UN: Hongera Rais Samia, tutafanya kazi kwa karibu, kuisaidia Tanzania

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amempongeza, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (mashirika).
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres. (Picha na UN).

Ametoa pongezi hizo kupitia taarifa iliyotolewa mchana na msemaji wake,Stéphane Dujarric mjini New York nchini Marekani.

Katibu Mkuu amesema, anatarajia kufanya kazi kwa karibu na Rais Samia ikiwemo kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Rais Samia ameapishwa Machi 19, 2021 baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. Joseph Pombe Joseph Magufuli kufariki dunia Machi 17 kutokana na matatizo ya moyo.

Samia Suluhu Hassan anakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania. Samia anashika wadhifa huo baada ya kuhudumu kama Makamu Rais na kwa mujibu wa katiba, kufuatia kifo cha Rais Magufuli anatakiwa kisheria kushika wadhifa wa urais.

Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanasiasa wa chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) alizaliwa Zanzibar Januari 27, mwaka 1960. Aliianza safari yake ya kisiasa mwaka 2000 alipochaguliwa katika baraza la wawakilishi la Zanzibar kama mwakilishi wa kiti maalum na kuteuliwa na kushika wadhifa wa uwaziri na Rais wa Zanzibar wakati huo, Amani Karume, akiwa mwanamke pekee katika nafasi ya juu ya uwaziri katika baraza hilo la mawaziri.

Mwaka 2010, Bi Samia akaona ni vyema kuwania ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ambapo alishinda kiti cha Jimbo la Makunduchi kwa kupata asilimia 80 ya kura.

Safari yake katika uongozi wa serikali ilianzia pale ambapo alichaguliwa na Rais wa Awamu ya Nne Dkt.Jakaya Kikwete mwaka 2014 kuwa waziri wa nchi katika masuala ya Muungano. 

Wakati Tanzania ilipokuwa katika mchakato wa kujadili katiba mpya ya nchi alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa bunge la katiba na kushiriki jukumu muhimu la kuandika rasimu ya katiba mpya.

Samia alisoma katika shule za Ng’ambo na Lumumba mjini Unguja, baadaye alijiunga na Taasisi ya Utawala wa Fedha ZIFA kwa masomo ya takwimu. Baada ya masomo hayo aliajiriwa katika wizara ya mipango na maendeleo na baadaye kujiunga na Chuo kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro. 

Alihudhuria pia masomo ya juu katika chuo kikuu cha Manchester huko London, Uingereza na kupata shahada ya uchumi na pia amesoma katika chuo kikuu cha New Hampshire hapa Marekani.

Samia ni Makamu Rais wa kumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alishika wadhifa huu mara ya kwanza November 5, mwaka 2015, chini ya Rais John Magufuli.

Mwaka 2015 gazeti la Mshale liliandika kuhusu kupanda katika nyanja ya siasa za Tanzania kwa Bi Samia na kuuliza swali, “je mwanamke anaweza kupanda na kuwa rais katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki? Tusubiri tuone muda tutapata jibu gani".

Bi.Samia anatoa jibu kwa kushika wadhifa wa rais na kuwa mwanamke wa kwanza katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Samia aliolewa na Hafidh Ameir mwaka 1978, na kujaaliwa watoto wanne mmoja wa kike na watatu wa kiume. 

Aidha, ni mtoto wake wa kike Mwanu Hafidh Ameir ndiye aliyefuata nyayo za mama yake na kuwa mwakilishi katika baraza la wawakilishi Zanzibar.

Wakati huo huo, Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Zlatan Milišić, amempongeza rais wa sita wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania , Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa rasmi na kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania

Kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter mwakilishi mkazi huyo amesema , Umoja wa Mataifa nchini Tanzania uko tayari kufanya kazi na serikali yake na kumtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news