Waziri Jafo awataka watumishi wa umma kujiunga Mwalimu Commercial Bank

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo (Mb), amewataka watumishi wa kada ya ualimu na watumishi wengine wa umma kujiunga na Benki ya Biashara ya Walimu ijulikanayo kama ‘Mwalimu Commercial Bank’ ili waweze kunufaika na huduma zitolewazo na benki hiyo, abaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya kadi za Viza, Mwalimu Mobile na Mwalimu Wakala, Mhe Jafo amesema umefika muda kwa maafisa masoko wa benki hiyo, kuwatembelea watumishi walimu na wasio walimu kwa ajili ya kuwashawishi waweze kujiunga na benki ya Mwalimu.
Amesema walimu wengi wakijiunga na huduma za benki hiyo kutaiwezesha kukuwa zaidi, kwani kundi hilo linakadiriwa kuwa na watumishi laki tatu ambao ni asilimia 72.6 ya watumishi wote wa umma

“Kutokana na wingi wenu huu lazima muone ipo haja sasa ya kujiunga kwa wingi, lakini msiishie hapo tu, bali pia wafikieni watumishi wengine wa kada zingine, nalisema hili kwani najua nguvu ya walimu ni kubwa na hakuna la kuwashinda,” amesema.

Waziri Jafo amekumbusha kuwa malengo ya kuanzishwa kwa benki hiyo yalikuwa ni kuwahudumia walimu kama wateja wao wakuu lakini kufikia sasa idadi ya walimu waliojiunga kupata huduma za benki ni 41,000 tu.

“Hapa maafisa masoko bado mna kazi kubwa ya kujenga uelewa wa pamoja ili watu wafahamu kwamba hiki ni chombo chao,”amesema.

Akizungumzia kuhusu huduma mpya zilizoanzishwa na benki hiyo, Waziri Jafo amesema kuanzishwa kwa huduma hizo ni ishara kuwa huduma zitolewazo na benki hiyo zimeongezeka, hivyo ni jukumu la uongozi wa benki hiyo kuongeza hamasa na ushawishi kwa walimu na watumishi wengine wa umma kujiunga ili kufaidi huduma za benki hiyo.

“Uanzishwaji wa huduma hizi, ni ishara kwamba mmeongeza wigo, hata mtu ambaye alikuwa anasita kujiunga na benki yenu, sasa mmempatia suluhisho kwani kupitia huduma kama ya Mwalimu Mobile, mtu ataweza kufanya muamala eneo lolote lile alipo, hivyo tumieni mwanya huo kuwahamasisha walimu na watumishi wengine kujiunga zaidi,” amesema.

Waziri Jafo amesema kutokana na huduma za benki hiyo kutokuwa karibu na maeneo wanayofanyia kazi walimu hasa maeneo ya vijijini, baadhi ya walimu wanalazimika kuziacha kadi zao kwa taaasisi binafsi zinazotoa huduma za kifedha ili waweze kukopa mikopo mbali mbali, hivyo akaitaka benki hiyo kusogeza huduma karibu na walimu ili kuwawezesha kupata huduma ya benki hiyo.

Pia Waziri Jafo, ameitaka Bodi ya Benki ya Mwalimu kuona kwa namna gani wataweza kutoa mikopo kwa riba shindani na kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo ya Nyumba kwa wateja wao ili iwe kichocheo cha wateja wengi zaidi kujiunga katika benki hiyo.

Awali akitoa salamu kabla ya kumkaribisha Waziri Jafo, Mwenyekiti wa bodi ya benki ya Walimu Francis Ramadhan, amesema benki hiyo inazidi kuboresha huduma zao kwani tayari wana ofisi katika Mikoa ya Mbeya, Morogoro na Mwanza pamoja na sehemu za huduma zipatazo 2000 nchini kote pamoja na kuanzisha huduma ya Bima kwa wateja wake.

Mwalimu Commercial Bank, ilianzishwa mwaka 2012, na inamilikiwa na Chama cha Walimu kwa asilimia 51 ya hisa, huku wadau wengine ukiwemo Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) ambao unamiliki asilimia 16 na asilimia nyingine zilizosalia zinamilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NIHF na wadau wengine.

Post a Comment

0 Comments