TANZIA: Mwandishi wa ITV akutwa amefariki, mwili wake watupwa njia panda ya ITV


Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni limethibitisha kutupwa kwa mwili wa aliyekuwa mwandishi wa habari ITV/Radio one na mtayarishaji wa kipindi cha Jarida la Wanawake, Blandina Sembu katika eneo la njia panda ya ITV na watu wasiojulikana waliokuwa wakitumia gari aina ya Noah, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Pia Kituo cha Runinga cha ITV kimeripoti taarifa za uthibitisho kuhusu kupatikana kwa mwili wa Blandina Sembu ukiwa umetupwa njia panda ya ITV, Mwenge mkoani Dar es salaam.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Ramadhan Kingai ameeleza kuwa walipata taarifa za mwili wa Blandina Sembu kutupwa mbele ya baa ya Maryland saa tano usiku.

Amesema, gari aina ya Toyota Noah ilifika katika eneo hilo na kusimama kwa muda mfupi kabla ya kutupa mwili wa Blandina akiwa tayari amefariki.

Kamanda Kingai ameeleza kuwa bodaboda waliokuwa wamepaki jirani na eneo hilo walishuhudia gari lililowashaa taa likisimama kwa dakika mbili kisha wakaona mwanamke ametupwa hapo.

“Uchunguzi unaendelea ila tulichobaini huyu mtu hakuuliwa pale, mauaji yalifanyika sehemu nyingine pale walienda kumtupa, amekutwa na majeraha usoni yanayoashiria alikuwa akijaribu kupambana kujitetea na hata jicho lake linaonekana alipigwa na kitu kizito,"amesema Kamanda huyo.

Post a Comment

0 Comments