CCM yatangaza safu mpya chini ya Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan

Leo Aprili 30, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameshinda nafasi ya Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kura 1862 sawa na asilimia 100 ya wajumbe wote, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI (Dodoma).
Matokeo hayo yametangazwa jijini Dodoma katika Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa JAKAYA KIKWETE.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Mheshimiwa Job Ndugai ameyasema hayo ukumbini hapo wakati akitangaza matokeo huku kukiwa hakuna kura hata moja iliyoharibika.



Amesema, wajumbe wote ni 1862,waliopiga kura ni 1862 na hakuna kura iliyoharibika hivyo Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshinda kwa asilimia zote.

Mbali na hayo amesema, walioshinda nafasi ya NEC ni Happiness Mgongo kwa kura 839 na Rehema Simba kwa kura 867.

Ndugai amesema kuwa, katika mchakato huo wajumbe waliogombea nafasi ya NEC ya CCM ni sita, wanne wakiwa wanaume na wawili wakiwa wanawake.

"Hivyo hawa wanawake ndio wameshinda tulikubaliana 50 kwa 50 ila wanawake wamechukua asilimia 100 zote,”amesema.

Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko ya viongozi wake wakuu kitaifa ikiwemo nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa inashikiliwa na Bashiru Ally pamoja na nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi iliyokuwa inashikiliwa na Humphrey Polepole.

Katika mabadiliko hayo, CCM imempitisha Daniel Chongolo ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, huku nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ikichukuliwa na Shaka Hamdu Shaka.

Aidha, nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha,Frank George Hawasi anaendelea na nafasi yake huku Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ngebela Lubinga naye akiendelea.

Pia Katibu wa NEC Oganaizesheni ni Maurdin Kastiko ambapo chama kimesema, Pereira Silima atapangiwa majukumu mengine ya kitaifa.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Bara inachukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ambapo Rodrick Mpogolo atapangiwa majukumu mengine ya kitaifa.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Dkt.Abdallah Juma Sadala Mabodi kwa mujibu wa CCM anaendelea na nafasi yake kama awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news