MWALIMU MAKURU LAMECK AMPONGEZA RAIS SAMIA KURUHUSU VYOMBO VYA HABARI VILIVYOFUNGIWA VIFUNGULIWE

Mwalimu Makuru Lameck Joseph ambaye ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini Mkoa wa Mara, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuiagiza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa, anaripoti Amos Lufungulo (DIRAMAKINI) Mara.

Amesema, hatua hiyo ya Rais Samia ni ya kupongezwa kwani ina afya kwa Tasnia ya Habari na kwamba hatua hiyo inatoa dira katika kuthamini na kuheshimu Uhuru wa Vyombo vya Habari Nchini.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na DIRAMAKINI Mjini Musoma mara baada ya uamuzi huo kutolewa na Rais Samia katika Ikulu ndogo iliyopo jijini Ilala mkoani Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine Mwalimu Makuru amesema Rais Samia amejibu kilio chao.

"Nampongeza Rais Samia kutoa agizo la kufungulia Vyombo vya Habari ambavyo vilikuwa vimefungiwa. Kaonesha dhamira thabiti ya kuthamini mchango wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa Habari Kama ambavyo shauku hiyo imekuwepo kwa wengi,"amesema.

"Vyombo vya Habari vizingatie weledi na misingi ya kisheria Katika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha. Kama ambavyo Rais Samia kaelekeza, vyombo vya Habari vinamchango mkubwa kwa Maendeleo ya Nchi yetu, naomba viendelee kuthaminiwa kusudi vitekeleze majukumu yake kwa uhuru,"amesema Mwalimu Makuru.

Akizungumzia kuhusiana na Demokrasia Mwalimu Makuru amesema wananchi pia wanapaswa kuwa huru kuzungumzia kero, ufanisi na mapendekezo yao kwa viongozi wanaowatumikia pasipo kutishwa na mamlaka za kiserikali jambo ambalo litawezesha kupata mawazo mapya yatakayowezesha kuongeza hamasa ya uwajibikaji kwa viongozi katika kuimarisha juhudi za maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

"Kiongozi aliyepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi iwapo amefanya jambo jema lazima apongezwe kwa ubunifu wake na weledi katika kuwatumikia. Kama amefanya mambo yasiyofaa akikosolewa asichukie badala yake ayachukue mawazo anayopewa na ayafanyie kazi kwa manufaa ya Wananchi na siyo kujenga uadui nao kwani Taifa letu limejengeka katika misingi ya Demokrasia na Uhuru."amesema Makuru.

Pia, amemuomba Rais Samia kuichukua mipango mizuri ya watangulizi wake waliopita na aifanyie kazi, ili Wananchi wanyonge waendelee kuzidisha imani yao kwa Serikali na chama Cha Mapinduzi ambacho kimeendelea kuwaletea Maendeleo Watanzania.

Makuru amewaomba Watanzania wote kutoa ushirikiano wa dhati kwa Rais Samia na Serikali yake kusudi waweze kutekeleza azma ya kuwaletea maendeleo wananchi, huku akiwaasa viongozi katika maeneo mbalimbali Nchini, kutanguliza uzaoendo, uadilifu wanapotatua kero za Wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news