CHADEMA wasusia uchaguzi mdogo Jimbo la Muhambwe

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Benson Kigaila amesema, chama hicho hakitashiriki uchaguzi mdogo katika Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dar es Salaam).

Ameyabainisha hayo leo Aprili Mosi, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuelezea maamuzi ya Kamati Kuu kwa madai kuwa, uchaguzi huo hautakuwa huru na haki.

Hayo yanajiri baada ya Tume ya Uchaguzi nchini (NEC) kutangaza kuwa uchaguzi huo mdogo katika jimbo hilo utafanyika Mei 2, 2021.

Kigaila amedai kuwa, miongoni mwa dosari zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ni baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa na wengine kunyimwa fomu za kuomba uteuzi za NEC ikiwemo mawakala kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura

Aidha, tayari Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemteua, Dkt.Florence Samizi kuwa mgombea wa nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.

Jimbo la Muhambwe liko wazi baada ya aliyekuwa Mbunge Mhandisi Atashasta Nditiye kufariki dunia Februari 12, 2021 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali ya gari iliyotokea Februari 10, 2021 eneo la Nane Nane jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news