Joseph Magufuli: Mama yetu (Janeth Magufuli) anaumwa

Mtoto wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, Joseph amesema mama yake, Janeth Magufuli anaendelea na matibabu baada ya kupata mshtuko kufuatia kifo cha mumewe kilichotokea Machi 17, 2021 jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Mtoto wa Hayati Dkt.John Magufuli, Joseph Magufuli. (Picha na Mwandishi DIRAMAKINI).

Joseph akizungumza leo Aprili 18, 2021 katika Kongamano la Viongozi wa Dini jijini Dodoma amesema mama yake hayupo vizuri kiafya, lakini anaendelea na matibabu.

“Mama hakuweza kuja kwa sababu ya tatizo la kiafya alipatwa na mshtuko baada ya baba kufariki, yupo anaendelea na matibabu, mama anawashukuru viongozi wa dini na watu wote kwa kuliombea Taifa wakati wote wa msiba na ilikuwa jambo gumu kumpoteza mzazi na kiongozi wa Taifa,"ameeleza Joseph.

Pia mtoto huyo ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili upendo, amani na mshikamano viendelee kutawala nchini.

Joseph amewashukuru viongozi wa dini na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wote nchini ambao walikuwa pamoja nao tangu walipompoteza baba yao hadi maziko.

"Nimekuja hapa kama mwakilishi, mama yangu (Janeth magufuli) hakuweza kuja kwa sababu ya tatizo kidogo la kiafya, mama alipata mshtuko baada ya baba yetu kufariki, yupo anaendelea na matibabu, anaendelea vizuri, anawashukuru sana Watanzania kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wote wa msiba wa baba yetu,"amesema.

Awali Mufti wa Zanzibar, Sheikh Al Kaabi amewataka Watanzania kuwa na utii kwa viongozi kwa kuwa wamepata bahati ya kuwa na viongozi wenye nia njema kwa ajili ya kuliongoza Taifa.

Sheikh Al Kaabi Akiwasilisha mada ya utii na uzalendo kwa umoja wa Taifa, amesema ni muhimu kila mmoja ampe haki mwenzake bila kutanguliza tofauti za kidini, itikadi na ukabila.

“Ni wajibu wetu kuwatii viongozi bila kujali ukubwa wala udogo wao.Tuna bahati nzuri tumepata viongozi wenye nia nzuri na makusudio mema kwetu na Tanzania nzima. Nikimzungumzia mama Samia ni kiongozi wa kwanza mwanamke, mwanamke ni mtu mwenye huruma na tunaamini mama Samia una huruma kwa wananchi wako

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amesema Hayati Dkt.John Magufuli alikuwa na utu, alijenga uadilifu, uaminifu kwa watendaji na wafanyakazi na alikemea maovu kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Mafunzo mengine aliyotuachia ni utu, alikuwa akiwajali watu, kuwasaidia wanyonge kupata haki zao, kuwaonea huruma lakini pia alikuwa na ukarimu kwa watu, kubwa sana na ambalo nimeona wasaidizi wake wakilifanya ni kujishusha ambayo ni silaha kubwa sana kwa nafasi uliyonayo.

“Pia alikuwa mstari wa mbele kutatua matatizo ya watu yaliyobana akayapa ufumbuzi, kujenga nidhamu yeye na aliyekuwa makamu wake wa rais na waziri mkuu walifanya kazi kubwa sana ya kutatua matatizo makubwa ya nchi,”amesema.

Post a Comment

0 Comments