MWALIMU MAKURU LAMECK JOSEPH AWAPA NENO WATANZANIA

Watanzania wameombwa kushirikiana kwa dhati na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe.Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake, hasa kwa kuchapa kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla, anaripoti Amos Lufungulo (DIRAMAKINI) Mara.
Kada ya chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph. (Picha na Amos Lufungilo/ DIRAMAKINI).

Pia wamehimizwa kuzingatia ushauri wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliokuwa akiutoa kupitia hotuba zake mbalimbali wa kudumisha amani, umoja na utengamano wa kitaifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kauli hiyo imetolewa leo April Mosi, 2021 na Kada ya chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph wakati akizungumza na DIRAMAKINI ambapo pamoja na mambo mengine, amesema Taifa limepata bahati na heshima kubwa ya kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alifanya kazi pamoja na Hayati Magufuli akiwa Makamu wake kwa ufanisi mkubwa.

Hivyo amesema kila mmoja atarajie mafanikio thabiti katika nyanja za kiuchumi na kijamii kutekelezeka.

"Rais Samia amefanya kazi na Hayati Dakt.Magufuli akiwa Makamu wake na Miradi mingi mikubwa ya kimkakati imetekelezeka maeneo mbalimbali nchini, tulishuhudia hata katika Mkoa wetu wa Mara Hospitali kubwa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyojengwa kuanzia 1975 ikikamilika katika kipindi cha miaka mitano. Hiyo haitoshi ujenzi wa Miradi ya Hospitali za Wilaya umefanyika, uboreshwaji wa Shule kongwe Nchini zaidi ya 70 ulifanyika na Miradi mingi mikubwa imejengwa,"amesema.

"Hayo yote yalifanywa na Hayati Magufuli na Mama Samia Hassan wakiwa katika utekelezaji wa Ilani, mambo mengine mazuri tuyatarajie kutoka katika uongozi wake cha msingi tumuelewe anachotuelekeza na tukifanyia kazi kwa ufanisi na manufaa yetu. Akisema tufanye kazi lazima tuzingatie maelekezo yake na Viongozi wengine wa Serikali waliochini yake na tumuombee wakati wote kusudi utumishi wake uzidi kulistawisha Taifa kwa miaka atakayoliongoza,"amesema Mwalimu Makuru.

Aidha, Mwalimu Makuru amewaasa Mawaziri na Manaibu Waziri waliobahatika kuchaguliwa na Rais Samia kuhudumu katika kipindi hiki, wazingatie maelekezo anayowapa katika kuhakikisha wanawezesha Maendeleo ya Wananchi na Taifa.Na kwamba, dhamana waliyoipata waitumie vyema kuleta Mapinduzi ya kiuchumi na kijamii huku aliwaomba wamtangulize Mungu katika utumishi wao.

Katika hatua nyingine, Mwalimu Makuru amewahimiza Watanzania kuendelea kuthaminiana, kujaliana, kupendana, na kushikamana ili kuzidi kuudhihirishia ulimwengu kuwa Watanzania ni wamoja.

"Taifa letu lilijengwa katika misingi yenye falsafa ya uchumi wa kujitegemea tangu enzi la Baba wa Taifa. Hivyo tumuenzi Hayati John Pombe Magufuli Kama alivyokuwa akisema Nchi yetu inauwezo wa kujiendesha yenyewe bila kutegemea misaada Kutoka Nchi za Nje yenye masharti magumu isiyo na tija kwa maslahi ya Taifa,"amesema Makuru.

Post a Comment

0 Comments