Makamu wa Kwanza wa Rais:Matatizo chaguzi ndogo yasituondoe kwenye matumaini

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amewaomba Wananchi kutokuyapa nafasi matatizo yaliyoshuhudiwa kwenye chaguzi ndogo mbili za hivi karibuni na kutokuvunja matumaini waliyonayo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na ukombozi wa kweli wa nchi yao, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Akizungumza na waumini wenzake wa dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Ijumaa leo Aprili 2,2021 katika Msikiti wa Kibweni, Bububu, kando kidogo ya kitovu cha Unguja Mjini, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais amesema kwamba Wazanzibari wote wanapaswa kuendelea kuvuta subira na kuzidi kukumbushana kwamba lengo kubwa la pamoja ni kuikomboa na sio kuiangamiza Zanzibar.

Katika chaguzi hizo mbili ukiwemo ule wa uwakilishi wa jimbo la Pandani kisiwani Pemba, ambao mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo alitangaziwa ushindi wa asilimia 52 na ule wa udiwani wadi ya Kinuni kisiwani Unguja, ambapo mgombea wa CCM alitangaziwa ushindi wa zaidi ya asilimia 80  kuliripotiwa matukio ya watu kupigwa.
 
Hata hivyo, Mheshimiwa Othman amewaambia waumini hao kwamba wachukulie kwamba chaguzi hizo ndogo lilikuwa ni jaribio na sio mtihani wenyewe.

"Jaribio linakuja kabla ya mtihani, na kufeli kwa jaribio haimaanishi kufeli kwa mtihani. Chaguzi ndogo zilizopita wiki moja nyuma ilikuwa ni jaribio kwetu, na sintofahamu zilizojitokeza katika uchaguzi huo wa Pandani na Kinuni zisitukatishe tamaa ya kufaulu mtihani wetu, Tuendelee kujenga imani, na tujipanga kwa ajili ya mtihani wetu,"amesema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Katika nasaha zake kwa waumini hao, Mheshimiwa Othman amewaambia yeye amebeba matumaini yale yale aliyokuwa nayo mtangulizi wake, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, na amewaomba waendelee kuwa na imani na subira.
"Najua wananchi wengi wanatamani kuona na wengine kusikia kwamba tutasema nini baada ya tukio hili. Ila niseme tu kwamba tuendelee kuwa wamoja na mshikamano na tujipange kwa mtihani wa ukombozi wa Zanzibar yetu,” amesema Mheshimiwa Othman.

Chaguzi hizo ndogo zilikuwa za kwanza kufanyika tangu kuundwa kwa serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar na kwa wengi ziliangaliwa kama kipimo cha jinsi moyo wa Maridhiano unaohubiriwa na viongozi wakuu wa nchi unavyoweza kufanya kazi katika mazingira ya ushindani wa kisiasa.

Profesa Omar Fakih Hamad alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa uwakilishi jimbo la Pandani, akirithi nafasi iliyowachwa wazi na Marehemu Abubakar Khamis Bakar, aliyefariki dunia wiki chache baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Post a Comment

0 Comments