Wasioitakia mema Tanzania wamkera Waziri Mkuu, atoa neno kwa wanaomzushia Rais mabaya

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kushikamana, kudumisha amani na wapuuze kauli za chuki zinazotolewa na watu wasioitakia mema nchi kuhusu afya ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwani ni mzima wa afya, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Njombe).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kushiriki katika Sala ya Iijumaa kwenye Msikiti wa Ijumaa, Njombe mjini, Machi 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

”Tuendelee kufanya ibada na kupata mawaidha yanayohamasisha amani na utulivu. Rais Dkt. Magufuli ni mzima wa afya anaendelea na majukumu yake wakati sisi wasaidizi wake tukizunguka kuwahudumia wananchi. Leo nimezungumza naye na anawasalimia.”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Machi 12, 2021 baada ya kushiriki sala ya Ijumaa mjini Njombe, ambapo amesisitiza kuwa Rais anafanya kazi kulingana na mpango kazi wake. Amesema wananchi wanatakiwa kushikamana na kuifanya nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi waendelee kuliombea Taifa na wawapuuze baadhi ya Watanzania ambao hawapo nchini na wamekuwa wakitoa kauli za chuki kwa sababu hawapendi maendeleo ya nchi na wanatamani kuona Taifa likiporomoka.

”...Tuwapuuze baadhi ya Watanzania ambao wamejawa na chuki tu, wamejawa na husda tu na wanatamani kuwachonganisha na kutaka kushuhudua Taifa hili likiporomoka.”

”Kuanzia juzi hata leo asubuhi nimeona Watanzania wenzetu wenye husda tena hawako ndani wako huko wanashawishi vyombo vya Kimataifa viseme Rais wa Tanzania anaumwa kajifungia hizo ni chuki tu, husda tu.”

”Watanzania tulieni uongozi wenu upo imara na mafanikio tunayaona, kumzushia rais ugonjwa ni chuki, wanasema atoke aende wapi? Ulishamkuta siku moja anazurura Kariakoo? Rais ana mpango wake wa kazi si mtu wa kuzurura.”

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawasaidizi wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijijini na kwamba anafanyakazi kulingana na mpangokazi wake, hivyo amewataka Watanzania waendelee kuwa na amani huku wakiamini Serikali yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news