Rais Dkt.Mwinyi:Waajiriwa fanyeni kazi kikamilifu, msipofanya hivyo mnafanya dhuluma

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba kazi ni ibada hivyo amewataka wale wote walioajiriwa kufanya kazi watekeleze jukumu hilo ipasavyo na iwapo watafanya kinyume yake watakuwa wanafanya dhuluma, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Waumini wa Dini ya Kiislam Jijini Dodoma wakiitikia dua ikisomwa na Sheikh. Abdi Mussa (hayupo pichani) baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Tarawekh iliofanyika katika Masjid Nunge Jijini Dodoma jana usiku 22-4-2021(Picha na Ikulu) .

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Masjid Aljalil, Mbuzini, Wilaya ya Magharibi “A”, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika salamu hizo Alhaj Dk. Mwinyi aliwataka wale wote walioajiriwa kufanya kazi watekeleze majukumu hayo ipasavyo na watakapofanya kinyume yake watakuwa wanadhulumu kwani watakuwa wakilipwa mishahara ambayo hawaitendei haki.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Sheikh.Abdi Mussa baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Tarawekh iliofanyika katika Masjidi Nunge Jijini Dodoma, na (kushoto kwa Rais ) Bw. Yunus Suru na (kulia kwa Rais) Bw. Omar Kirasi.(Picha na Ikulu) .

“Kazi ni ibada, inapokuwa mtu anakulipa uwende ukafanye kazi uhudumie watu halafu wewe unakwenda kazini si kwa nia ya kufanya kazi bali ni kwa nia ya kuonekana basi unadhulumu, na unawadhulumu wale ambao wana haki ya kupata huduma zako na unaidhulumu nchi kwa jumla inayokulipa mshahara”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya wamafanyakazi katika sekta ya umma hawatekelezi majumuku yao uipasavyo hivyo, alisisitiza kwamba ni vyema wakafanya kazi kama taratibu zilivyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa muda waliopangiwa.

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba maendeleo hayawezi kupatikana iwapo kutakuwa na dhulma ambayo haionekani kwani Serikali imeweka wafanyakazi ili kupata maendeleo.

Alisisitiza kwamba kila mmoja ajione ana wajibu mbele ya Mola wake wa kufanya kazi kwani kazi ni sehemu ya ibada katika kutekeleza jukumu hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Sheikh.Abdi Mussa (hayupo pichani) baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Tarawekh, iliofanyika katika Masjid Nunge Jijini Dodoma na (kulia kwa Rais) Sheikh.Omar Kirasi na (kushoto kwa Rais) Sheikh Yunus Suru, wakiitikia dua.(Picha na Ikulu)

Aliongeza kwamba ibada si kwenda misikitini peke yake bali ibada ni hata kufanya kazi na kuilisha familia yako kwa kipato cha halali.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuimarisha na kuidumisha amani kwani dunia hivi leo ni kama kijijini na inatosha kuona jinsi nchi nyengine kama vile Somali, Siria na Iraq watu hawawezi kukusanyana kufanya ibada.

Alieleza kwamba yanayotokea nchi nyengine siziso na amani ni fundisho tosha kwa wananchi wa Zanzibar, hivyo ni vyema wakaendelea kuidumisha amani waliyonayo.

Alisema kuwa umoja ni muhimu kwani ndio unaodumisha amani hivyo, bila ya umoja amani itatetereka na dini ya Uislamu imekwua ikiwataka waumini kuwa wamoja, kuvumiliana na wote kuwa ndugu.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba kipindi kiliopo hivi sasa nchini ni kipindi chenye umoja ambapo mifarakano imeondoka kabisa hivyo, ni wajibu kwa kila mmoja kuhakikisha hali hairejea kama ilivyotokea hapo siku za nyuma.
Sheikh Abdi Mussa akisoma dua baada ya kumaliza kwa Ibada ya Sala ya Tarawekh iliofanyika katika Masjid Nunge Jijini Dodoma.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dk. Mwinyi amewasihi wananchi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu kutokana na jukumu zito alilokabidhiwa la kuwaongoza watu kwa haki ambalo linahitaji msaada na dua kwa wingi, hivyo katika mwezi huu wa Ramadhani wamuombee ili atekeleze aliyoyatolea ahadi na aliyoyadhamiria katika nafsi yake kuwasaidia Wazanzibari.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti huo Sheikh Mohammed Omar Ali alieleza umuhimu wa kuimarisha amani hapa nchini kwani ni neema adhimu ambazo Mwenyezi Mungu amewawezesha Wazanzibari.

Aliongeza kwamba watu wengi hawaujui umuhimu wa amani kwani bado amani ipo nchini na wananchi wa Zanzibar hawajawahi kupita katika kipindi cha kukosa amani.

Hivyo, alisisitiza umhimu wa amani na kueleza kwamba bila ya kuwa na amani watu hawawezi kufanya ibada misikitini, kufunga pamoja na kutekeleza nguzo ya hija na kutekeleza shughuli za maendeleo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na Viongozi wa Masjid Nunge Jijini Dodoma baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Isha na Tarawekh, iliofanyika katika msikiti huo.(Picha na Ikulu).

Aidha, Sheikh Mohammed Omar alieleza umuhimu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuweza kusaidiana kwani huu ni mwezi wa kuzidisha kutoa na kutodhulumiana.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alifika nyumbani kwa Bi Zuwena Ali hapo hapo Mbuzini, ambaye ni mgonjwa na kumjuulia hali yake pamoja na kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu ampe afya njem.

Post a Comment

0 Comments