Askofu Shoo:Viongozi mliokuwa na tabia ya kujiinua acheni

Kanisa la Kiinjili la Kilutheria Tanzania (KKKT) limewaonya baadhi ya viongozi waliokuwa na tabia ya kujiinua mithili ya nyoka aina ya kifutu na kuwataka kukaa mguu sawa mbele ya Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Kilimanjaro).

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dkt.Fredrick Shoo wakati wa mahubiri yake kwenye ibada ya Sikukuu ya Pasaka yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la KKKT usharika wa Moshi Mjini.

Dkt.Shoo amesema,upole na unyenyekevu siyo ishara ya udhaifu bali hekima na busara zinazoonesha nguvu na uwezo wa wanawake katika uongozi.

Pia amewapongeza wanawake na kusema sasa ni kipindi cha kuonesha kwamba unyenyekevu upo, lakini kusimama katika njia ambayo ni sahihi ambayo Mungu ndiyo anaitaka, ni jambo kubwa sana kuliko wale wanaojiinua na kujifanya vifutu.

Dkt.Shoo amempongeza mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira pamoja na wanawake wengine kwa kupewa roho ya upole na unyenyekevu, kwani kuna watu wanatafsiri upole kwamba ni udhaifu jambo ambalo siyo kweli.

"Upole na unyenyekevu siyo udhaifu, hata maandiko matakatifu hayajaandika hivyo, imani yangu ni kwamba Mungu ataendelea kuwapa nguvu wewe na wanawake wengine kushirikiana na Rais Samia,"amesema.

Wakati huo huo,Askofu Dkt.Shoo amempongeza Dkt.Mghwira kwa kuwakumbusha watu kuhusu uwepo wa Corona, kwani siyo wakati wa kudai kuwa ugonjwa huo haupo bali wananchi kushikilia mambo mawili ambayo ni kuchukua tahadhari na kumuomba Mungu.

Akizungumza kanisani hapo, Mkuu wa mkoa Dkt.Anna Mghwira ametaka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwani ni miongoni mwa mikoa iliyoathirika na ugonjwa huo sanjari na kuwapo kwa wagonjwa na vifo vingi bila kufafanua.

Dkt.Mghwira ametaka wananchi kutoacha tiba za asili ambazo zimethibitishwa na wataalam huku pia viongozi wa dini nao wakibeba jukumu lao la kufanya sala na maombi ili Mungu aweze kulinusuru taifa letu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news