MAAGIZO SITA YA RAIS SAMIA KWA TAMISEMI HAYA HAPA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo sita kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), huku akisisitiza ukusanyaji wa mapato na matumizi ufanyike kulingana na matakwa ya sheria na kanuni,anaripoti Nteghenjwa Hossesh (OR-TAMISEMI).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia mara baada ya kuwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi Ikulu jijini Dar es salaam Aprili 6, 2021.

Kauli hiyo ameitoa Aprili 65,2021 alipokuwa akiwaapisha Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi, Jijini Dar es Salaam.

“Nimemleta mwanamama madhubuti(Ummy Mwalimu) nimempa Katibu Mkuu mzuri na wasaidizi niimani yangu kazi itafanywa, najua TAMISEMI ni Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi na hiyo kazi inafuata hivi karibuni ili safu itimie na kazi iende kufanywa,”amesema Mhe. Rais Samia.

Akizungumzia kuhusu haki za wananchi, Mhe.Rais Samia amesema imezoeleka viongozi wa kitaifa wanapokwenda ziara hupokelewa na mabango ya wananchi wakilalamikia kero mbalimbali.

“Mabango mengine sio masuala au mambo ya kushughulikiwa ngazi za juu ni masuala ya kushughulikiwa huko chini kwa hiyo naomba tunapokuja huko tukikuta bango liwe masuala ya kitaifa lakini sio mambo yakushughulikiwa huko chini.”

“Nataka niseme bango moja aidha Mkurugenzi au Mkuu wa Wilaya amekwenda na hii haina maana mkazuie watu kuandika kero zao kwasababu najua tunapokuja watu wakija na mabango mnaenda mbio kuyakusanya na kuwanyuka watu na kuwapeleka mnapopajua nyie ili wasiseme yanayowasibu naomba kero za wananchi zishughulikiwe, tumekuja tumekuta bango moja Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi umekwenda na tukikuta malalamiko mnawafinya wananchi wasiseme hivyo hivyo tutashughulikiana,”amesema Mhe.Rais.

Aidha, amesema TAMISEMI ina jukumu la Afya ya watanzania na kuitaka kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya Afya na Elimu ili watanzania wapate fursa zaidi ya kuelimika na kupata huduma za afya

“Kwenye miundombinu ya elimu ni shule za sekondari za wasichana, zina bajeti maalum naomba zikasimamiwe, tunatarajia kujenga shule 26 hadi 2025 hili likatimie,”amesema.

Pia kuendelea kujenga hospitali za Wilaya, pia vituo vya afya na kumaliza maboma ya zahanati.
“Natambua kwamba kuna walimu 6000 au zaidi ambao wengine wameacha kazi, kustaafu, kufariki na sababu mbalimbali na inahitajika warudishiwe, hawa sio ajira mpya ni replacement, Utumishi mpo hapa pamoja na TAMISEMI naomba mkalitizame hilo, walimu 6000 warudishwe haraka ili wakatoe huduma kwa watanzania,”amesema.

Kadhalika, amesema upande wa afya kuna ajira za madaktari kutokana na ujenzi kukamilika wa Vituo vya afya na Hospitali na bajeti ya mwaka huu ni kuweka vifaa na watumishi.

“Kwa hiyo Utumishi na TAMISEMI muendele kuangalia hilo la watumishi na vitendea kazi kwenye huduma za afya na vilevile sekta ya elimu,”amesema.

Kadhalika, amesema Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA) imepewa kazi ya barabara za vijijini na kwamba kuna haja kubwa sana baada ya mvua kunyesha ya kutengeneza barabara lakini uwezo ni mdogo.

“Kuna Halmashauri zina uwezo mkubwa kifedha, TARURA na TAMISEMI angalieni mtakavyoshirikiana kama TARURA ina ukosefu wa fedha lakini Halmashauri zinafedha angalieni hilo na zile zitakazotoka Hazina zitaenda upande mwingine,”amesema.

Post a Comment

0 Comments