Naibu Waziri Waitara: Wakandarasi, wafanyakazi wa namna hii hatuwataki

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewaonya wakandarasi na wafanyakazi wababaishaji na wanaoidanganya Serikali kuwa wana sifa na vigezo lakini wanajenga barabara na madaraja chini ya viwango kuacha tabia hiyo mara moja.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akisisitiza jambo kwa menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (hawapo pichani), wakati alipotembelea na kufanya nao kikao kazi kilichofanyika katika ofisi za bodi hiyo, jijini Dodoma.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja chini ya viwango husababisha gharama kubwa kwa Serikali kutokana na kufanya matengenezo ya barabara mara kwa mara.

Naibu Waziri Mwita ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, katika kikao kazi na menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na kupokea taarifa ya Bodi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ameupongeza mfuko huo kwa namna unavyoweza kusimamia matengenezo ya barabara nchi nzima kwa uharaka unaoendelea kufanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Meneja wa Mfuko wa Barabara, Bw. Eliud Nyauhenga, akiwasilisha taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha kilichofanyika katika ofisi ya Bodi, jijini Dodoma.

Amezungumzia umuhimu wa wafanyakazi kutoa elimu sahihi kwa Jamie ili kuilinda miundombinu yote ya Barabara, Madaraja, Reli, Bandari, Vivuko na Viwanja vya Ndege ili idumu kwa muda mrefu.

“Tutahakikisha tunachujana humu humu ndani na ukigundua kuwa wewe sio mwenzetu ujitafakari mapema kabla sijakufikia, tunahitaji watumishi wazalendo na wakandarasi wenye sifa na weledi sio wababaishaji”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.Waitara amewataka watendaji kuongeza kasi katika maamuzi hasa pale inapotokea dharura ya madaraja na barabara kukatika na kusababisha wananchi kukosa huduma mbalimbali za kijamii.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa watumishi kutumia muda wao wa Serikali vizuri kwa kuleta michango chanya yenye ubunifu pamoja na kuweka mkazo katika kutatua changamoto za wananchi kwa haraka na kasi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, (mbele wa kwanza kulia), akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), mara baada ya kumaliza kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bodi hiyo kwa Naibu Waziri huyo, Meneja wa Mfuko wa Barabara Bw. Eliud Nyauhenga, amesema kuwa mfuko umeweza kufadhili tafiti mbalimbali zinazofanywa kwenye ujenzi wa gharama nafuu ili kujenga barabara nyingi zaidi na imara.

Nyauhenga, ameongeza kuwa Bodi imeendelea kutoa elimu kwenye ngazi zote kuhusu matumizi bora ya barabara ili kuilinda miundombinu hiyo na kupunguza gharama kubwa za matengenezo.

Naibu Waziri Waitara yupo katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Tanga yenye lengo la kujitambulisha, kuzifahamu taasisi zinazosimamiwa na Wizara yake, kukagua miradi pamoja na kuzungumza na wafanyakazi kuhusu mwelekeo wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news