Tunamzika Hayati Magufuli leo, lakini kuna jambo tunatafakari

Leo Machi 26, 2021 ni maziko ya Kitaifa kama si maziko ya Kimataifa ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Hayati Dkt.Magufuli alifariki jioni ya Machi 17, 2021. Hayo ikiwa ni kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kwa sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuapishwa Machi 19, 2021) kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma kuhusiana na kifo hicho wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo mkoani Dar es Salaam.

Kifo cha mzee wetu huyo, tunaweza kusema Watanzania wengi hatukitarajia maana kilikuja kwa ghafla mno, ni kifo ambacho kimewaumiza wengi kutokana na umahiri wa Hayati Dkt.Magufuli katika kuyatekeleza yale ambayo anayaamini kwa maslahi ya wengi au Taifa.

Watanzania waliweka imani kubwa kwake, kwa sababu waliona vitu vikitendeka kwa vitendo, makundi ya watu ambao walionewa nyakati fulani, yeye alikomesha tabia hiyo na kuweka usawa,vitu vilifanyika kwa wakati na haki ikatendeka kwa wote.

Tunapomsindikiza Hayati Dkt.Magufuli leo katika nyumba yake ya milele huko kijijini kwake wilayani Chato mkoani Geita, kuna baadhi ya mambo ambayo tunaguswa kuyasema na kuyashauri.

Mosi,ndani ya mifumo yetu ya Serikali tunadhani,kuna kasoro kidogo ambayo huenda inachangiwa na makundi ya watu, hali hii imesababisha mambo mengi ya Serikali tena yale ya siri kwa maslahi mapana ya Taifa, kuufikia umma kabla ya mamlaka zenye ridhaa ya kufanya hivyo kuwasilisha.

Wengi wetu, tumeshuhudia kabla kifo cha mzee wetu Hayati Dkt.Magufuli, tayari kuna taarifa zilikuwa zinasambaa zikidai mara Rais anaumwa sana, mara Rais amefariki.

Taarifa hizo zilizidi kuenea zaidi licha ya viongozi wakuu wa Serikali kuwataka Watanzania kuzipuuza taarifa hizo, kwa kuwa hazikuwa za kweli badala yake zilikuwa za uongo.

Aidha, mbali na angalizo hilo, watu hao hao kwa nyakati tofauti waliendelea kuzisambaza taarifa hizo kana kwamba wao ndiyo walikuwa na taarifa zaidi kuliko mamlaka husika.

Hali hiyo ilitoa taswira ambayo si njema kwa mamlaka zetu, kwani ilionekana kuna watu wa nje wana taarifa zaidi kuliko wale waliopo karibu na ngazi husika.

Mimi ninaamini katika njia moja tu ya kujenga na kuliweka Taifa letu katika hali ya uzalendo na nidhamu itakayotuwezesha kuwajibika kwa maslahi ya Tanzania na si kwa manufaa ya wenye maslahi binafsi.

Kwa msingi huo tunafikiri kuna haja kwa uongozi mahiri wa mama shupavu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan kwanza kabla ya yote kumtanguliza Mungu mbele, pili kuzifanyia baadhi ya taasisi nyeti ikiwemo inayohusika na mambo ya mawasiliano na usalama wa nchi mabadiliko.

Mabadiliko kwa maana gani? Ndani ya taasisi hizo kuna baadhi ya vitu haviendi sawa, huenda wapo watumishi ambao suala la maadili na uzalendo kwa Taifa hawaliwezi, kutokana na hali hiyo wanaweza kuwa chanzo cha kupenyeza taarifa nyeti za Serikali kwa watu ambao hawakupaswa ziwafikie, hatua ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa mambo yenye unyeti mkubwa kama yanayohusiana na Ikulu au Rais kuenea mitaani. Uwajibikaji kwa watakaobainika ndiyo tiba ya hilo tatizo.

Tanzania ni taifa lenye rasilimali nyingi za asili na zenye thamani kubwa, pale anapojitokeza mtumishi mmoja au wawili katika taasisi nyeti na kutoa siri za Serikali kwa maadui,analifanya Taifa letu kuwa katika hali mbaya.

Wito wetu kwa Watanzania,leo tunamzika kiongozi wetu Hayati Dkt.Magufuli ambaye tutaendelea kumuenzi na kumuombea kwa Mwenyenzi Mungu kutokana na mambo mengi makubwa aliyoyatenda kwa Taifa letu ndani ya kipindi cha miaka zaidi ya mitano akiwa Rais, lakini kubwa zaidi tuendelee kumuombea Rais wetu Samia Suluhu Hassan ili akatimize ndoto alizokuwa nazo mzee wetu.

Tunatambua mama yetu ni mpambanaji, lakini nguvu pekee ya kumuwezesha kuvuka changamoto kwa ajili ya kuliongoza Taifa letu kwa viwango bora ni sisi wenyewe kupiga magoti na kumuombea kwa Mungu, vivyo hivyo kufanya kazi kwa bidii.

Uogozi wa Diramakini kwa mara nyingine unatoa pole kwa familia ya Hayati Dkt.Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kwa kuondokewa na mpendwa wao. Mungu amlaze mahali pema. Amen.

Post a Comment

0 Comments