Baraza la Wawakilishi wamuomba Makamu wa Kwanza wa Rais kuingilia kati suala la mazingira

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi imemuomba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kusimamia maslahi ya Zanzibar kwenye mazingira kutokana na miradi ya Kimataifa inayohusiana  na suala hilo kuingizwa kwenye mambo ya Muungano, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Akizungumza leo Aprili 2, 2021 kwenye Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais iliyopo Migombani mjini Unguja, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimwa Hassan Khamis Hafidh, amesema kwamba Zanzibar, ambayo ni nchi ya visiwa, inaathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, lakini imekuwa haifaidiki sana na miradi ya kimataifa moja kwa moja na inapofika inakuwa si kwa wakati.

"Makamu, tunakuomba sana suala hili mulione na mulizungumze, Ikibidi hata kama ni mgao unaotolewa kuhusu mazingira, basi utufike na utufike kwa wakati, Kwani hata huku Zanzibar wapo watu wenye weledi katika suala la kimazingira, lakini kama kuna changamoto, basi ndio eneo sahihi kwetu kuweza kujifunza,"amesema Mwenyekiti huyo wa kamati na ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la Welezo.

Mheshimiwa Hassan alielezea jinsi ambavyo kuingizwa suala la mazingira katika Muungano kunavyoikosesha Zanzibar fursa, misaada na miradi ya moja kwa moja, kwa kuwa shughuli zote zinazohusiana na suala hilo humalizika Tanzania Bara, na inapotokea kuletwa Zanzibar huwa ni kwa hatua za utekelezwaji tu. 

Kwa upande wake, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud, aliwaambia wajumbe hao waliokwenda kumtembelea ofisini kwake kwa ushauri kwamba ni kweli kuwa suala la mazingira ni sehemu ya Muungano kwa muda mrefu sana, ila akasema kuwa,  "Ni wakati sasa kuzungumzwa na kuweza kusawazishwa ili kila upande wa Muungano uweze kunufaika.”

"Kwa sasa inabidi tumtumie sana waziri wetu, Mheshimiwa Saada Mkuya, ili kututafutia wafadhili binafsi kutoka maeneo mbali mbali ya dunia ili nasi Zanzibar tuweze kunufaika moja kwa moja na miradi ya mazingira,” amesema Makamu huyo wa Rais, huku akiitaka kamati hiyo kuendelea kuwa karibu na ofisi yake ili iwe na msaada zaidi kwa wananchi wa Zanzibar. 

Mheshimiwa Hassan alisema Idara ya Mazingira, ambayo iko chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ni miongoni mwa idara muhimu sana kwa taifa kwani uwepo wa mazingira salama basi maisha nayo huwa salama.

"Mheshimiwa Makamu, tunakupongeza sana kwa kuona Idara hii ya Mazingira ipo kwako, maana tunaamini wewe na Waziri wako, Mheshimiwa Saada Mkuya, ni watu sahihi sana katika eneo hili, na bila shaka tunategemea mabadiliko makubwa,"amesema Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi. 

Kwa upande mwingine, Kamati hiyo kupitia mwenyekiti wake, Mheshimiwa Hassan, iliomba msaada zaidi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika kuzipa msukumo Tume ya Ukimwi Zanibar na Idara ya Kitaifa ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Zanzibar ili kuweza kupunguza na kuondoa kabisa matatizo hayo.

”Ukimwi na madawa ya kulevya yamekuwa yakipoteza sana nguvu kazi ya vijana wa taifa hili,” amesema Makamu wa Kwanza wa Rais akiongeza kwamba Ofisi yake inayachukulia masuala yote hayo kwa umuhimu mkubwa na kwamba muda wowote ipo tayari kutoa muongozo na usimamizi, isipokuwa akazidi kusisitiza mashirikiano na mshikamano. 

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi ilikutana na Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mashauriano na mazungumzo ya kikazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news