Ameieleza mahakama kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo Oktoba 30, 2019 akiwa muuguzi katika hospitali hiyo ambapo aliomba rushwa ya sh. 200,000 kutoka kwa Kasembe Bundara Nangale ili apatiwe dawa ya kifua kikuu (TB) kwa ajili ya mama yake mzazi aliyekuwa amelazwa hospitali hapo.

Mazengo amesema kuwa tarehe hiyo mshitakiwa alipokea kiasi cha sh. 50,000 kwa njia ya simu kama malipo ya awali ya sh 200,000 alizoomba na kuongeza kuwa Novemba 1, 2019 alipokea kiasi kingine cha sh. 50,000 kama sehemu ya malipo hayo pia na kufanya jumla kuwa sh. 100,000.

Mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo hivyo kesi hiyo kuahirishwa hadi Aprili 28, mwaka huu, mshitakiwa yuko nje kwa dhamana ya sh. 300,000 ambapo upande wa Jamhuri unategemea kupeleka mashahidi 6 mahakamani hapo.

Post a Comment

0 Comments