Polisi wamshikilia mwanajeshi wa JWTZ kwa kumuua kwa kisu mke wake, madai ni kuchepuka

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia askari wa Jeshi la Wananchi kwa tuhuma za kumchoma kisu hadi kufa mke wake Fatuma Salumu (31) aliyekua mkazi wa Mwanalugali Kata ya Tumbi Wilaya ya Kibaha, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Pwani).

Mtuhumiwa mwenye namba MT 109695 PTE Godfrey Magiladi wa kikosi cha 36 KJ anadaiwa kumchoma kisu Fatuma kwa madai ya kutuhumiana kufanya tendo la ndoa nje ya ndoa yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa amesema tukio hilo limetokea Aprili 25, mwaka huu majira ya saa nne usiku huko eneo la Mwanalugali na Fatuma alikufa akiwa anakimbizwa kupatiwa matibabu katika hospitali ya Tumbi.

Wankyo amesema, mtuhumiwa amekamatwa baada ya tukio hilo mahojiano yanaendelea na ushahidi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa mmoja wa majirani amesema kuwa baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa alikimbia na kumuacha marehemu akiwa chini hadi wasamariawema walipojitokeza na kumkimbiza hospitalini.

Katika tukio lingine mwanamke 46 (jina linahifadhiwa) ambaye alikuwa mfanyabiashara wa pombe za kienyeji aliokotwa akiwa amefariki dunia.

Kamanda Wankyo amesema, kabla ya kifo cha mwanamke huyo Aprili 25,mwaka huu usiku wa manane akiwa na mama yake mzazi wakitokea katika klabu yao ya kuuzia pombe walirudi nyumbani na mama yake.

Amesema, baadae marehemu aliaga kutoka kwa mama yake kwenda kwake ambapo hakufika mpaka alipookotwa pembezoni mwa barabara akiwa amefariki dunia kwa kunyongwa shingo.

Jeshi la Polisi linawashikilia watu 17 wanaohusishwa na tukio hilo ambao wanaendelea kuhojiwa.

Kamanda Wankyo ametoa rai kwa wakazi wa mkoa wa Pwani kuacha kujichukulia sheria mkononi, kama kuna jambo linawakwaza walifikishe katika Mamlaka zinazohusika ili hatua zichukuliwe haraka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news