Mwenyekiti CCM Mara akemea wanaomchafua Rais mstaafu Kikwete mitandaoni, awataka kuheshimu wazee wastaafu

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) amewataka wanaomtukana Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete katika mitandao ya kijamii kuacha mara moja kwani hayo si maadili ya Kitanzania huku akiwataka kuwaheshimu wazee wastaafu.
Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete (kushoto), kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3).

Kiboye ameyasema hayo mkoani hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mambo mbalimbali yanayohusiana na walivyojipanga kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kuanzia ngazi za chini hadi juu huku akigusia kuhusiana na tabia hiyo ambayo imezuka kwa sasa kwa baadhi ya watu kutumia mitandao ya kijamii kuwakejeli na kuwatukana viongozi wastaafu.

"Waache mara moja, Chama Cha Mapinduzi tuna maadili yetu, si maadili ya kusema sema ovyo kama watu wanaokaa vijiwe vya kahawa, kama mtu ana dukuduku au hoja yake anapaswa kuiwasilisha ngazi husika na si kuchafua viongozi wetu wastaafu. Hii tabia iliyozuka ya kumtukana Rais mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete katika mitando ya kijamii inakera sana.

"Hivyo ni wajibu wetu kama Watanzania kuendelea kudumisha mshikamano na umoja wetu huku tukiendeleza utamaduni wetu wa mdogo kumuheshimu mkubwa na mkubwa kumuheshimu mdogo, hii ni njia sahihi ya kuyaendeleza maadili yetu, kwani tukiendelea kuwachafua viongozi wetu wastaafu hatutakuwa tunajenga, bali tutakuwa tunaharibu,"amesema Kiboye.

Pia amesema, tabia hiyo ya kumchafua kiongozi huyo mstaafu haileti picha nzuri kwa Taifa ikizingatiwa kwamba aliwatumikia Watanzania katika nafasi ya urais ndani ya miaka 10 kwa bidii na unyenyekevu.

"Unapomtukana Mheshimiwa Kikwete, unawatukana Watanzania wote ambao walimpatia dhamana kwa kipindi chote cha miaka 10 ya urais,ni kweli wakati mwingine kila binadamu anaweza kuwa na mapungufu yake, lakini si vema kuongea ongea tu bila ukweli, tumpe heshima mzee wetu kama alivyotuheshimu sisi Watanzania, kama kuna mtu mwenye hoja kumuhusu, awasilishe ngazi husika iwe kwa chama mahali pengine na si kuandika mitandaoni kumchafua,"amesema Kiboye.

Mbali na hayo, Kiboye alisema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2020 hadi 2025 inaendelea kutekelezwa kwa kasi, huku akiwataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi za chini kuendelea kufuatilia kila kona ya mkoa ili pale watakapobaini changamoto waweze kuripoti kwa hatua zaidi.

Post a Comment

0 Comments